Tafuta

Kumbukumbu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi tarehe 4 Oktoba 2022: Mshikamano na maskini, umuhimu wa amani duniani pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kumbukumbu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi tarehe 4 Oktoba 2022: Mshikamano na maskini, umuhimu wa amani duniani pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.  (ANSA)

Kumbukumbu ya Mt. Francisko wa Assisi: Maskini, Amani na Utunzaji Bora wa Mazingira.

Kardinali Matteo Maria Zuppi kama sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu hii yaliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko mjini Assisi, Italia, katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha udugu wa karibu, upendo na mshikamano wa udugu wa kweli, chemchemi ya furaha na matumaini ya kweli yanayowawezesha waamini kuzungumzia fadhila ya amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 4 Oktoba anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mlinzi na Mwombezi wa Italia, aliyeishi kati ya Mwaka 1181 hadi tarehe 3 Oktoba 1226. Alibatizwa na kupewa jina la Yohane, akachezea ujana wake kwa kupenda sana anasa na matanuzi ya “kufa mtu.” Lakini baadaye alitubu na kumwongokea Mungu, kiasi cha kusadaka maisha yake kwa ajili ya huduma kwa maskini na wakoma waliokuwa wametengwa. Akajitahidi kumfuasa Kristo Yesu, Mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Katika maisha yake, Mtakatifu Francisko wa Assisi alishangazwa sana na huruma, upendo na unyenyekevu wa Mungu, uliopelekea hata akatungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu akazaliwa na Bikira Maria Pangoni, mahali pa kulishia wanyama. Safari hii ya unyenyekevu, ya Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ikapata maana ya pekee kama “Njia ya Msalaba” hata akatundikwa na kufa Msalabani, kifo cha aibu. Hii ni sadaka inayoendelezwa na Mama Kanisa katika Ibada ya Misa Takatifu inayotolewa sehemu mbalimbali za dunia. Mtakatifu Francisko wa Assisi alijisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu kwenye nchi za Kiislam huku akitumia silaha ya IMANI na huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa majadiliano ya kidini na kwamba, alikuwa tayari kuyamimina na maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake.

Mtakatifu Francisko wa Assisi: Amani, Maskini na Mazingira
Mtakatifu Francisko wa Assisi: Amani, Maskini na Mazingira

Vijana wengi wakavutwa na mtindo wa maisha ya Mtakatifu Francisko kiasi hata cha kulazimika kauanzisha Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Wafrancisko wa Assisi na kanuni ya Shirika hili ikaridhiwa na Papa Onorio wa III kunako mwaka 1223. Katika maisha na utume wake, akabahatika kupata makovu ya madonda Matakatifu mwilini mwake. Aliwapenda sana wanyama na kuyaona mazingira kuwa ni nyumba ya wote, kiasi cha kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu hadi kifo, kiasi cha kulikumbatia Fumbo la kifo kama dada. Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kama sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu hii yaliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko mjini Assisi, Italia, katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha udugu wa karibu, upendo na mshikamano wa udugu wa kweli, chemchemi ya furaha na matumaini ya kweli yanayowawezesha waamini kuzungumzia fadhila ya amani. Ni katika hali na mazingira kama haya, uvunjifu wa amani unatoweka na faraja inarejea tena moyoni. Kristo Yesu ni nuru ya ulimwengu inayowaangazia waja wake faraja, tayari kusimama na kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Mtakatifu Francisko alikuwa na mvuto mkubwa kwa vijana baada ya kuongoka.
Mtakatifu Francisko alikuwa na mvuto mkubwa kwa vijana baada ya kuongoka.

Ni muda wa kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kuna madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya, waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu nchini Italia. Huu ni mwaliko wa wongofu kwa ajili ya ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu, tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, katika masuala ya kisiasa na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Watu watambue, waheshimu na kuthamini umoja unaofumbatwa katika utofauti wao kielelezo cha amana na utajiri wa watu wa Mungu nchini Italia. Ni mwaliko wa kushikamana ili kupambana na umaskini wa hali na kipato unaoendelea kusigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watu wa Mungu wasimame kidete dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kuenzi Injili ya uhai. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wajitahidi kuganga na kuponya madonda makubwa ambayo yamejificha akilini mwa watu tayari kupokea, kushirikisha na kuwagawia wengine zawadi ya uhai. Katika hatari ya vita iliyoko mbele ya macho ya Jumuiya ya Kimataifa, Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Italia anawaalika wadau wakuu katika mgogoro huu, kujizatiti katika majadiliano, ili kweli haki na amani viweze kutamalaki katika akili na nyoyo za watu; mshikamano wa umoja na udugu wa kibinadamu uimarishwe na kudumishwa na wote!

Assisi 2022

 

 

04 October 2022, 15:26