Tafuta

Familia za Kikristo ziwe ni mahali ambapo, imani, matumaini, mapendo, maadili na utu wema vinarithishwa, kama ushuhuda wa nuru ya Kristo Yesu na tunu msingi za Kiinjili. Familia za Kikristo ziwe ni mahali ambapo, imani, matumaini, mapendo, maadili na utu wema vinarithishwa, kama ushuhuda wa nuru ya Kristo Yesu na tunu msingi za Kiinjili.  

Familia za Kikristo Ziwe ni Mahali Pa Kurithisha: Imani, Maadili, Utu Wema na Utakatifu

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher: Waamini wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa utu wema, haki, amani, upendo, ukarimu na mshikamano, sanjari na kuzingatia kweli za Kiinjili. Familia za Kikristo ziwe ni mahali ambapo, imani, matumaini, mapendo, maadili na utu wema vinarithishwa, kama ushuhuda wa nuru ya Kristo Yesu na tunu msingi za Kiinjili. Wawe na ujasiri wa kutoka katika giza la dhambi na kuanza mchakato wa kutembea katika nuru ya Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa kuanzia tarehe 18 hadi tarehe 20 Machi 2023 anafanya hija ya kichungaji nchini Albania, kwa mwaliko uliotolewa kutoka kwa viongozi wa Serikali na Kanisa nchini humo. Albania na Vatican, zilianza kuwa na mahusiano ya kidiplomasia kuanzia mwaka 1920, lakini uhusiano huu ulisuasua wakati wa Utawala wa Kikomunisti nchini humo na huo ukawa ni mwanzo wa madhulumu na nyanyaso dhidi ya Kanisa nchini humo. Mahusiano ya kidiplomasia yaliweza kujengwa upya tarehe 7 Septemba 1991 baada ya Utawala wa Kikomunisti kuangushwa chini. Baraza la Maaskofu Katoliki Albania linasema, ziara hii ya kichungaji ya Askofu mkuu Paul Richard Gallagher ni kuendeleza mchakato wa kuimarisha mahusiano na mafungamamo ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili ambayo yameoneshwa kwa namna ya pekee baada ya Mtakatifu Yohane Paulo II kutembelea Albania tarehe 25 Aprili 1993 na Baba Mtakatifu Francisko kufanya hija yake ya kitume nchini humo tarehe 21 Septemba 2014. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher akiwa nchini Albania, Dominika tarehe 19 Machi 2023 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Rrëshen, amewataka watu wa Mungu nchini Albania kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili, baada ya kuvuka machungu na huzuni nyingi na sasa wanaalikwa kushangilia kwa sababu watashibishwa kwa utamu na faraja ya Mungu, wakati huu wanapoadhimisha Dominika ya furaha “Laetare”: “Lætare Jerusalem: et conventum facite omnes qui diligitis eam: gaudete cum lætitia, qui in tristitia fuistis: ut exsultetis, et satiemini ab uberibus consolationis vestræ.” Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu daima yuko kati pamoja na waja wake.

Mashuhuda wa Albania ni msingi wa Kanisa
Mashuhuda wa Albania ni msingi wa Kanisa

Kipindi cha Kwaresima ni muda muafaka wa kutafakari wito, dhamana na wajibu ambao waamini wamejitwalia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowawezesha kushiriki: Unabii, Ufalme na Ukuhani wa Kristo Yesu. Huu ni wakati wa kutafakari kuhusu: maji, mwanga na maisha ya mwanadamu, kama yanavyofafanuliwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake, tayari kuwakirimia waja wake: Utakaso wa dhambi unaowawezesha kutembea katika nuru ya Kristo Msulubiwa, ili hatimaye, kupata maisha na uzima wa milele. Ni mwaliko wa kutoka katika giza la dhambi na mauti na kuanza mchakato wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya imani, matumaini na mapendo na Fumbo la Utatu Mtakatifu, huku wakiendelea kujikita katika toba na wongofu wa ndani tayari kutembea katika nuru ya Kristo Yesu kama viumbe vipya. Na matunda ya safari hii ya nuru ni wema wote, haki na ukweli kama anavyobainisha Mtume Paulo. Rej Efe 5: 8-14. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni mambo yanayokita mizizi yake katika utamaduni wa kifo. Waamini wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa utu wema, haki, amani, upendo, ukarimu na mshikamano, sanjari na kuzingatia kweli za Kiinjili. Familia za Kikristo ziwe ni mahali ambapo, imani, matumaini, mapendo, maadili na utu wema vinarithishwa, kama ushuhuda wa nuru ya Kristo Yesu na tunu msingi za Kiinjili. Watambue kwamba, wanapokabiliana na changamoto, matatizo na fursa mbalimbali watambue kwamba, Kristo Yesu yuko kati pamoja nao. Wakristo wote, lakini kwa namna ya pekee, watu wa Mungu nchini Albania wanapaswa kutangaza na kushuhudia ujasiri wa imani kama walivyofanya mashuhuda 38 wa imani nchini Albania kwa kusadaka maisha yao kwa ajili ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vijana wahamasike zaidi kuwa ni mashuhuda wa imani.

Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni muhimu sana
Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni muhimu sana

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher akiwa nchini Albania, Jumamosi, tarehe 18 Machi 2023 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Scutari, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 30 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea nchini Albania, ili kuwatia shime, ari na mwamko wa kimisionari, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kwa njia ya: Neno na Sakramenti zake aguse na kuwatakasa kutoka katika undani wa maisha yao kama ilivyokuwa kwa yule mtu kipofu tangu kuzaliwa kwake. Hii ni changamoto ya kusikiliza kwa makini na kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha. Hivi ndivyo alivyofanya Mama Theresa wa Calcutta, Mama wa maskini kati ya maskini zaidi, ambaye ni mzaliwa wa Albania. Huu ni mwaliko wa kukiri, kutangaza na kushuhudia imani kwa matendo adili na matakatifu na hivyo kuondokana na matendo ya giza. Baba Mtakatifu Francisko anasema, majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni sehemu ya vinasaba vya uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko na kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher alihitimisha mahubiri yake, kwa kuwaweka watu wa Mungu nchini Albania chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Shauri Jema anayeheshimiwa sana na watu wa Mungu nchini Albania kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 26 Aprili 1992.

Wakristo wawe ni mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo
Wakristo wawe ni mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher akiwa nchini Albania amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali ya Albania na pande zote mbili zimeonesha utashi wa kutaka kuboresha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Albania. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher ameipongeza Serikali ya Albania kwa kukamilisha mchakato, ili hatimaye, iweze kujiunga na Umoja wa Ulaya, EU. Huu ni muungano wa kisiasa na wa kiuchumi wa nchi 27 za Ulaya, ulioanzishwa kunako mwaka 1991 juu ya msingi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya. Madhumuni makubwa hasa ni kujenga uchumi wa pamoja, kuboresha maisha ya watu wa Ulaya na kuzuia vita kati ya nchi za Ulaya. Nchi 19 za Umoja huu hutumia pesa moja ya Euro. Nchi nyingi za Umoja zimepatana kufungua mipaka yao bila vizuizi kwa wakazi wote. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher amekaza kusema, hija za kitume zilizofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1993 na Baba Mtakatifu Francisko mwaka 2014 pamoja na ile iliyofanywa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kunako mwaka 2019 zinapania kuendelea kujenga na kudumisha uhusiano na ushirikiano wa Kimataifa na nchi ya Albania. Ziara hii ya kikazi nchini Albania imekuwa ni fursa ya kulishukuru na kulipongeza Kanisa mahalia kwa kuendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Albania hususan katika sekta ya elimu, afya, maendeleo pamoja na ustawi wa jamii. Mada nyingine tete zilizojadiliwa na viongozi katika mikutano yao ya faragha ni pamoja: Athari ya Vita kati ya Urusi na Ukraine, matumaini ya Albania kujiunga na Umoja wa Ulaya sanjari na umuhimu wa kujenga ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Ulaya.

Albania
20 March 2023, 15:14