Tafuta

Papa Francisko amemteuwa Mh. Padre Stephano Musomba, OSA na Mh. Padre Henry Mchamungu kuwa Maaskofu wasaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania. Papa Francisko amemteuwa Mh. Padre Stephano Musomba, OSA na Mh. Padre Henry Mchamungu kuwa Maaskofu wasaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania. 

Maaskofu Wasaidizi Jimbo Kuu DSM: Stephano Musomba & Henry Mchamungu

Mheshimiwa sana Padre Stephano Musomba, wa Shirika la Waugustiani, OSA, hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mavurunza. Mwingine ni Mheshimiwa sana Padre Henry Mchamungu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, ambaye hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Jaalimu wa Sheria za Kanisa Seminari kuu ya Segerea! Dar ni raha tupu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amewateuwa Maaskofu wasaidizi wawili kwa ajili ya Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania. Walioteuliwa ni Mheshimiwa Padre Stephano Musomba, wa Shirika la Waugustiani, OSA, hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mavurunza, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Mwingine ni Mheshimiwa Padre Henry Mchamungu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, ambaye hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Jaalimu wa Sheria za Kanisa Seminari kuu ya Karol Lwanga, Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam na Rais wa Mahakama ya Kanisa na Katibu wa Tume ya Sheria za Kanisa, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Askofu Msaidizi mteule Stephano Musomba, OSA, alizaliwa tarehe 25 Septemba 1969 Kijijini Malonji, Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi na Kitawa, akaweka nadhiri zake za daima tarehe 25 Septemba 2002. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 24 Julai 2003. Kati ya mwaka 2004 hadi mwaka 2008 alikuwa mjini Roma kwa masomo ya Mababa wa Kanisa kwenye Taasisi ya Mababa wa Kanisa ya Augustianum na huko akajipatia Shahada ya Uzamili. Kama Padre ametekeleza utume wake kama Paroko-usu, Mlezi katika nyumba ya Shirika kati ya mwaka 2016 – 2018 huko Morogoro na Jaalimu katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Jimbo Katoliki la Morogoro kuanzia mwaka 2008-2009. Tangu mwaka 2008 amekuwa ni Katibu wa Shirika, nchini Tanzania, Paroko wa Parokia ya Temboni, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Hadi kuteuliwa kwake, amekuwa ni Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mavurunza, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Askofu Msaidizi mteule Henry Mchamungu, alizaliwa tarehe 8 Januari 1965 huko Legho, Kilema, Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 24 Januari 1994 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tangu wakati huo, kama Padre amewahi kuwa Mkurugenzi wa Miito Jimbo kuu la Dar es Salaam kati ya mwaka 1994 hadi mwaka 1998. Mlezi na Jaalimu wa Sheria za Kanisa, Seminari kuu ya Segerea kati ya mwaka 1998-1999. Baadaye akatumwa na Jimbo kuu la Dar es Salaam kujiendeleza zaidi kwenye Chuo Kikuu cha CUEA, Nairobi kati ya mwaka 1999 hadi mwaka 2001. Aliporejea, akatumwa kwenda kufundisha Seminari kuu ya Segerea na kuwa Hakimu wa Mahakama ya Jimbo kuu la Dar es Salaam kati ya mwaka 2001 hadi 2006. Baadaye alitumwa na Jimbo kuu la Dar es Salaam kujiendeleza zaidi katika Sheria za Kanisa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Katholische Privat-Univesität Linz”, huko nchini, Austria kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2011 na kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa. Hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam alikuwa ni Jaalimu wa Sheria za Kanisa Seminari kuu ya Karol Lwanga, Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam na Rais wa Mahakama ya Kanisa na Katibu wa Tume ya Sheria za Kanisa, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Jimbo kuu la Dar es Salaam

 

07 July 2021, 15:00