Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Hati ya Kutendea Kazi Kimabara
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho haya yamegawanyika katika awamu kuu tatu kuanzia Mwezi Oktoba 2021 hadi Oktoba 2023. Awamu ya kwanza ni kwa ajili ya Makanisa mahalia pamoja na taasisi zote zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki ni kuanzia tarehe 10 Mwezi Oktoba 2021 hadi 15 Agosti 2022. Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ni kuanzia Mwezi Septemba 2022 hadi Machi 2023. Awamu ya Tatu, Kanisa la Kiulimwengu ni kuanzia mwezi Oktoba 2023. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wote wa Mungu kujizatiti kikamilifu ili waweze kuwa ni wajenzi wa sanaa ya watu kukutana. Huu ni muda muafaka wa kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu. Ni wakati wa kukoleza utamaduni wa Sala, Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu na kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu anataka kuliambia nini Kanisa kwa nyakati hizi. Ni wakati wa kukutana na kutajirisha kutokana na karama, miito na utume ambao watoto wa Kanisa wamekirimiwa kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ni makutano yanayohitaji ukweli na uwazi, ujasiri na uwepo ili kukutana na wengine. Huu ni mwelekeo mpya unaowataka waamini kutoka katika: uchoyo, ubinafsi na mazoea yao, tayari kukutana na Mwenyezi Mungu ambaye yuko na anatembea pamoja nao katika ukweli na uwazi!
Makutano ya kweli anasema Baba Mtakatifu yanafumbatwa katika sanaa ya kusikiliza kwa makini kama alivyofanya Kristo Yesu kwa yule kijana aliyekuwa na kero kubwa moyoni mwake kuhusu maisha ya uzima wa milele. Waamini wawe ni mahujaji wanaopenda Injili na wakiwa wazi kupokea zawadi za Roho Mtakatifu. Hiki ni kipindi cha neema ya kukutana, kusikilizana na hatimaye kufanya mang’amuzi ya pamoja. Waamini watambue kwamba, hata kabla ya kuanza kujitaabisha kumtafuta Mwenyezi Mungu katika maisha yao, Mwenyezi Mungu ndiye aliyekuwa wa kwanza kujitaabisha kuwatafuta! Wataalam waelekezi 50 wa maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu tangu tarehe 21 Septemba hadi tarehe 2 Oktoba 2022 walikuwa “wamejichimbia” mjini Frascati, ili kuandaa hati ya kutendea kazi katika Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Awamu ya Pili, baadaye wakakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Huu ulikuwa ni muda wa kusikilizana, kufanya upembuzi yakinifu na hatimaye, kufanya mang’amuzi ya kina kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Mungu. Wataalam waelekezi kutoka sehemu mbalimbali za dunia wameandaa Hati ya Kutendea Kazi katika ngazi ya Kimabara.
Wataalam waelekezi wamehariri muhtasari wa mapendekezo yaliyotolewa kutoka katika Maadhimisho ya Awamu ya Kwanza ya Sinodi na kwa hakika mwitikio umekuwa ni mkubwa sana, ikilinganishwa na maadhimisho ya Sinodi zilizotangulia. Wataalam waelekezi wameungana na wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu pamoja na Baraza la Sinodi za Maaskofu chini ya uongozi wa Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu pamoja na Kardinali Jean-Claude Hollerich, S.I., Mwezeshaji mkuu katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Hati ya Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi imepitishwa na Baraza la Sinodi za Maaskofu na hatimaye kumkabidhi Baba Mtakatifu Francisko, tayari kuwakabidhi watu wa Mungu. Hii ni sehemu ya mchakato wa Kanisa kupyaisha maisha na utume wake, kwa kuwashirikisha zaidi waamini walei, ili kujenga utamaduni wa kusikiliza, kung’amua na hatimaye utekelezaji wake. Mama Kanisa anahimizwa kusoma alama za nyakati na kutoa majibu muafaka, kwa kuzingatia: Maandiko Matakatifu, Mapokeo hai ya Kanisa pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa.