Tafuta

Viongozi wa Kidini Barani Afrika wametia saini kwenye Tamko la Pamoja Kupinga Utumwa mamboleo unaodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! Viongozi wa Kidini Barani Afrika wametia saini kwenye Tamko la Pamoja Kupinga Utumwa mamboleo unaodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! 

Tamko la Pamoja Kupinga Utumwa Mamboleo Ulimwenguni 2021

Viongozi 14 wa kidini kutoka Barani Afrika tarehe 6 Agosti 2021 wametia saini kwenye Tamko la Pamoja Kupinga Utumwa Mamboleo unaodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hawa ni viongozi wanaowajibika kimaadili kupambana na mambo yote yanayokwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu! Utu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Kwa mara ya kwanza katika historia, viongozi 14 wa kidini kutoka Barani Afrika tarehe 6 Agosti 2021 wametia saini kwenye Tamko la Pamoja Kupinga Utumwa Mamboleo unaodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuna zaidi ya watu milioni 40 ambao wameathirika kutokana na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Hawa ni viongozi wanaowajibika kimaadili kupambana na mambo yote yanayokwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hizi ni juhudi zinazoragibishwa na Mtandao Mpya wa Uhuru Duniani “The Global Freedom Network”. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alikuwa ni kati ya viongozi wakuu wa dini kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ambao tarehe 2 Desemba 2014 walitia mkwaju kwenye Tamko la Pamoja la Kupambana na Utumwa Mamboleo. Utumwa huu unaojionesha kwa namna ya pekee kabisa katika: biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, kazi za suluba, ukahaba, pamoja na mambo yote ambayo yanashindwa kuheshimu na kuthamini utu, heshima na haki msingi za binadamu hayana budi kutamkwa kwamba ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Viongozi wa kidini waliamua kulivalia njuga tatizo hili kwa kuwasaidia watu kwa mawazo na matendo, ili kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, waweze kukomesha utumwa mamboleo, kwani kila binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ana haki ya kupewa heshima na udugu wa kibinadamu. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, kuna uwezekano mkubwa wa kufuta kabisa utumwa mamboleo kutoka katika uso wa dunia na kwamba, huu ni wajibu wa viongozi wa dini kimaadili. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa kidini pamoja na umati mkubwa wa watu uliokuwa umekusanyika mjini Roma kushuhudia tukio hili la kihistoria alisema kwamba, utumwa mamboleo unaendelea kunyanyasa na kudhulumu, utu na heshima ya binadamu, changamoto kwa viongozi wa kidini ni kushirikiana katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo. Hawa ni watu wanaonyanyasika: kimwili, kiuchumi, kingono na kisaikolojia.

Baba Mtakatifu alikumbusha kwamba, Mungu ni upendo na chimbuko la uhuru kamili, unaofungamanisha mahusiano ya kijamii, kwa ajili ya mafao ya wengine katika hali ya usawa na udugu wa kibinadamu. Watu wote ni sawa mbele ya Mwenyezi Mungu na wanapaswa kutambulikana kutokana na utu wao. Viongozi wa kidini anasema Baba Mtakatifu wameamua kujifunga kibwebwe ili kupambana na mfumo mzima wa utumwa mamboleo, unaowaathiri zaidi maskini, kiasi cha kuuzwa kama bidhaa dukani! Wanyonge hawa ndio wanaopaswa kulindwa na kutetewa dhidi ya biashara haramu ya binadamu, ngono na viungo; matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na kazi za suluba wanazofanyishwa watoto, kiasi cha kuathiri malezi na makuzi yao. Utumwa huu unafanyika kila sehemu ya maisha ya mwanadamu na kwamba, tatizo hili linazidi kukua na kuongezeka mwaka hadi mwaka, changamoto kwa viongozi na watu wote wenye mapenzi mema kushikamana kwa dhati dhidi ya utumwa mamboleo, kwa kufanya kwanza toba na wongofu wa ndani, ili kila mtu aweze kuheshimiwa na kuthaminiwa utu na haki zake msingi.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC lilisema kwamba, kila mwanadamu ameumbwa huru na Mwenyezi Mungu; jambo ambalo linapaswa kuendelezwa kwa kujenga na kudumisha mafao ya wengi, usawa na udugu wa kibinadamu kati ya watu. Utumwa mamboleo unaofumbatwa katika biashara haramu ya binadamu, kazi za suluba, ukahaba, biashara ya viungo vya binadamu, ndoa shuruti pamoja na mambo yote yasiyoheshimu na kuthamini utu na heshima ya binadamu, hayana budi kuchukuliwa kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Kwa miaka mingi kumekuwepo na mapambano dhidi ya utumwa mamboleo pamoja na watu kudai haki zao msingi kwa kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi na jinsia; mambo ambayo yananyanyasa utu na heshima ya binadamu. Changamoto kubwa iliyoko kwa wakuu wa dini mbalimbali duniani ni kuhakikisha kwamba, tamko hili linavaliwa njuga ili liweze kutekelezwa katika medani mbalimbali za maisha ya watu. Ni janga linalogusa maisha ya watu: kiuchumi, kijinsia, kisaikolojia pamoja na kudhalilisha wahanga wa vitendo hivi vya kinyama. Mtandao Mpya wa Uhuru Duniani unapania pamoja na mambo mengine: kuhakikisha kwamba, utumwa mamboleo unakomeshwa kwa kung'oa mizizi, ili Jamii iweze kuwa ni mashahidi wa huruma ya Mungu na upendo kwa watu wote waliotumbukizwa katika utumwa mamboleo.

Utumwa Mamboleo
10 August 2021, 14:56