Tafuta

Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani inaadhimishwa tarehe 25 Julai 2021: Mama Kanisa kutoa Rehema kamili kwa waamini watakaotimiza masharti. Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani inaadhimishwa tarehe 25 Julai 2021: Mama Kanisa kutoa Rehema kamili kwa waamini watakaotimiza masharti. 

Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani 2021: Rehema Kamili Kutolewa!

Idara ya Toba ya Kitume kwa maelekezo ya Baba Mtakatifu Francisko imeagizwa kutoa Tamko Kuhusu Rehema Kamili inayotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Wazee na Wajukuu inayoadhimishwa tarehe 25 Julai 2021. Waamini waliojiandaa kikamilifu kwa kufuata masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa ili kujipatia rehema kamili, watapata, rehema hii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mafundisho ya imani na ibada ya rehema katika Kanisa yameunganika kabisa na matunda ya Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linafundisha kwamba, Rehema kamili ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa. Huu ni msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata baada ya kutimiza mashari yaliyotolewa na Mama Kanisa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya watakatifu wake. Rehema imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Rehema Kamili au Rehema ya Muda kutokana kwamba, inaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi. Kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili. Nne, asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu.

Mwishoni atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema kamili. Ni katika muktadha huu, Idara ya Toba ya Kitume: "Penitenzieria Apostolica", kwa maelekezo ya Baba Mtakatifu Francisko imeagizwa kutoa Tamko Kuhusu Rehema Kamili inayotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Wazee na Wajukuu inayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Waamini waliojiandaa kikamilifu kwa kufuata masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa ili kujipatia rehema kamili, watapata. Ikiwa kama watawatembelea na kuwahudumia wazee wanaohitaji zaidi msaada au wenye ulemavu. Wanaweza kuwatembelea na kuonana nao mubashara au kuwasaidia kwa njia ya mitandao ya kijamii. Wazee, wagonjwa na walemavu wanaweza kujipatia rehema kamili ikiwa kama kutoka katika undani wa nyoyo zao, wataweza kutubu na hatimaye, kujiunga na vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Kwa kusali Rozari Takatifu, Kufanya Njia ya Msalaba au kuhudhuria Ibada nyingine zinazotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya maadhimisho haya.

Wazee, wagonjwa na walemavu wajitahidi walau kusali: Kanuni ya Imani, Baba Yetu na Salam Maria kwa kutolea mahangaiko yao kwa Mwenyezi Mungu katika imani na upendo kwa jirani zao, kama njia ya kutimiza malipizi ya dhambi zao pamoja na kusali kwa nia za Baba Mtakatifu, pale itakapowezekana. Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume anapenda kutumia fursa hii kutoa mwaliko kwa Mapadre waliopewa dhamana ya kuungamisha waamini, kutekeleza dhamana na wajibu huu, uwepo na utayari wao wa kusikiliza maungamo kama kielelezo cha upendo wa shughuli za kichungaji. Tamko hili ni halali tu, kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani kwa Mwaka 2021. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani itakayokuwa inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Nne ya Mwezi Julai. Na kwa mwaka huu ni hapo Jumapili tarehe 25 Julai 2021. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao!

Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya unanogeshwa na kauli mbiu: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani na Wajuu wao yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20: Hii ni ahadi ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya na wazee, kushirikishana na hatimaye, kuwa ni wadau pia katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wazee wanahamasishwa kutumia ujuzi, uzoefu na mang’amuzi yao kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa dunia, ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Baba Mtakatifu anasema, wazee wengi wana kumbukumbu ya machungu katika maisha, lakini ikumbukwe kwamba, kumbukumbu ni sehemu ya maisha na kama ikutumiwa vyema inaweza kusaidia mchakato wa ujenzi wa dunia inayosimikwa katika msingi wa haki na ukarimu na kwamba, msingi wa maisha ya kweli ni kumbukumbu! Sala ya wazee ina nguvu kiasi hata cha kuweza kuulinda ulimwengu. Kwa hakika wazee ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Wazee ni watu muhimu sana katika historia ya binadamu. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani iwe ni fursa ya kuwapenda zaidi, ili hatimaye, kujifunza kutoka kwao kama waalimu, walinzi na warithishaji wa hekima na busara kwa vijana wa kizazi kipya. Mama Kanisa anapenda kuwaambia na kuwahakikishia wazee kwamba, ataendelea kuwa pamoja na wazee hadi ukamilifu wa dahali!

Rehema Kamili

 

21 July 2021, 16:26