Tafuta

Msalaba wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani 2023 kati ya Mwezi Septemba na Oktoba unatembezwa nchini Hispania. Msalaba wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani 2023 kati ya Mwezi Septemba na Oktoba unatembezwa nchini Hispania. 

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani 2023: Msalaba wa Vijana!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno linapenda kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu kabla na wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023. Kati ya Mwezi Septemba na Oktoba 2021 Msalaba wa Vijana utatembezwa kwenye miji 50 iliyoko nchini Hispania na hatimaye, kilele cha matembezi haya ni mwaka 2023, Msalaba utakapoingia nchini Ureno!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni cheche ya mwanga wa imani, matumaini, mapendo na zawadi kubwa ambayo Mtakatifu Yohane Paulo II ameliachia Kanisa na kwamba, matunda ya maadhimisho haya ni juhudi za sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kabla, wakati na baada ya maadhimisho haya! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni maabara au karakana za imani, kama alivyopenda kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II, enzi zake!  Hapa pamekuwa ni chemchemi na chimbuko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba, Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, limejikuta likiwa na sura ya ujana, pasi na makunyanzi. Hili ni Kanisa ambalo limewasukuma vijana kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vijana wamekuwa kweli ni wadau wa Heri za Mlimani, Manabii wa nyakati hizi na vyombo vya ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Vijana wanapaswa kutambua kwamba, Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa lake; mahali ambapo vijana wanaweza kuchota tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni chombo muhimu sana cha unjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ni mahali ambapo wenye kiu na njaa ya maisha ya uzima wa milele wanaweza kushibishwa kwa kujishikamanisha na upendo wa Kristo Yesu.  Hili ni Jukwaa la majadiliano kati ya Kanisa na Vijana, changamoto kwa pande hizi mbili anasema Mtakatifu Yohane Paulo II, ni kusikilizana kwa makini. Hii ni Epifania na ufunuo wa imani; ni mahali pa kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa vijana. Hii ni amana na urithi mkubwa kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II kwa ajili ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni yatafanyika mwezi Agosti 2023, huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno linapenda kuchukua fursa hii kuanza kuwahamasisha vijana kushiriki kikamilifu kabla na wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023. Ratiba inaonesha kwamba, kati ya Mwezi Septemba na Oktoba 2021 Msalaba wa Vijana utatembezwa kwenye miji 50 iliyoko nchini Hispania na hatimaye, kilele cha matembezi haya ni mwaka 2023, Msalaba wa Vijana utakapoingia nchini Ureno, tayari kwa maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, tarehe 22 Aprili 1984 mara tu baada ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Ukombozi, yaani kuanzia mwaka 1983 hadi 1984, aliwakabidhi vijana Msalaba, alama ya Mwaka Mtakatifu, lakini zaidi kama kielelezo cha upendo na huruma ya Kristo Yesu kwa walimwengu. Ni ushuhuda unaoonesha kwamba, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, mwanadamu ameweza kukirimiwa ukombozi. Tangu wakati huo, Msalaba huu ukajulikana kuwa ni Msalaba wa Vijana, ambao umezunguka na kuzungushwa na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa kipindi cha miaka yote hiyo!

Itakumbukwa kwamba, Msalaba wa Vijana tangu Mwaka 1984 unahifadhiwa kwenye Kituo cha Vijana Kimataifa cha San Lorenzo, kilichoko mjini Roma. Msalaba huu umetembezwa sehemu mbali mbali za dunia sanjari na Sanamu ya Bikira Maria, Afya ya Warumi, “Salus Populi Romani” iliyounganishwa kwenye hija ya Msalaba wa Vijana kwa mara ya kwanza kunako Mwaka 2003. Msalaba wa Vijana umekuwa ni kielelezo cha sala, dhamana ya uinjilishaji na majadiliano ya kina kuhusu imani ya Kanisa Katoliki miongoni mwa vijana na watu wenye mapenzi mema. Msalaba umekuwa ni amana ya imani na ushuhuda wa vijana kwa Kristo na Kanisa lake; ni kielelezo cha imani, matumaini na mapendo kwa wale waliokata tamaa na hasa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ni nafasi kwa vijana wa kizazi kipya kugundua tena ndani mwao ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba, ili hatimaye, kufufua ndani ya nyoyo zao, imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu!

Msalaba Vijana
02 August 2021, 15:01