Tafuta

Mama Kanisa tarehe 6 Agosti 2021 ameadhimisha kumbukumbu ya miaka 43 tangu alipofariki dunia Papa Paulo VI. Mama Kanisa tarehe 6 Agosti 2021 ameadhimisha kumbukumbu ya miaka 43 tangu alipofariki dunia Papa Paulo VI. 

Mtakatifu Paulo VI: Majadiliano Katika Maisha na Utume wa Kanisa

Mt. Paulo VI alipenda kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi. Mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki tarehe 21 Juni 1963, kunako tarehe 10 Agosti 1964, akachapisha Waraka wake wa kwanza wa "Ecclesiam suam” yaani "Kanisa la Bwana.” Huu ni Waraka unaonesha dira na mwelekeo wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Katika maadhimisho ya Sherehe ya Kung’ara Bwana, tarehe 6 Agosti, 2021, Mama Kanisa amefanya kumbukumbu ya miaka 43 tangu Mtakatifu Paulo VI alipofariki dunia, yaani tarehe 6 Agosti 1978 akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolf, nje kidogo ya mji wa Roma na kuzikwa tarehe 12 Agosti 1978 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.  Mtakatifu Paulo VI anasema, Sherehe ya Kung’ara kwa Kristo Yesu inaangaza nuru ya ajabu katika maisha ya kila siku ili kufukuzia mbali giza la kifo linalosumbua akili ya mwanadamu. Mlimani Tabor, Yesu anaufunua utukufu na Umungu wake, mbele ya mashuhuda aliowateuwa mwenyewe ili kudhihirisha kwamba, kweli alikuwa ni Mwana mpendwa wa Mungu, Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake. Tukio hili linautukuza ubinadamu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu! Rej. Mk 8:31-34. Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, tarehe 6 Agosti 2021 ameadhimisha kumbukumbu hii chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kuzunguka kaburi la Mtakatifu Paulo VI.

Katika mahubiri yake, amegusia kuhusu fumbo la kifo na ufafanuzi wa maana ya Fumbo hili kadiri ya mwanga angavu wa Roho Mtakatifu. Mtakatifu Paulo VI alilipenda sana Kanisa la Kristo, kiasi hata cha kusadaka maisha yake! Kardinali Marcello Semeraro anasema, tangu mwanzo wa utume wake kama Askofu, amekuza na kudumisha heshima na upendo kwa Mtakatifu Paulo VI aliyefariki dunia akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo. Ni kiongozi wa Kanisa aliyependa kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kama inavyojionesha mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki tarehe 21 Juni 1963, kunako tarehe 10 Agosti 1964, akachapisha Waraka wake wa kwanza wa kichungaji, unaojulikana kama "Ecclesiam suam” yaani "Kanisa la Bwana.” Huu ni Waraka unaonesha dira na mwelekeo wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, kwa kuzingatia changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Ni katika mwelekeo huu, Mtakatifu Paulo VI akafanya hija ya kitume huko katika Nchi Takatifu ili kukutana na kusali na Patriaki Anathegoras, mwanzo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa.

Mtakatifu Paulo VI katika Waraka huu analitaka Kanisa kutambua dhamana na wajibu wake; kuanza mchakato wa kujipyaisha kwa kujielekeza katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Ni Waraka unaojikita katika fadhila ya mapendo kwa Mungu na jirani. Ni kutokana na mwelekeo huu, Kanisa halina budi kuwashirikisha watu upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watu watambue kwamba, Kristo Yesu ndiye ile hazina iliyofichika machoni pa wengi, lakini ni muhimu sana katika maisha ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo! Ilikuwa ni tarehe 6 Agosti 1964, Mtakatifu Paulo VI alipoanza utume wake mjini Vatican kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakati Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Siku kuu ya Kung'ara kwa Bwana, kielelezo cha ufunuo wa Mungu na utukufu wa Kristo, ili kuwaimarisha Mitume wake waweze kukabiliana barabara na Kashfa ya Msalaba. Miaka kumi na minne baadaye, Papa Paulo VI tarehe 6 Agosti 1978, akiwa Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, akafariki dunia, huku akiwa anasali, ile sala kuu, yaani Sala ya Baba Yetu.

Mt. Paulo

 

 

07 August 2021, 14:36