Tafuta

Mkutano wa utangulizi wa mifumo ya chakula: mkazo matumizi ya chakula asilia pamoja na kuwawezesha wakulima vijijini. Mkutano wa utangulizi wa mifumo ya chakula: mkazo matumizi ya chakula asilia pamoja na kuwawezesha wakulima vijijini. 

Mkutano wa Utangulizi wa Mifumo ya Chakula Roma: Chakula Asilia

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika hotuba yake elekezi amekazia zaidi kuhusu ongezeko la baa la njaa duniani kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Kupungua kwa ubora wa chakula na lishe sanjari na kuanza kutoweka kwa chakula asilia kutoka katika jamii ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuwalisha wenye njaa na kuwanywesha wenye kiu ni dhamana ya kimaadili kwa Kanisa la Kiulimwengu. Chakula na maji ni kati ya haki msingi za binadamu na haki nyingine zote zinapata umuhimu wake katika: Chakula na Maji, changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga moyo wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata chakula na maji safi na salama kwa ajili ya matumizi yao kama sehemu ya haki msingi za binadamu pasi na ubaguzi. Yesu mwenyewe anasema kwamba, Yeye ni mkate wa uzima wa milele na anapenda kuwaalika wote wenye njaa na kiu kujongea mbele yake ili aweze kuwalisha na kuwanywesha. Matendo haya ya huruma kimwili, yanajenga mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu ambaye amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma ya Baba wa milele! Kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba, chakula kinatumiwa vyema, mwaliko kwa familia ya binadamu kuhakikisha kuwa, inatumia vyema rasilimali za dunia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Rasilimali hizi si kwa ajili ya mafao ya watu wachache ndani ya jamii; wala kwa ajili ya mahangamizi ya binadamu mwenyewe, bali ni kwa ajili ya kuendeleza huduma fungamani inayojikita katika ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Watu wajifunze kuheshimu, kutunza na kugawana chakula na jirani zao kama kielelezo cha Injili ya ukarimu, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu! Serikali ya Italia kuanzia tarehe 26 hadi 28 Julai 2021 kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, inaendesha mkutano wa utangulizi wa Mifumo ya Chakula (UN Food Systems Summit, Unfss) kama sehemu ya maandalizi ya Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika Jijini New York, Marekani, mwezi Septemba 2021 kuhusu Maendeleo ya Mifumo ya Chakula mintarafu Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa wajumbe wa mkutano huu amesema kwa ufupi kwamba, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yameendelea kusababisha uharibifu kwa mazingira na ukame kwa maisha ya kiroho.

Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuzalisha chakula kingi na cha kutosha mahitaji ya watu, lakini kwa bahati mbaya bado kuna umati mkubwa wa watu unaopekenywa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, ukosefu wa maji safi na salama pamoja na tiba muafaka kwa magonjwa yanayowasumbua binadamu. Hii ni kashfa inayokwenda kinyume cha haki msingi za binadamu. Kwa upande wake, Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika hotuba yake elekezi amekazia zaidi kuhusu ongezeko la baa la njaa duniani kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Kupungua kwa ubora wa chakula na lishe sanjari na kuanza kutoweka kwa chakula asilia kutoka katika jamii ya binadamu! Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na maboresho makubwa ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa kutumia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, bila kuwasahau wakulima wadogo wadogo vijijini ambao wanachangia sana katika uzalishaji wa chakula kwa mahitaji ya familia zao na ziada kwa ajili ya kujiongezea uwezo wa kiuchumi. Kuna uhusiano mkubwa katika mnyororo wa uzalishaji wa chakula, wakazi na mahali mazao ya chakula yanapotoka.

Mkutano wa Utangulizi wa Mifumo ya Chakula wa Umoja wa Mataifa (UN Food Systems Summit, Unfss) ni muhimu sana, ili kuwakumbusha walimwengu kwamba, baa la njaa linazidi kuongezeka kutokana na madhara ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Leo hii kuna changamoto kubwa ya ugavi wa chakula kutokana na UVIKO-19, jambo ambalo linawaacha mamilioni ya watu wakisiginwa kwa baa la njaa sehemu mbalimbali za dunia. Kuna haja ya kuangalia mfumo wa uzalishaji na matumizi ya chakula asilia, ili hatimaye, kuanza kupunguza utegemezi wa chakula kinachozalishwa viwandani na ambacho kwa asilimia kubwa kimejaa kemikali. Uzalishaji wa mazao ya chakula asilia upewe kipaumbele cha pekee ili kuweza kukabiliana na changamoto ya matumizi mabaya ya ardhi pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anakaza kusema, watu mahalia kwa miaka mingi walikuwa na mifumo bora ya uzalishaji na utunzaji bora wa chakula, lakini leo hii, hawana soko tena. Uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, ukame pamoja na majanga ya moto yanayoendelea kusikika sehemu mbalimbali za duniani ni changamoto ya kujerea tena katika mifumo ya uzalishaji wa chakula kwa ajili ya matumizi ya nyumbani badala ya kukimbilia uzalishaji wa mazao ya chakula kwa ajili ya biashara, kwa kusukumwa na nguvu ya uchumi. Tafiti mbalimbali zilizofanywa na: Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO; Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo wa Umoja wa Mataifa, IFAD pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, zinaonesha mchango mkubwa unaoweza kutolewa na watu mahalia katika mchakato wa mapambano ya baa la njaa duniani.

Watu mahalia wakiwezeshwa kiuchumi wanaweza kuchangia sehemu kubwa ya mapambano dhidi ya la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani. Uzalishaji wa mazao ya chakula unapaswa kuongezeka maradufu ili kuweza kuwalisha watu bilioni 9 ifikapo mwaka 2050 kadiri ya takwimu za FAO. Wazalishaji wadogo wadogo wa mazao ya chakula, wajengewe uwezo ili kuchangia zaidi katika mfumo wa uzalishaji wa chakula duniani.

Baa la Njaa

 

28 July 2021, 15:41