Tafuta

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio: Siku ya Kimataifa ya 35 ya Kuombea Amani Duniani iliyoanzishwa na Mt. Yohane Paulo II tarehe 26 Oktoba 1986. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio: Siku ya Kimataifa ya 35 ya Kuombea Amani Duniani iliyoanzishwa na Mt. Yohane Paulo II tarehe 26 Oktoba 1986. 

Jumuiya ya Mt. Egidio: Mkutano wa 35 wa Kuombea Amani Duniani 2021

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kuanzia tarehe 6 hadi 7 Septemba 2021 inaendesha Mkutano wa Sala Kimataifa kwa ajili ya kuombea amani dunia, kwa ushiriki na uwepo wa viongozi wakuu wa kidini kutoka sehemu mbalimbali za duniani, akiwemo Baba Mtakatifu Francisko. Mkutano huu unanogeshwa na kauli mbiu “Watu ndugu, Ardhi ya baadaye.” Mazingira, Amani na Udugu yamekaziwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Professa Andrea Riccardi, akiwa kijana mbichi bado, hapo tarehe 7 Februari 1968 alianzisha Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu mjini Roma na kujikita katika mambo makuu matatu yaani: Sala, Maskini na Amani duniani. Kanisa kuu la Bikira Maria wa Trastevere liliko mjini Roma, likawa ni makao makuu ya sala, maisha na utume wao sehemu mbalimbali za dunia. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ni matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unaokazia pamoja na mambo mengine: Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamadunia; sanjari na umuhimu wa kulinda na kudumisha amani, ustawi, maendeleo, mshikamano na udugu wa kibinadamu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha! Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 26 Oktoba 1986, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa aliwakutanisha viongozi wa kidini huko mjini Assisi, nchini Italia, kwa ajili ya kusali na kuombea amani duniani! Mkutano huu, ukawa ni chachu ya kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ili kudumisha amani duniani. Sala na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku ni nyenzo msingi ya ujenzi wa amani duniani.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Miaka 25 baadaye, aliwataka waamini wa dini mbalimbali kuendeleza roho na moyo wa sala kutoka Assisi kwa kudumisha majadiliano na upatanisho. Alikazia umuhimu wa vijana kufundwa utamaduni wa haki na amani na kwamba, majadiliano ya kidugu ni muhimu sana katika kukuza haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kuanzia tarehe 6 hadi 7 Septemba 2021 inaendesha Mkutano wa Sala Kimataifa kwa ajili ya kuombea amani dunia, kwa ushiriki na uwepo wa viongozi wakuu wa kidini kutoka sehemu mbalimbali za duniani, akiwemo Baba Mtakatifu Francisko. Mkutano huu unanogeshwa na kauli mbiu “Watu ndugu, Ardhi ya baadaye.” Mkutano huu umeandaliwa wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kupambana na athari za janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, tayari kuanza upya kwa kujikita katika umoja, ushirikiano na udugu wa kibinadamu. Ni mkutano unaowashirikisha wajumbe kutoka katika nchi 40 duniani. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; haki, amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu. UVIKO-19 imesababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 4.55 na wagonjwa waliolazwa hadi kufikia tarehe 7 Oktoba 2021 ni milioni 219. Wazee ni kati watu waliofariki zaidi kwa ugonjwa wa UVIKO-19.

Kuna watu ambao wamekosa fursa za ajira, watoto na vijana wameshindwa kuendelea na masomo na kwamba, kumekuwepo na mpasuko mkubwa wa huduma za kiafya na kijamii katika ujumla wake. Yote haya ni madonda yanayoikabili Jumuiya ya Kimataifa na yanapaswa kupewa suluhu ya kudumu inayofumbatwa katika umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliozinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020, unagusia magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi; mshikamano wa udugu wa kibibadamu; utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waraka huu umekuwa ni rejea makini katika mchakato wa kuganga na kupyaisha madonda yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Ujenzi wa ulimwengu mpya ni mchakato wa watu wote wa Mungu unaojikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki na amani duniani. Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha majadiliano katika ngazi mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni yasaidie kujenga msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Amani ya kweli inajengwa katika msingi wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili; kanuni maadili na utu wema; utawala wa sheria na haki msingi za binadamu! Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni sehemu ya hali halisi ya maisha ya binadamu yanayopswa kufanyiwa kazi kwa kujikita katika kanuni maadili, sheria za kimataifa sanjari na ujenzi wa siasa ya amani duniani inayofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani; upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu majadiliano pamoja na kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Jumuiya ya Kimataifa iwekeze katika uchumi unaojali na kuzingatia mahitaji msingi ya binadamu, utu na heshima yake!

Mt. Egidio
07 October 2021, 13:51