Tafuta

Mama Kanisa anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema: kulinda na kutangaza: ukuu, ukweli, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia. Mama Kanisa anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema: kulinda na kutangaza: ukuu, ukweli, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia. 

Dumisheni Ukuu, Ukweli, Uzuri na Utakatifu wa Familia Kanisa Dogo la Nyumbani

Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa, Familia na Maisha kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Matatizo na changamoto ni sehemu ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa, Familia na Maisha kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai”. Kwa ufupi anakazia kuhusu: Thamani ya maisha, ukuu na utu wa binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; Utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi.

Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watu wanaotetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Familia, Kanisa dogo la nyumbani linahamasishwa kuwa ni madhabahu ya Injili ya uhai, ambamo zawadi ya maisha inapokelewa na kutolewa. Familia iwe ni mahali pa kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya mwanadamu kwa njia ya mshikamano na kutembea kama watoto wa mwanga. Lengo ni kuondokana na utamaduni wa kifo kwa kukumbatia na kuambata utamaduni wa uhai. Kila mtu pamoja na taasisi mbalimbali anayo dhamana ambayo anapaswa kuiendeleza, kama shuhuda wa Injili ya uhai na chachu ya mabadiliko ya kweli ndani ya jamii. Amani ya kweli inalinda na kuendeleza Injili ya uhai!

Mtakatifu Yohane Paulo II alisimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia dhidi ya sera na mikakati inayolenga kubomoa taasisi ya familia. Mama Kanisa anatambua umuhimu wa familia katika Jamii, ndiyo maana anaendelea kutangaza ukuu wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema kwamba, Familia ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inapaswa kulindwa na kudumishwa hata kama ni kwa kujisadaka kwa njia ya maisha, kama ilivyotokea kwake, ili walimwengu waweze kusoma na kuitafakari Injili ya mateso ya familia, kama maandalizi makini ya kulinda na kuitetea familia katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Askofu Mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi ya Ndoa na Familia ya Yohane Paulo II, katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 22 Oktoba 2021 amezindua Mwaka wa Masomo 2021-2022 kwa Ibada ya Misa Takatifu. Amewashukuru na kuwapongeza viongozi waliomaliza muda wao wa huduma katika taasisi hii na kuwakaribisha wale walioteuliwa na kukubali kupokea dhamana hii. Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia kuanzia tarehe 19 Machi 2021 hadi 26 Juni 2022 unanogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu. Huu ni wakati muafaka kwa familia ya Mungu kurejea tena na kufanya tafakari ya kina kuhusu Wosia wa “Amoris laetitia” ambao unakazia: Upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka kuwa ni chemchemi na asili ya maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Anawahimiza wazazi na walezi kuimarisha elimu, malezi na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao. Ni wajibu wa Kanisa kuwasindikiza, kung’amua na kuwasaidia wanafamilia wanaolegalega katika maisha na wito wao wa ndoa na familia. Tafakari hii ifanywe kwa msaada wa nyenzo mbalimbali za shughuli za kichungaji kwa kusikiliza na kuyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na watu wa Mungu. Mkazo utolewe kwenye maandalizi ya wana ndoa watarajiwa, elimu kuhusu maana na mahusiano ya kimaumbile miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Waamini waelimishwe zaidi kuhusu: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Iwe ni nafasi ya kuadhimisha makongamano ya kitaifa na kimataifa kuhusu: upendo wa familia, wito na njia ya utakatifu ili kukabiliana na changamoto mambaoleo zinazoendelea kuibuka kila kukicha kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Askofu Mkuu Vincenzo Paglia anasema, maisha ya ndoa na familia ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wanandoa wote, kwa kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya wanandoa, Mwenyezi Mungu sanjari na watu wanaowazunguka. Wataalamu wa maisha ya ndoa na familia, wawasaidie waamini kutekeleza dhamana na wajibu wao katika maisha ya ndoa na familia!

Kwa upande wake, Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça, Mhifadhi mkuu wa Nyaraka za Kanisa na Mkutubi mkuu wa Maktaba ya Kanisa Katoliki katika hotuba yake amekazia uhusu Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliozinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020. Katika Waraka huu, Baba Mtakatifu unagusia magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu anakazia maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça anakazia mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu katika misingi ya ukweli na haki, ili kukuza na kudumisha urafiki wa kijamii. Udugu wa kibinadamu ni mchakato unaohitaji uvumilivu, utulivu, wongofu wa ndani na amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Ndoa na Familia

 

24 October 2021, 07:49