Tafuta

Nguvu ya sala katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Nguvu ya sala katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko.  (Vatican Media) Tahariri

Nguvu ya Sala Katika Maisha na Utume wa Papa Francisko: Maana ya Sala

Papa Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameendelea kujiaminisha kwenye sala na maombezi ya watu wa Mungu, tangu siku ile alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, tarehe 13 Machi 2013. Kuomba sala na maombezi ya waamini, ukawa ni mtindo wa maisha anaoendelea kuushuhudia katika nyaraka na mikutano yake na watu mbalimbali. Watu wengi nao wamejiaminisha katika sala na maombi yanayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika shida zao

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, sala ni kuinua moyo na kutazama kuelekea mbinguni. Ni mlio wa shukrani katika majaribu na furaha. Unyenyekevu ndio msingi wa sala kwa sababu mwanadamu mbele ya Mwenyezi Mungu, daima ni mwombaji. Sala ni jibu la imani kwa ahadi ya bure ya wokovu, jibu la mapendo kwa kiu ya Mwana wa pekee wa Mungu. Ni moyo ndio unaosali, kama moyo uko mbali na mwenyezi Mungu, tendo la sala ni bure. Moyo ni mahali anapoishi mtu na kiini kilichofichika, kisichoweza kufikiwa na akili ya kibinadamu. Moyo ni mahali pa kufanyia maamuzi mazito katika maisha; kifo au uhai, ni mahali pa kukutana na Mwenyezi Mungu; mahali pa agano. Sala ya Kikristo ni uhusiano na Agano kati ya Mungu na mtu katika Kristo. Kimsingi, sala ni tendo la Mungu na la mwanadamu linalobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu na kutoka kwa mwamini, yote ikielekezwa kwa Baba katika umoja wa utashi wa kibinadamu wa Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili. Katika Agano Jipya, Sala ni uhusiano hai wa watoto wa Mungu na Baba yao mwema bila mipaka, na Mwanaye Yesu Kristo pamoja na Roho Mtakatifu. Neema ya Ufalme ni “Umoja wa Utatu Mtakatifu yote kabisa pamoja na roho wote kabisa. Maisha ya sala ni desturi ya kuwa mbele ya uwepo wa Mungu Mtakatifu mara tatu na katika umoja naye. Umoja huo wa maisha unawezekana siku zote kwa sababu, kwa Ubatizo, waamini wamekuwa kitu kimoja na Kristo Yesu. Sala ni ya Kikiristo kwa sababu ni umoja na inaenea katika Kanisa, ulio mwili wake. Mapana yake ni yale ya upendo wa Kristo. Rej. 2559-2597.

Papa Francisko amesimika maisha na utume wake katika nguvu ya sala
Papa Francisko amesimika maisha na utume wake katika nguvu ya sala

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha yake na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameendelea kujiaminisha kwenye sala na maombezi ya watu wa Mungu, tangu siku ile ya kwanza alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, tarehe 13 Machi 2013. Kuomba sala na maombezi ya waamini, ukawa ni mtindo wake wa maisha anaoendelea kuushuhudia katika nyaraka na mikutano yake na watu mbalimbali. Hata watu wengi nao wamejiaminisha katika sala na maombi yanayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Wengi wameshangazwa kuhusu kumbukumbu yake, wanapomwomba kuwakumbuka katika sala na sadaka yake. Huu ni ushuhuda wa mchakato wa ujenzi wa ujirani mwema na ukaribu kama Kristo Yesu anavyofundisha. Hivi ndivyo anavyoandika Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu, nguvu ya sala na mwaliko wa Baba Mtakatifu Francisko kumkumbuka katika sala na kuendelea kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu tarehe 13 Oktoba 2013 katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican alifafanua kuhusu ujasiri na udumifu katika maisha ya sala; Jinsi ya kusali vyema na hivyo kuondokana na tabia ya kusali kwa mazoea, ili kujipatia neema na baraka, kwani ujasiri na udumifu katika sala ndiyo sala yenyewe, kwani mwamini anaamini kwamba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anasikiliza sala ya mja wake na atamjibu kwa wakati wake,  kwani Kristo Yesu anasema, “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.” Mt 7:7.

Sala ya watu wa Mungu ina nguvu katika maisha na utume wa Papa
Sala ya watu wa Mungu ina nguvu katika maisha na utume wa Papa

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kusali na kuomba; kutafuta na kubisha, ili kuweza kupata neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Katika kipindi cha miaka kumi ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kusindikizwa kwa sala za waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Ameendelea kujipambanua kuwa yeye pia ni mtu was ala. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake. Sala, Sadaka na Maombi ni zawadi kubwa ambazo, kila mwamini katika hali yake, anaweza kumpatia Baba Mtakatifu Francisko, kama ilivyojitokeza hivi karibuni, alipokuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma. Moyo usiokuwa na shukrani hukausha mema yote. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya Matawi, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewashukuru waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema waliomsindikiza kwa sala na sadaka zao, wakati alipokuwa anaumwa na hatimaye kulazwa!

Papa Nguvu ya Sala

 

03 April 2023, 15:15