Tafuta

Askofu mteule Balthazar Ntivuguruzwa wa Jimbo Katoliki la Kabgayi nchini Rwanda Askofu mteule Balthazar Ntivuguruzwa wa Jimbo Katoliki la Kabgayi nchini Rwanda 

Askofu Balthazar Ntivuguruzwa wa Jimbo Katoliki Kabgayi, Rwanda

Askofu mteule Balthazar Ntivuguruzwa wa Jimbo Katoliki Kabgayi alizaliwa tarehe 15 Septemba 1967, Wilayani Muhanga. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 18 Januari 1997 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Kabgayi. Katika maisha na utume wake kama Padre amewahi kuwa Gaimu Gambera, Paroko-usu, Katibu wa Askofu Jimbo, Jaalimu na mwalimu wa taaluma na Gambera wa Taasisi ya elimu ya juu ya Kikatoliki Kabgayi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la kung’atuka kutoka madarakani lililowasilishwa kwake na Askofu Smaragde Mbonyintege wa Jimbo Katoliki la Kabgayi, nchini Rwanda. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteuwa Mheshimiwa Sana Padre Balthazar Ntivuguruzwa wa Jimbo Katoliki Kabgayi kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Kabgayi. Hadi kuteuliwa kwake, tarehe 2 Mei 2023 Askofu mteule Balthazar Ntivuguruzwa alikuwa ni Gambera wa Taasisi ya Elimu ya Juu ya Kikatoliki Kabgayi. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Balthazar Ntivuguruzwa wa Jimbo Katoliki Kabgayi alizaliwa tarehe 15 Septemba 1967, Wilayani Muhanga. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 18 Januari 1997 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Kabgayi.

Baraza la Maaskofu Katoliki wakiwa na Papa Francisko
Baraza la Maaskofu Katoliki wakiwa na Papa Francisko

Tangu wakati huo kama Padre, amewahi kufanya utume wake kama: Kaimu Gambera na Mwalimu Seminari Ndogo ya Kabgayi kati ya Mwaka 1997-2000. Katibu muhtasi wa Askofu Jimbo la Kabgayi kuanzia mwaka 2000-2003. Baadaye akatumwa nchini Ubelgiji kujiendeleza zaidi na hatimaye akajipatia Shahada ya Uzamivu mintafaru Maadili kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Luvain, “Université Catholique de Louvain.” Alibahatika kuwa Paroko-usu wa Parokia ya Saint-Rémy na Sainte-Renelde, Jimbo kuu la Malines-Bruxelles kati ya mwaka 2003-2010. Aliporejea Jimboni mwake, aliteuliwa kuwa Jaalimu na Mwalimu wa Taaluma, Seminari kuu ya Nyakibanda kati yam waka 2010 hadi mwaka 2017. Tangu mwaka 2017 hadi kuteuliwa kwake, tarehe 2 Mei 2023 Askofu mteule Balthazar Ntivuguruzwa alikuwa ni Gambera wa Taasisi ya Elimu ya Juu ya Kikatoliki Kabgayi.

Uteuzi Rwanda
03 May 2023, 16:02