Tafuta

Bikira Maria ni Mfariji wa wale wote wanaoteseka:kiroho na kimwili. Bikira Maria ni Mfariji wa wale wote wanaoteseka:kiroho na kimwili. 

Bikira Maria Faraja ya Watu Wanaoteseka Kiroho na Kimwili!

Watu wanakimbilia ulinzi wa Bikira Maria wakiomba ili waweze kuanza tena maisha yanayosimikwa katika mshikamano na udugu wa kibinadamu. Bikira Maria Mfariji wa wale wanaoteseka, asaidie kuponya mateso ya wale wote waliopoteza ndugu zao kutokana na UVIKO-19. Bikira Maria awakirimie nguvu ya kuanza tena upya, huku wakiishi kwa amani, ujasiri na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 29 Agosti 2021 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 500 ya Kuvikwa Taji kwa Bikira Maria wa Oropa, kwenye Madhabahu ya Jimbo Katoliki Biella, lililoko Kaskazini mwa Italia. Bikira Maria kuvikwa taji la dhahabu ni tukio linaloadhimishwa kila baada ya miaka 100. “Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.” Mdo 1:14. Kardinali Giovanni Battista Re katika hotuba yake baada ya kumvika Taji ya Dhahabu Bikira Maria wa Oropa, amesema, huu ni mwendelezo wa sala inayopata chimbuko lake kunako mwaka 1620. Tangu wakati huo, kuna mamilioni ya mahujaji waliofika Madhabahuni hapa, ili kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano na Mwenyezi Mungu, ili awakirimie amani, faraja na mwanga angavu katika maisha yao. Ni mahali ambapo waamini wamekimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. Hata leo hii, bado wanakimbilia ulinzi wa Bikira Maria Mama wa Mungu wakiomba katika shida zao, ili waweze kuanza tena maisha ya kawaida yanayosimikwa katika mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Bikira Maria Mfariji wa wale wanaoteseka, asaidie kuganga na kuponya mateso ya wale wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki zao kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Bikira Maria awakirimie nguvu ya kuanza tena upya, huku wakiishi kwa amani, ujasiri na matumaini. Waamini wanamwomba Bikira Maria ili aweze kuwafundisha kuwa wakarimu na watu wenye mshikamano na vijana wasiokuwa na fursa za ajira; wale wote waliopoteza nafasi za Kazi; kwa wale wanaoteseka katika umaskini na upweke hasi, wapate faraja. Bikira Maria Malkia wa familia, aziombee familia ili ziweze kuungana na kushikamana kwa dhati, ili kamwe wanafamilia wasimsahau Mwenyezi Mungu! Familia ziwe ni mahali pa amani na utulivu; upendo na maridhiano, ili kuvuka changamoto na matatizo yanayoweza kuibuka ndani ya familia na badala yake, familia iwe ni kitovu cha maelewano na msamaha! Bikira Maria aziombee familia ili ziweze kuzamisha mizizi yake katika imani, mapendo na kuendelea kutembea katika mwanga wa Injili ya uaminifu kwa Mungu.

Bikira Maria aendelee kuwaombea vijana wa kizazi kipya ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya wito wa Daraja Takatifu ya Upadre na maisha ya kitawa, muhimu sana katika kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika ulimwengu mamboleo! Bikira Maria mwingi wa huruma na mapendo, aendelee kuzisimamia na kuziombea familia ambazo zinaogelea katika matatizo na changamoto mbalimbali bila kuzisahau zile ambazo zimevunjika na kusambaratika kutokana na sababu mbalimbali. Bikira Maria aendelee kuwasaidia waamini kupata mwanga angavu unaoyaangazia mapito ya maisha yao. Bikira Maria aendelee kulilinda Kanisa, Baba Mtakatifu, Maaskofu, Mapadre, watawa, waamini na watu wote wa Mungu katika ujumla wake. Bikira Maria ailinde na kuisindikiza Jumuiya ya waamini wa Jimbo Katoliki la Biella, Piemonte, Italia na dunia katika ujumla wake, ili daima waweze kusimama kidete kulinda, kutetea mafao ya wengi; ili ziwepo jitihada za kujenga na kudumisha: haki, amani na mapendo katika nyoyo na jamii.

Wakristo wajitahidi kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za Kikristo na hatimaye, asaidie mchakato wa safari ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa nchini Italia. Wakristo wawe ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma ya upendo kama Bikira Maria alivyofanya kwa kumtembelea Elizabeth na hivyo kumshirikisha furaha sanjari na kumpatia msaada. Bikira Maria awe ni mfariji na matumaini ya waja wake!

Bikira Maria Oropa
04 September 2021, 14:35