Tafuta

Mkutano wa Lambeth: Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kardinali Luis A. G. Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Mkutano wa Lambeth: Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kardinali Luis A. G. Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu.  

Mkutano wa 15 wa Lambeth: Ushuhuda wa Ushirika: Imani, Huruma na Mapendo

Kanuni msingi za majadiliano ya kiekumene yakite mizizi yake katika maisha. Huu ni mchakato wa toba, wongofu na upatanisho ili kujenga ushirika wa Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu katika umoja na utofauti wake Ni umoja katika: Imani, Sakramenti na Wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Kumbe, kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu asili ya Kanisa na ushirika wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Lambeth “Lambeth Conference” ni mkusanyiko wa Maaskofu wa Jumuiya ya Kianglikan unaoitishwa na Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Canterbury lililoko nchini Uingereza kila baada ya miaka kumi. Ni mkutano wenye mamlaka ya hali ya juu, ambamo wajumbe wake, wanatoa ushauri kwa vipaumbele vya Kanisa Anglikan katika kipindi cha miaka kumi. Mkutano wa 15 wa Lambeth ulizinduliwa rasmi tarehe 26 Julai kwa ibada rasmi na unahitimishwa tarehe 8 Agosti 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kanisa la Mungu kwa Ulimwengu wa Mungu: kutembea, kusikiliza na kushuhudia pamoja.” Mkutano huu unapembua kwa kina na mapana maana ya ushirika wa Kanisa la Kiangalikan, ili kuitikia na kujibu changamoto, fursa na matatizo yanayojitokeza katika ulimwengu wa Karne ya 21. Uinjilishaji unaotekelezwa na Kanisa Katoliki katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza.

Mkutano wa 15 wa Lambeth umeitishwa na Askofu mkuu Welby
Mkutano wa 15 wa Lambeth umeitishwa na Askofu mkuu Welby

Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa ushirika wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Mkutano wa 15 wa Lambeth wajumbe kutoka Vatican wameshiriki na kutoa hotuba zao. Hawa ni Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Kardinali Kurt Koch, katika hotuba yake amekazia: majadiliano ya kiekumene ili kutekeleza mapenzi ya Mungu na Wakristo wakiwa wameungana waweze kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, dhamana inayopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo. Ni mwaliko wa kutubu na kuwongokea Mungu kwa kutambua na kukiri dhambi ya utengano ndani ya Kanisa, tayari kujizatiti katika ujenzi wa ushirika wa Kanisa unaoonekana.

Kanuni za Kikatoliki kuhusu majadiliano ya kiekumene zinapaswa kuzingatiwa, ili hatimaye, majadiliano ya kiekumene yaweze kujikita katika uhalisia wa maisha ya watu. Huu ni mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho ili kujenga ushirika wa Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu katika umoja na utofauti wake. Huu ni umoja katika: Imani, Sakramenti za Kanisa na Wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Kumbe, kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu asili ya Kanisa na ushirika wake. Majadiliano ya kiekumene hayana budi kukita mizizi yake katika asili ya imani ya Kikristo: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.” Efe 4:4-6. Ili kuweza kufikia ushirika kamili wa Kanisa, waamini lazima waoneshe ujasiri na unyenyekevu, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu yenye mvuto na mashiko! Utengano na migawanyiko ndani ya Kanisa inatishia ushuhuda wa Injili. Baba Mtakatifu Francisko anakazia pamoja na mambo mengine, utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu, Huduma kwa Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na Ushuhuda unaosimikwa katika kweli za Kiinjili. Rej. Evangelii gaudium 246. Dharura ya majadiliano ya kiekumene inasimikwa katika ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili, kwa sababu majadiliano ya kiekumene na utume wa Kanisa ni sawa na chanda na pete, yanategemeana na kukamilishana.

Ushirika wa Kanisa ushuhudiwe katika uhalisia wa maisha ya waamini
Ushirika wa Kanisa ushuhudiwe katika uhalisia wa maisha ya waamini

Kwa upande wake, Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu amekazia umuhimu wa kujenga mshikamano wa huduma katika maisha adili na matakatifu; katika huruma, upendo na unyenyekevu kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi, wahamiaji na maskini duniani. Hii ni changamoto kwa Wakristo kuwa na ndoto ya ujenzi wa nyumba moja ya maisha ya Kiroho, yaani Kanisa, ili Wakristo popote pale walipo waweze kujisikia kweli wako salama nyumbani. Nyumba hii ya pamoja, yaani Kanisa ni mkusanyiko wa watu kutoka katika: mataifa, makabila, lugha, tamaduni, mila na desturi mbalimbali. Kanisa liwe ni mahali pa upendo na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji. Kamwe dini zisitumike kama kichocheo cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii Kanisa liwe makini na watu wanaotaka “kujimwambafai” hawa ni wale wanaotafuta umaarufu usiokuwa na mvuto wa mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kiasi cha kusababisha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Wakristo wajifunze kutembea kwa pamoja katika unyenyekevu unaosimikwa kwenye fadhila ya huruma na upendo kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, hadi kutundikwa Msalabani.

Wakristo wajenge na kudumisha ushirika, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Maadhimisho ya Mkutano wa 15 wa Lambeth yanasimikwa katika Maandiko Matakatifu na kwa namna ya pekee kwa mwaka huu, wajumbe wanaongozwa na Waraka wa kwanza wa Mtakatifu Petro kwa Watu wote unaokazia kwa namna ya pekee kabisa: Mafundisho ya Ubatizo, kweli kuu za kiimani katika Kristo Yesu na maisha adili kadiri ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; Umuhimu wa kuvumilia mateso kwa saburi; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu na wokovu wa roho za watu unaopata chimbuko lake katika mateso, kifo na ufufuko kwa Kristo Yesu kwa wafu. Maadhimisho ya Mkutano wa 15 wa Lambeth ni muhimu hasa katika nyakati hizi, ambamo walimwengu wanashuhudia: vita, kinzani na migawanyiko ya kila aina.

Mkutano wa Lambeth

 

 

 

07 August 2022, 16:13