Tafuta

Kardinali Mauro Piacenza tarehe 2 Agosti 2021 ameadhimisha Siku ya Msamaha wa Assisi kwa Ibada ya Misa Takatifu. Kardinali Mauro Piacenza tarehe 2 Agosti 2021 ameadhimisha Siku ya Msamaha wa Assisi kwa Ibada ya Misa Takatifu. 

Msamaha wa Assisi kwa Mwaka 2021: Huruma & Upendo wa Mungu

Kardinali Mauro Piacenza tarehe 2 Agosti 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la “Santa Maria Degli Angeli in Porziuncola.” Katika mahubiri amegusia kuhusu huruma ya Mungu, Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima; Umuhimu wa Imani inayobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa, kwa kuanza mchakato wa upyaisho kutoka ndani ya Kanisa lenyewe! Huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 4 Agosti 2016 alitembelea mji wa Assisi, mahali alipozaliwa Mtakatifu Francisko wa Assisi ili kusali kwenye Kikanisa cha “Porziuncola” ambacho kwa mapenzi ya Mungu na ugunduzi wa Mtakatifu Francisko wa Assisi, katika kipindi cha miaka 800 kimekuwa ni chemchemi ya neema na baraka kwa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hija hiyo ya binafsi ya Baba Mtakatifu ilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 ya Msamaha wa Assisi. Waamini waliojiandaa barabara na kutimiza masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa wanaweza kujipatia pia rehema kamili katika maadhimisho ya Sikukuu ya Msamaha wa Assisi unaoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Agosti. Askofu mkuu Domenico Sorrentino wa Jimbo Katoliki la Assisi-Nocera Umbra-Gualdo Tadino nchini Italia katika Waraka wake wa Kichungaji kwa Familia ya Mungu Jimboni mwake, anawaalika waamini kuanza upya kwa kujikita katika Msamaha wa Assisi hasa katika kipindi hiki, ambacho Jumuiya ya Kimataifa inakabiliwa na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Huu ni muda wa kusali, kutafakari na kuomba rehema na neema ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Watu wa Mungu wanajiandaa pia kuadhimisha Jubilei ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi na kielele cha maadhimisho haya ni Mwaka 2026. Injili ya Kristo ilikuwa ni mwongozo wa maisha kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi pamoja na wafuasi wake, wakajenga Jumuiya ambayo ilikuwa kama mwili mmoja, roho moja na tumaini moja la wito wao. Familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Assisi-Nocera Umbra-Gualdo Tadino inataka kwa namna ya pekee kabisa kupyaisha: ari na mwamko wake wa kimisionari, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni muda muafaka wa kunogesha Injili ya ndoa na familia inayosimikwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kumbe, ni wajibu wanafamilia kutangaza na kushuhudia uzuri, utakatifu na heshima ya maisha ya ndoa na familia kama njia muafaka ya kuyatakatifuza malimwengu! Familia kadiri ya mpango wa Mungu kama ilivyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu, Mafundisho tanzu ya Kanisa, kanuni maadili na utu wema na familia jinsi ilivyo katika ulimwengu mamboleo ni changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu Injili ya familia!

Ni katika muktadha huu wa maadhimisho ya Msamaha wa Assisi kwa Mwaka 2021, Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume, Jumatatu tarehe 2 Agosti 2021 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la “Santa Maria Degli Angeli in Porziuncola.” Katika mahubiri amegusia kuhusu huruma ya Mungu, Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima; Umuhimu wa Imani inayobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa, kwa kuanza mchakato wa upyaisho kutoka ndani ya Kanisa lenyewe! Kardinali Mauro Piacenza katika mahubiri yake amekaza kusema, Kristo Yesu ni ufunuo wa upendo na huruma ya Baba wa milele. Huruma na upendo ni kiini cha Mwenyezi Mungu pamoja na utambulisho wake. “Deus caritas est”. Ili waamini waweze kuishi kikamilifu upendo na huruma ya Mungu wanapaswa kuzingatia mambo msingi yafuatayo: Jambo la kwanza ni ufuasi wa Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Yn 14:6.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ibada ya Misa Takatifu ni kielelezo cha sadaka ya Kristo Msalabani, chemchemi ya msamaha na wokovu wa binadamu. Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu ni ufunuo wa chemchemi ya upendo, huruma, msamana na imani thabiti. Waamini wanaweza kujichotea huruma, upendo na msamaha wa Mungu kutoka kwenye kisima cha wokovu, lakini kwa namna ya pekee kabisa ni kutoka katika Sakramenti za Kanisa. Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu ni nguzo msingi katika maisha ya waamini. Waamini wajenge utamaduni wa kukimbilia kwenye huruma ya Mungu ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani. Waonje huruma na msamaha wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu! Wajichotee neema na baraka kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, ili kujenga na kudumisha urafiki na mafungamano na Kristo Yesu. Hii ni changamoto kwa waamini kupyaisha maisha na utume wao kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Kusamehe maana yake ni kujiweka katika mazingira ya kusamehe na kusamehewa; kupenda na kupendwa, kwa sababu binadamu ameumbwa kwa ajili ya upendo.

Wakristo wanachota utakatifu wao kutoka kwa Kristo Yesu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanazungumzia wito wa watu wote kuwa watakatifu. “Wafuasi wa Kristo walioitwa na Mungu siyo kadiri ya matendo yao, bali kadiri ya azimio la neema yake na kuhesabiwa haki katika Bwana Yesu, katika Ubatizo wa imani walifanywa kweli watoto wa Mungu na washiriki wa tabia ya Mungu, na hivyo watakatifu halisi” LG. 40. Utakatifu wa Wakristo kabla ya kuwa ni dhamana, ikumbukwe kwamba, ni zawadi ya upendo inayofumbatwa katika imani. Hii ni changamoto kwa waamini kuuvua utu wao wa kale na kuanza kutembea katika mwanga mpya wa imani. Wawe ni watu wenye huruma na mapendo; watambue udhaifu na dhambi zao, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, ili aweze kuwahesabia haki. Wakristo wanapaswa kumuiga Yesu katika maisha yao, kwa kutambua kwamba, utakatifu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe, wanapaswa kuishi kama watakatifu.

“Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.” Kol. 3:12. Utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kushikamana na Kristo Yesu, Mzabibu wa kweli, ili waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Yn 15:5. Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la mitume, chemchemi ya huruma, upendo, msamaha na wokovu wa binadamu. Kanisa linaloundwa na watakatifu pamoja na wakosefu linahitaji kutubu na kumwongokea Mungu, kama njia ya kupyaisha maisha na utume wake katika ulimwengu mamboleo. Bikira Maria ni kielelezo cha utakatifu wa maisha na ni Mama wa huruma ya Mungu. Rej. LG 8.

Baba Mtakatifu Francisko anamtaja Bikira Maria kuwa ni mwanamke ambaye moyo wake ulichomwa kwa upanga, anayeelewa uchungu wa binadamu. Kama Mama wa wote ni alama ya matumaini kwa watu wa Mataifa wanaopitia machungu na magumu ya maisha. Bikira Maria ni mmisionari anayewasindikiza waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani, akifungulia imani mioyo ya waamini moto wake wa upendo wa kimama. Ni Mama anayeshiriki katika mapambano ya changamoto za maisha ya kila siku na pia anashiriki historia yak ila taifa lilipokea Injili na anakuwa kile kinachowabainisha kihistoria. Rej. EG 286.

Msamaha wa Assisi

 

 

02 August 2021, 14:41