Sinodi,Tume ya maandalizi ya mkutano mkuu imeanzishwa
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Kuna wajumbe saba, akiwemo mtawa mmoja, katika Tume ya matayarisho ya utekelezaji wa mkutano mkuu wa kawaida wa Sinodi. Baraza hilo, lililoanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 10, ya kifungu cha 1-2 cha Katiba ya Kitume Episcopalis Communio, imeundwa tarehe 15 Machi 2023 na itaongozwa na Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi ya Maaskofu.
Wajumbe
Wajumbe wa tume hiyo ni: Padre Mjesuit Padre Giacomo Costa, mratibu; Askofu Mkuu Timotheo John Costelloe; Askofu Mkuu Daniel E. Flores; Sr. Shizue Hirota; Monsinyo Lucio A. Muandula; Profesa Dario Vitali. Katibu ni Askofu Tomasz Trafny. Mjumbe mkuu wa Sinodi, Kardinali Jean-Claude Hollerich, pia atashiriki katika kazi ya Tume. Sambamba na kuanzishwa kwa Tume ya maandalizi, Sekretarieti ya Sinodi ilipendekeza kuwa Jumatano tarehe 31 Mei, 2023 katika ukumbusho wa kiliturujia wa Siku Kuu ya Bikira Maria mwishoni mwa mwezi wa Maria, kutekeleza kwa pamoja sala kwa Maria ulimwenguni kote katika maandalizi ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Lengo, kwa mujibu wa taarifa ni “kuwafahamisha Watu wa Mungu umuhimu wa Mchakato unaoendelea na kuwasihi waamini kuusindikiza kwa sala” na kuuweka “chini ya ulinzi maalumu wa Mama yetu wa Mchakato mzima wa Sinodi katika Kanisa, hasa kazi ya Mkutano Mkuu”.
Muda wa maombi kwa makanisa yote ulimwenguni
Mwaliko uliotolewa kwa niaba ya Kardinali Grech kwa wakuu wa Makanisa Katoliki ya Mashariki na marais wa Mabaraza ya Maaskofu, ni kutekeleza wakati wa sala muhimu ambayo itaonesha uzuri wa dini karibu na madhabahu ya Maria, tarehe 31 Mei 2023 ambayo itachaguliwa kwa hiari ya Mabaraza ya Maaskofu binafsi katika kila nchi. Sala lazima ijumuishe ushiriki wa miito mbalimbali ya kikanisa (walei, wa mapadre, na watawa kike na kiume). Hata jumuiya za parokia, kwa kukubaliana na askofu wao wa jimbo, zinaalikwa kutenga muda wa sala siku hiyo kwa ajili ya shughuli ya Sinodi. Hata hivyo, Papa Francisko, Alhamisi 16 Machi 2023, Papa Francisko amekutana na Kardinali Mario Grech Katibu Mkuu wa Sinodi akiwa na Wajumbe wa Tume kwa ajili ya Sinodi ya kawaida ya XVI kwa ajili ya Maaskofu.