Tafuta

Siku ya Wazee na Wajukuu Wao: Muda Muafaka wa kuenzi na kudumisha Injili ya huruma, upendo na mshikamano. Siku ya Wazee na Wajukuu Wao: Muda Muafaka wa kuenzi na kudumisha Injili ya huruma, upendo na mshikamano. 

Siku ya Wazee na Wajukuu Duniani kwa mwaka 2021: Ujumbe Maalum!

Wito wa wazee duniani ni kulinda mapokeo, amana na utajiri wa jamii ili kuweza kuurithisha kwa kizazi kipya pamoja na kuwalinda vijana katika hija ya maisha yao hapa duniani ili wasijikwae, wakateleza na hatimaye kukengeuka! Wazee hata katika uzee wao, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu . Wazee na vijana wanahitajiana na kukamilishana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Kwanza ya Wazee Duniani, Jumapili tarehe 25 Julai 2021 unanogeshwa na kauli mbiu: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. Hii ni ahadi ya uwepo endelevu na fungamani wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya na wazee, kushirikishana na hatimaye, kuwa ni wadau pia katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wito wa wazee duniani ni kulinda mapokeo, amana na utajiri wa jamii ili kuweza kuurithisha kwa kizazi kipya pamoja na kuwalinda vijana katika hija ya maisha yao hapa duniani ili wasijikwae, wakateleza na hatimaye kukengeuka! Wazee hata katika uzee wao, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi kieleweke kwa msaada na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Wazee na vijana wanahitajiana, ili kukamilishana katika hija ya maisha yao na hakuna mtu anayeweza kujiokoa peke yake.

Baba Mtakatifu anawataka mababu, mabibi na wazee kujikita katika nguzo kuu tatu za maisha: Ndoto, Kumbukumbu na Sala kama kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kwa waja wake. Kwa bahati mbaya sana, wazee katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia wanaonekana kana kwamba, ulimwengu mamboleo si mahali pao tena, pengine ingewabidi kutafuta mahali pa kuishi. Wazee ni watu wanaotelekezwa na ndugu na jamaa zao. Wananyimwa haki zao msingi na huduma muhimu kama vile afya; mara nyingi ni watu wanaoteseka sana kutokana na utamaduni wa kifo ambao unaendelea kuwanyemelea watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Wazee wamegeuzwa kuwa ni walezi wa wajukuu zao vijijini wakati watoto wao wenyewe “wanakula bata kwa mrija” huku wakiendelea kutesa kwa zamu.” Jambo hili ni hatari sana kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya watu wa Mungu. Wazee wengi hawakuwa na kipato cha kutosha, kiasi cha kuwawezesha kufurahia maisha ya uzeeni na hasa ikiwa kama wazee hawa walikuwa ni waadilifu. Kumbe, vijana wanapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi na watoto, ndugu na jamaa ili kujenga uchumi wa kaya zao. Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kuthaminiwa mchago wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na kutetea, kulinda na kudumisha haki zao msingi.

Kwa upande wake, Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales anasema, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wajenge na kudumisha utamaduni wa kuwathamini na kuwaenzi wazee kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na chemchemi ya matumaini kwa watu wa Mungu. Waamini watambue kwamba, kila mtu ni zawadi ya Mungu kwa jirani yake; kumbe, ni wajibu kumshukuru Mungu kwa zawadi hizi. Wazee wajengewe mazingira ya kurithisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, Kiutu na Kitamaduni kwa vijana wa kizazi kipya. Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, CEE, linakaza kusema, Mwenyezi Mungu daima yuko kati pamoja na waja wake hadi utimilifu wa dahari. Kristo Yesu anaendelea kuwa ni rafiki na mwandani wa safari ya maisha ya kiroho na watu wake licha ya matatizo na changamoto mbalimbali za maisha na hasa wakati huu, Jumuiya ya Kimataifa inapokabiliana na janga na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Katika hali na mazingira kama haya, wazee wengi wamekumbwa na hofu na hata wazee wengi zaidi kupoteza maisha yao. Kumbe, kuna haja ya kutangaza na kuenzi uwepo mwanana wa wazee katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Vijana na wazee wajenge utamaduni wa ujirani mwema, ili wote kwa pamoja waweze kusaidiana katika kuinjilishana, huku wakiongozwa na imani thabiti kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kanisa lijenge sera na utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wazee washirikishwe katika sera na mikakati ya ujenzi wa Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia uaminifu wa upendo wa Mungu. Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno linasema, watu wa Mungu katika marika yao, wanapaswa kukua, kukomaa na kuendelea kujizatiti katika upendo unaomwilishwa kwenye mahusiano na mafungamano ya kijamii. Hii ni changamoto ya kudumisha utamaduni wa umoja, upendo na ukarimu wa kidugu unaokita mizizi yake katika Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno kwamba familia zitaenedelea kujenga umoja, upendo na mshikamano wa kidugu, ili kweli familia ziweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani. Waamini wamwombe Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia mapaji yake saba, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, tayari kulisaidia Kanisa kusoma alama za nyakati na kuendelea kujipyaisha zaidi, ili hatimaye, liwe ni Kanisa moja, takatifu katoliki na la mitume.

Kanisa lishuhudie ushiriki wa watoto wake katika maisha na utume wa Kanisa, tayari kujielekeza katika mchakato wa uinjilishaji mpya. Yote haya yasaidie kuleta toba na wongofu wa ndani, maskini na wazee wakipewa kipaumbele cha kwanza. Nalo Baraza la Maaskofu Katoliki Australia, linawataka wazee kusimama kidete kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Watambue kwamba, bado wana wito na utume wa kuinjilisha na kurithisha imani na tunu msingi za maisha kwa vijana wa kizazi kipya. Changamoto katika sekta ya afya, ustawi na maendeleo ya jamii zisaidie kuboresha hali na maisha ya wazee, ili waendelee kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake, Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linatoa wosia kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha ujirani mwema na wazee, kwa njia ya huduma ya upendo na hasa kwa wazee ambao wako majumbani. Kipindi hiki ambacho kuna maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, waamini wajenge moyo wa ujirani mwema, udugu na mshikamano wa kibinadamu. Wazee washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wasiwasahau kuwakumbuka na kuwaombea pia Mapadre na Watawa wazee waliosadaka maisha yao katika mchakato wa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu!

Maadhimisho Wazee

 

24 July 2021, 14:55