Tafuta

Mkutano wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu ujenzi wa Lebanon. Kiasi cha milioni 370 kinahitajika ili kuhakikisha kuhusu usalama wa chakula na huduma msingi za kijamii. Mkutano wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu ujenzi wa Lebanon. Kiasi cha milioni 370 kinahitajika ili kuhakikisha kuhusu usalama wa chakula na huduma msingi za kijamii. 

Vatican: Mkutano wa Kimataifa Kuhusu Ujenzi wa Lebanon 2021

Lebanon inahitaji kiasi cha dola za Kimarekani milioni 370 ili kukabiliana na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula; huduma ya maji safi na salama; afya na elimu. Lebanon itapaswa kuendeleza majadiliano na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, kuandaa na hatimaye kutekeleza mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2022 kwa kuzingatia misingi ya uhuru, ukweli na uwazi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 4 Agosti 2021, Mwaka mmoja tangu Mlipuko wa Lebanon ulipotokea, amesema bado ametia nia ya kutembelea Lebanon na kamwe hachoki kusali na kuwaombea, ili Lebanon iweze kurejea tena kuwa ni ujumbe wa amani na udugu wa kibinadamu huko Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikishwa na mlipuko huo, kiasi cha kupoteza: maisha, makazi, fursa za ajira na ndoto ya kuendelea kuishi. Baba Mtakatifu ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi ili kuisaidia Lebanon, ili iweze “kufufuka tena” kwa vitendo na wala si kwa maneno matupu! Ameonesha matumaini yake kwa mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa pamoja na Ufaransa kwamba, utaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: ujenzi mpya wa Lebanon! Tarehe 4 Agosti 2021 Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Serikali ya Ufaransa, Nchi 33, Mashirika ya Kimataifa 13 pamoja na wawakilishi 5 kutoka Lebanon, umefanya mkutano kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, kama sehemu ya mwendelezo wa mkutano uliofanyika tarehe 2 Desemba 2020.

Hali ya maisha ya wananchi wengi wa Lebanon imeshuka sana na wananchi wote wa Lebanon wametakiwa kuwajibika barabara katika mchakato wa kufufua tena nchi yao. Viongozi wa kisiasa wametakiwa kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata taarifa kamili katika misingi ya ukweli na uwazi, ili kufahamu kile kilichopelekea Mlipuko wa Lebanon tarehe 4 agosti 2020. Mlipuko huo umewatumbukiza wananchi wote wa Lebanon katika mgogoro wa kiuchumi na ukata wa fedha; ukosefu wa huduma na mahitaji msingi. Hali hii imepelekea pia kuibuka kwa machafuko ya kisiasa ambayo yamekwamisha uundwaji wa serikali. Kimsingi wananchi wa Lebanon hawana imani na wanasiasa. Lebanon inahitaji kiasi cha dola za Kimarekani milioni 370 ili kukabiliana na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula; huduma ya maji safi na salama; afya na elimu pamoja na kujielekeza zaidi katika kuokoa maisha ya watu wengi waliokata tamaa. Lebanon itapaswa kuendeleza majadiliano na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, kuandaa na hatimaye kutekeleza mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2022 kwa kuzingatia misingi ya uhuru, ukweli na uwazi.

Ni katika muktadha huu, Monsinyo Wachowski Mirosław Stanisław, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican, amesema kwamba, Kanisa pamoja na Mashirika yake ya Misaada Kitaifa na Kimataofa limechangia sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa ujenzi mpya wa Lebanon kwa kutoa huduma ya moja kwa moja kwa waathirika pamoja na maboresho katika sekta ya elimu, afya na ujenzi wa makazi bora ya watu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Lebanon ina mchango mkubwa sana katika Ukanda wa Mashariki ya Kati, hasa kwa kujikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano. Lebanon inapaswa kuendelea kuwa ni ujumbe amani na udugu wa kibinadamu kutoka huko Mashariki ya Kati. Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu ndani nan je ya Lebanon kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala si kwa watu wachache wanao neemeka kwa mateso ya wananchi wa Lebanon. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kushikamana ili kuwajengea watu wa Lebanon matumaini kwa kuwawezesha wananchi wa Lebanon kushiriki kikamilifu katika hatima ya ujenzi wa nchi yao!

Kwa upande wake, Kardinali Béchara Boutros Raï, O.M.M., Patriaki wa Kanisa la Wamaroniti Wakatoliki nchini Lebanon katika mahubiri yake, kumbukizi la Mwaka mmoja tangu Mlipuko wa Lebanon utokee, amekazia umuhimu wa waamini kuchota faraja na matumaini kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Maandiko Matakatifu na kwamba, maisha yao yana thamani kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu. Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, yawe ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Familia ya Mungu nchini Lebanon, tarehe 4 Agosti 2021 imesali na kuwakumbuka wale wote waliopoteza maisha kutokana na Mlipuko wa Lebanon, kama kielezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Watu wa Mungu nchini Lebanon wana haki ya kutaka kufahamu ukweli na kuona haki inashika mkondo wake. Huu ni wakati wa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Lebanon mpya inayosimikwa katika umoja, upendo na mshikamano wa Kitaifa na Kimataifa. Ni fursa ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wananchi wanataka mabadiliko yanayofumbatwa katika misingi ya: Umoja na amani, uhuru na demokrasia ya kweli, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya hali na maisha ya wananchi wa Lebanon. Hakuna sababu ya kukata wala kujikatia tamaa, bali wananchi waendelee kujikita katika kanuni maadili na utu wema.

Ujenzi wa Lebanon
05 August 2021, 15:18