Tafuta

Awamu ya kwanza ya Maadhimisho ya Sinodi ni kuanzia tarehe 1-29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili itaadhimishwa Mwezi Oktoba 2024. Awamu ya kwanza ya Maadhimisho ya Sinodi ni kuanzia tarehe 1-29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili itaadhimishwa Mwezi Oktoba 2024.  

Maadhimisho ya Sinodi Barani Afrika: Majadiliano, Familia, Haki na Amani

Matokeo na changamoto zilizojitokeza ni maswali makuu ambayo Makatibu wakuu wa Mashirikisho ya Mabaraza ya Maaskofu yanayounda SECAM walijitahidi kuyajibu kwa ufupi. Watu wa Mungu wameridhishwa na mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza. Shukrani za pekee, zinamwendea Baba Mtakatifu Francisko kwa ubunifu na wongofu huu wa shughuli za kichungaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kuanzia Oktoba 2023 hadi Oktoba 2024 yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Kusikiliza ni kujenga utamaduni wa kusali pamoja na Neno la Mungu, “Lectio Divina.” Awamu ya kwanza ya Maadhimisho ya Sinodi ni kuanzia tarehe 1-29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili itaadhimishwa Mwezi Oktoba 2024. Lengo ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa watu wa Mungu katika ujumla wao kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Maadhimisho ya Sinodi ni wakati muafaka wa toba na wongofu wa ndani, kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza, ili hatimaye, kuhamasisha umoja na ushiriki wa watu wa Mungu kutoka katika ngazi mbalimbali za maisha, kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emau.

Ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana kama watoto wa Mungu
Ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana kama watoto wa Mungu

Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu inapenda kuwaalika wadau katika tasnia ya mawasiliano ya habari, kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, mchakato wa kiimani unaopania kujenga na kudumisha umoja, ushiriki na utume wa Kanisa mintarafu jitihada za majadiliano ya kiekumene. Hayo yamebainishwa na Askogu Luis Marín de San Martín, O.S.A., Katibu mkuu Msaidizi wa Sinodi za Maaskofu, hivi karibuni alipokua anazungumza na Makatibu wakuu kutoka katika nchi zinazounda Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM kwa njia ya mtandao. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni mchakato unaofumbatwa katika jitihada za Mama Kanisa katika uinjilishaji kwa kuzingatia muktadha wa watu, mazingira na historia yao na wala si tukio lenye mwanzo na hatima yake. Mama Kanisa anapenda kujikita katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Juhudi zote hizi hazina budi kwenda sanjari na majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji yam tu mzima kiroho na kimwili. Mama Kanisa anatambua uzito wa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa ushiriki, umoja na utume wa Kanisa kama ilivyo pia katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho, kama ilivyokuwa kwenye Fumbo la Umwilisho, tunu msingi za kiinjili ziweze kupenya katika maisha na tamaduni za watu. Lengo ni kudumisha umoja katika tofauti za tamaduni za watu wa Mungu Barani Afrika na sehemu mbalimbali za dunia, ili kulitajirisha Kanisa.

Sinodi ya Maaskofu 2023-Oktoba 2024
Sinodi ya Maaskofu 2023-Oktoba 2024

Matokeo na changamoto zilizojitokeza ni maswali makuu muhimu ambayo Makatibu wakuu wa Mashirikisho ya Mabaraza ya Maaskofu yanayounda SECAM walijitahidi kuyajibu kwa ufupi. Watu wa Mungu katika ngazi mbalimbali wameridhishwa na mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza, ambao umewawezesha watu wa Mungu katika ngazi mbalimbali kushirikisha mawazo na maoni yao. Shukrani za pekee, zinamwendea Baba Mtakatifu Francisko kwa ubunifu na wongofu huu wa shughuli za kichungaji. Ni matumaini ya watu wa Mungu Barani Afrika kwamba, Kanisa litaweza kuibuka likiwa na nguvu, hai na kushikamana zaidi. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kidini, kisiasa na kiuchumi ni kati ya changamoto pevu zinazogumisha mchakato wa uinjilishaji na kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kuendelea kujikita zaidi katika majadiliano ya kidini, ili kuondokana na utamaduni wa kifo, vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kidini na kiimani, mchango uliotolewa na Padre Anthony Makunde, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Mama Kanisa haba budi kuendelea kuwekeza katika maisha na utume wa familia, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima; ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika: Uhai, huruma na mapendo.

Ushiriki wa watu wa Mungu katika maadhimisho ya Sinodi unavutia.
Ushiriki wa watu wa Mungu katika maadhimisho ya Sinodi unavutia.

Familia za Kikristo hazina budi kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia dhidi ya vikwazo na kinzani zinazojitokeza katika maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo. Ikumbukwe kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinatangazwa, zinashuhudiwa na zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kushikamana kama ndugu wamoja. Maisha ya ndoa na familia ni wito kwa waamini wengi ndani ya Kanisa. Tunu msingi za maisha ya kifamilia hazina budi kuvaliwa njuga la watu wa Mungu Barani Afrika kama sehemu ya mchango wao katika mchakato wa ujenzi wa umoja, utume na ushiriki wa watu wa Mungu katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na ujenzi wa msingi wa haki, amani na maridhiano. Amani duniani inapaswa kusimikwa katika: ukweli, haki, mshikamano na uhuru wa kweli. Taswira ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu katika muktadha wa Bara la Afrika ni ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana katika nyumba ya Mungu, ili kuimarisha umoja, ushiriki na utume wa Kanisa; mambo msingi katika azma ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. “Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze; ongeza urefu wa kamba zako; vikaze vigingi vya hema yako.” Isa 54: 2.

Sinodi Barani Afrika
19 January 2023, 14:52