Tafuta

2023.03.27 cKardinali  Karl-Josef Rauber 2023.03.27 cKardinali Karl-Josef Rauber 

Kadinali Karl-Josef Rauber aliaga dunia

Rais wa zamani wa Chuo cha Kipapa cha Kikanisa na aliyewahi kuwa Balozi katika maeneo magumu na mazingira ya kijamii alifariki 26 Machi usiku akiwa na umri wa miaka 88.Kufuatia na kifo chake Baraza la makardinali kwa sasa wako 222,ambapo 123 wanapiga kura na 99 hawawezi kupiga kura.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Kadinali Karl-Josef Rauber, wa Ujerumani  aliyekuwa Balozi wa Vatican kwa miaka mingi alifariki tarehe  26 Machi usiku akiwa na umri wa miaka 88. Alikuwa emezaliwa tarehe 11 Aprili 1934 huko Nuremberg (Nürnberg), katika Jimbo Kuu la Bamberg (Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani), na kupewa daraja la ukuhani mnamo mwaka wa 1959, na baadaye  alitekeleza huduma yake kwa miaka mitatu katika jumuiya ndogo ya Wakatoliki wa Nidda, huko Upper Hesse. Kuanzia mwaka wa 1962 alihamia Roma alisoma na kupata shahada ya Sheria ya Kanoni na kuhudhuria Chuo cha Kipapa cha Kikanisa. Mnamo 1966 alianza kazi yake ya kidiplomasia na hadi 1977 alikuwa mmoja wa makatibu wanne wa Giovanni Benelli  ambaye baadaye alikuwa Kardinali na askofu mkuu wa Firenze. Ni hapo katika kipindi ambacho alishikilia wadhifa wa katibu Msaidizi wa Vatican, Benelli na Papa Paul VI mwenyewe walikuwa na matokeo makubwa kwa maisha na huduma yake. kwa hiyo Kardinali  Rauber katika miaka kumi na moja iliyotumika katika Curia Romana kiukweli alipata uzoefu mkubwa wa kikanisa katika ushirika wa karibu na Papa.

Utumishi kwa muda mrefu katika diplomasia

Kuanzia 1977, kama mshauri wa Ubalozi, alihudumu katika uwakilishi wa kipapa huko Ubelgiji, Luxemburg na Ugiriki. Tarehe 18 Desemba 1982 Yohane Paulo II alimteua kuwa Balozi wa Vatican  nchini Uganda, akimteua kuwa askofu mkuu wa Giubalziana. Tarehe 6 Januari 1983 alipata daraja la uaskofu kutoka kwa Papa Wojtyła katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Januari 1990 alikabidhiwa urais wa Chuo cha Kipapa cha Kikanisa. Miaka mitatu baadaye, alirejea katika utumishi hai wa kidiplomasia kwanza kama mwakilishi wa kipapa nchini Uswizi na Liechtenstein (1993-1997), kisha Hungaria na Moldavia (1997-2003); hatimaye nchini Ubelgiji na Luxemburg (2003-2009), akimalizia pale ambapo kazi yake ya kidiplomasia ilikuwa imeanza.

Alikabiliana na changamoto 

Akiwa balozi wa kitume alilazimika kukabiliana na changamoto ngumu kwa Kanisa: nchini Uganda, kwa mfano, alitekeleza kazi yake katika miaka ambayo UKIMWI ulizuka na kuenea, na matokeo yake yalikuwa mabaya kwa watu; huko Uswisi alisaidia kusuluhisha mivutano iliyohusisha jimbo la Chur na Askofu Wolfgang Haas; katika Hungaria alisimamia awamu ya kurekebisha mahusiano kati ya Serikali na Kanisa baada ya enzi ya ukomunisti; huko Ubelgiji alifanya kazi katika muktadha wa kijamii na kisiasa ambao haukuwa rahisi kila wakati; na wakati uwakilishi wa kipapa kwa Umoja wa Ulaya ulipoundwa pia mjini Brussels, alichukua uamuzi wa kuoanisha na kugawanya kwa busara kazi ya taasisi hizo mbili za kidiplomasia nchini Ubelgiji.

Alichaguliwa kuwa Kardinali mwaka 2015

Akiwa na umri wa miaka 75, alistaafu utumishi mwaka 2009 na tangu wakati huo ametekeleza huduma yake ya kiroho na kichungaji nchini Ujerumani, katika nyumba ya Masista wa Maria wa Schönstatt huko Ergenzingen, jimbo la Rottenburg-Stuttgart, akidumisha maisha ya kila siku, uhusiano na Jimbo la Mainz. Baba Mtakatifu Francisko alimuunda kuwa Kardinali katika Mkutano  tarehe 14 Februari 2015.

28 March 2023, 16:24