Tafuta

Injili ya maisha itashinda dhidi ya kifo; Injili ya upendo, itashinda utamaduni wa chuki na uhasama na kwamba, wema utashinda ubaya!  Χριστὸς Ἀνέστη! Kristo Amefufuka! Injili ya maisha itashinda dhidi ya kifo; Injili ya upendo, itashinda utamaduni wa chuki na uhasama na kwamba, wema utashinda ubaya! Χριστὸς Ἀνέστη! Kristo Amefufuka!  (AMIR COHEN)

Ujumbe wa Pasaka Kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa Kwanza: Ushindi wa Kristo Mfufuka

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, katika tafakari yake ya Sherehe ya Pasaka anagusia: Mateso ya Ijumaa Kuu na Furaha ya Ufufuko wa Bwana, yaani Msalaba na Ufufuko wa Bwana. Wakati huu Fumbo la Pasaka linabeba uzito wa pekee, pengine kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mwanadamu kutokana na walimwengu kuendelea kuelemewa na utamaduni wa kifo pamoja na nyakati za giza na madhulumu mbalimbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo aliyeteswa, akafa na hatimaye kufufuka kutoka wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya: Imani, upendo, matumaini, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kumbe, Fumbo la Pasaka ni sababu na kiini cha imani, furaha na matumaini ya Wakristo hapa duniani kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake Kristo Yesu amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kumkirimia maisha ya uzima wa milele, mwaliko wa kudumisha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Pasaka ya Kristo ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na mauti
Pasaka ya Kristo ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na mauti

Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliweza kugeuza ubaya kuwa ni chemchemi ya historia ya wokovu kwa watu. Upendo wa Mungu unaendelea kububujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotobolewa na kubaki wazi, chemchemi ya Sakramenti za Kanisa na faraja kwa watu waliokata tamaa na kuendelea kuteseka, hasa nyakati hizi za shida na mahangaiko makubwa kutokana na vita, majanga asilia pamoja na magonjwa ya milipuko. Kwa njia ya huruma na upendo wa Mungu, waamini wamepewa matumaini mapya. Hii ni changamoto kwa waamini kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka kwa njia ya maisha yao! Wakristo wa Makanisa ya Mashariki wanaadhimisha Pasaka ya Bwana, Dominika tarehe 16 Aprili 2023. Ni katika muktadha huu, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, katika tafakari yake ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2023 anagusia: Mateso ya Ijumaa Kuu na Furaha ya Ufufuko wa Bwana, yaani Msalaba na Ufufuko wa Bwana. Wakati huu Fumbo la Pasaka linabeba uzito wa pekee, pengine kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mwanadamu kutokana na walimwengu kuendelea kuelemewa na utamaduni wa kifo pamoja na nyakati za giza na madhulumu mbalimbali.

Fumbo la Pasaka liwe ni chemchemi ya matumaini
Fumbo la Pasaka liwe ni chemchemi ya matumaini

Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha ufunuo wa huruma, upendo, msamaha, umoja na mshikamano unaovunjilia mbali vita, migogoro na kinzani. Na matokeo yake, watu wengi wanasongwa na upweke hasi na kifo. Mwanga wa Fumbo la Pasaka, ni kielelezo cha imani na matumaini mapya; wokovu na upatanisho; furaha na uchungu katika maisha. Huu ni uzoefu wa Ijumaa Kuu na Kesha la Pasaka na hatimaye, Pasaka yenyewe. Fumbo la Msalaba na Kilima cha Golgota ni sawa na chanda na pete, kamwe haviwezi kutenganishwa. Mji wa Yerusalemu una umuhimu wake kijiografia na pia katika Liturujia ya Kanisa, mwaliko kwa sasa ni kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. “Watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu, nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti mwanga umewazukia.” Mt 4:16. Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu linawakirimia watu wa Mungu, mang’amuzi, maono na mwelekeo mpya wa maisha. Ni katika muktadha huu, waamini wanaweza kuona kazi ya Uumbaji kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni mwanga angavu unaofukuzia mbali giza katika nyoyo za watu na ulimwengu katika ujumla wake. Ujumbe mahususi kwa watu wote wa Mungu anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, anapohitimisha tafakari yake ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2023 ni huu, Injili ya maisha itashinda dhidi ya kifo; Injili ya upendo, itashinda utamaduni wa chuki na uhasama na kwamba, wema utashinda ubaya!  Χριστὸς Ἀνέστη! Kristo Amefufuka!

Pasaka Makanisa Mashariki
15 April 2023, 15:18