Tafuta

Mkutano wa Sinodi Barani Afrika umeadhimishwa kuanzia tarehe 1-6 Machi 2023 huko Jijini Addis Ababa. Awamu ya Tatu, Kanisa la Kiulimwengu ni kuanzia mwezi Oktoba 2023 mjini Vatican. Mkutano wa Sinodi Barani Afrika umeadhimishwa kuanzia tarehe 1-6 Machi 2023 huko Jijini Addis Ababa. Awamu ya Tatu, Kanisa la Kiulimwengu ni kuanzia mwezi Oktoba 2023 mjini Vatican. 

SECAM: Familia ya Mungu Ni Utambulisho wa Kanisa Barani Afrika

Mababa wa Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu Barani Afrika iliyoadhimishwa kunako mwaka 1994, walikazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia na Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, ikawekwa kuwa ni kielelezo na chemchemi ya kiroho ya kila familia ya Kikristo. Walihimiza wajibu na dhamana ya wanandoa na familia; umuhimu wa jukumu la ndoa kama Sakramenti na kwamba wanaitwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Addis Ababa, Ethiopia.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho haya yamegawanyika katika awamu kuu tatu kuanzia Mwezi Oktoba 2021 hadi Oktoba 2024. Awamu ya kwanza ilikuwa ni kwa ajili ya Makanisa mahalia pamoja na taasisi zote zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki nayo yalianza tarehe 10 Mwezi Oktoba 2021 hadi 15 Agosti 2022. Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ni kuanzia Mwezi Septemba 2022 hadi Machi 2023 na hapa kutakuwa na Ujumbe na vipaumbele vya watu wa Mungu, vitakavyotumika kutengeneza “Hati ya Kutendea Kazi; Instrumentum laboris.” Kumbe, Mkutano wa Sinodi Barani Afrika umeadhimishwa kuanzia tarehe 1-6 Machi 2023 huko Jijini Addis Ababa. Awamu ya Tatu, Kanisa la Kiulimwengu ni kuanzia mwezi Oktoba 2023. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wote wa Mungu kujizatiti kikamilifu ili waweze kuwa ni wajenzi wa sanaa ya watu kukutana. Huu ni muda muafaka wa kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu. Ni wakati wa kukoleza utamaduni wa Sala, Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu na kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu anataka kuliambia nini Kanisa kwa nyakati hizi. Ni wakati wa kukutana na kutajirisha kutokana na karama, miito na utume ambao watoto wa Kanisa wamekirimiwa kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ni makutano yanayohitaji ukweli na uwazi, ujasiri na uwepo ili kukutana na wengine. Huu ni mwelekeo mpya unaowataka waamini kutoka katika: uchoyo, ubinafsi na mazoea yao, tayari kukutana na Mwenyezi Mungu ambaye yuko na anatembea pamoja nao katika ukweli na uwazi!

SECAM: Familia ya Mungu ni utambulisho wa Kanisa Barani Afrika
SECAM: Familia ya Mungu ni utambulisho wa Kanisa Barani Afrika

Mababa wa Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu Katoliki Barani Afrika iliyoadhimishwa kunako mwaka 1994, walikazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia na Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, ikawekwa kuwa ni kielelezo na chemchemi ya kiroho ya kila familia ya Kikristo. Walikazia umuhimu wa wajibu na dhamana ya wanandoa na familia; umuhimu wa jukumu la ndoa kama Sakramenti na kwamba, walikuwa wanaitwa na kuhamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia katika ulimwengu mamboleo. Kumbe, waamini walipewa wajibu wa kuokoa na kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na hivyo kuwa tayari kushirikiana na familia nyingine. Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” alikazia familia kwa kusema kwamba, familia ni hekalu la uhai, ni shule ya: Upendo, haki, amani, msamaha na upatanisho. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Familia ni mahali pa kuinjilisha na kuinjilishwa.

SECAM: Familia ni Kipaumbele cha kwanza Kwa Kanisa Barani Afrika
SECAM: Familia ni Kipaumbele cha kwanza Kwa Kanisa Barani Afrika

Katika mahojiano maalum kati ya Radio Vatican na Padre Anthony Makunde Katibu mkuu wa AMECEA yaani: Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, linaloundwa na Nchi 8 ambazo ni: Zambia, Malawi, Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia na Eritrea, anaelezea umuhimu wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Awamu ya Pili Barani Afrika kama sehemu ya mchakato wa familia ya Mungu Barani Afrika kujizatiti kushiriki katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili. Padre Anthony Makunde anasema, imekuwa ni fursa ya kung’amua fursa, changamoto na mahangaiko ya watu wa Mungu kutokana na: Umaskini, Ujinga, Maradhi; Ukosefu wa haki, amani na maridhiano. Pamoja na yote haya, Kanisa Barani Afrika halijakata tamaa, bali linasonga mbele kwa ari, nguvu na mwamko mpya, kwa kuendelea kujikita katika nguvu ya Neno la Mungu na kwa msaada wa Roho Mtakatifu, iko siku Kanisa litashinda. Wajumbe wa Maadhimisho ya Sinodi ya 16 ya Maaskofu Ukanda wa Afrika wakiwa wamekusanyika katika makundi 15 walisali na kutafakari na hatimaye wakaibuka na vipaumbele 15 vya Kanisa Barani Afrika. Baada ya tafakari ya kina, vipaumbele hivi vikapembuliwa kwa makini na hatimaye kubaki vipaumbele 8. Kama familia ya Mungu Barani Afrika inapaswa kujikita katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, amani, utawala bora na kwamba, rasilimali za Afrika ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Afrika. Tunu msingi za maisha ya Kiafrika hazina budi kupewa uzito unaostahili katika nyaraka na mafundisho ya Kanisa hususan, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, umoja na mshikamano, ukarimu, majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni na uwajibikaji wa pamoja.

Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zidumishwe na wote.
Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zidumishwe na wote.

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi hauna budi kusimikwa katika utamadunisho, liturujia na ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Kanuni auni, ushirika na umoja wa watu wa Mungu ni muhimu kupewa uzito wa pekee kwa kukazia malezi awali na endelevu. Kanisa la Kisinodi liwahusishe na kuwashirikisha watu wote wa Mungu bila ubaguzi. Malezi na majiundo ya awali na endelevu kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha ya utume wa Kanisa, ili kujenga miundo mbinu itakayoliwezesha Kanisa Barani Afrika kutembea bega kwa bega na kwa ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi hauna budi kufumbatwa katika tunu msingi za maisha ya watu wa Mungu: Uhai, utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Haki ya tabianchi, ni changamoto inayohitaji wongofu wa ikolojia unaopaswa kumwilishwa katika maisha na utumje wa Kanisa. Kuna haja ya kukuza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kuhusu ndoa na familia pamoja na kuangalia changanoito zake, ili kuzipatia suluhu ya kudumu katika mwanga wa tunu msingi za Kiinjili na utu wema. Padre Anthony Makunde Katibu mkuu wa AMECEA anakaza kusema, utambulisho wa Kanisa Barani Afrika unasimikwa katika taswira ya familia ya Mungu. Hapa ni mahali ambapo Kanisa mahalia linapata chimbuko, mizizi na utambulisho wake. Huu ni wakati wa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kulea tunu msingi za maisha ya familia Barani Afrika.

Ni wakati wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha familia
Ni wakati wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha familia

Padre Makunde anakaza kusema, Kanisa Barani Afrika bado ni changa. Lina vijana wengi na limebahatika kupata mafanikio makubwa, lakini bado kuna changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi kisinodi kwa kukazia: umoja, ushiriki na utume wa watu wote wa Mungu Barani Afrika na nje ya Afrika. Huu ni wakati wa kutembea pamoja kama Kanisa la Kisinodi, kwa kujikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Kanisa Barani Afrika linajiandaa kuzindua mpango mkakati wa malezi ya awali na endelevu ili kuendeleza: roho, ari na mwamko wa Kisinodi, uliowashwa katika safari ya pamoja ya watu wa Mungu katika kipindi cha Miaka miwili ya maadhimisho ya Sinodi. Jambo la msingi ni kuendeleza: Umoja, ushiriki na utume wa watu wote wa Mungu, ili kutangaza na kushuhudia imani pasi na woga, kuendelea kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Familia ya Mungu Barani Afrika, anasema, Padre Anthony Makunde Katibu mkuu wa AMECEA, iendelee kumwomba Mwenyezi Mungu ili awaimarishe waamini katika mchakato wa kujenga na kuliimarisha Kanisa la Mungu Barani Afrika.

Familia ya Mungu Afrika
14 March 2023, 16:26