Tafuta

Mwili wa Hayati Kardinali Laurent Monsengwo kurejeshwa Kinshasa tarehe 17 Julai 2021 Mwili wa Hayati Kardinali Laurent Monsengwo kurejeshwa Kinshasa tarehe 17 Julai 2021 

Mwili wa Kardinali Laurent Pasinya Kurejeshwa Kinshasa 17 Julai 2021

Mwili wa Hayati Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa, unatarajiwa kuwasili Jijini Kinshasa tarehe 17 Julai 2021 na utapelekwa moja kwa moja kwenye Kanisa kuu, ili waamini na watu wenye mapenzi mema waweze kutoa heshima zao, kusali na kumwombea. Tarehe 20 Julai Ibada ya Misa na Maziko ni tarehe 21 Julai 2021. Jembe, RIP.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, amefariki dunia Jumapili tarehe 11 Julai 2021 Kwenye Hospitali ya “Clinique de l'Europe, Le Port-Marly”, mjini Versailles nchini Ufaransa akiwa na umri wa miaka 81 tangu alipozaliwa. Taarifa kutoka Jimbo kuu la Kinshasa, zinasema kwamba, Mwili wa Hayati Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa, unatarajiwa kuwasili Jijini Kinshasa tarehe 17 Julai 2021 na utapelekwa moja kwa moja kwenye Kanisa kuu, ili waamini na watu wenye mapenzi mema waweze kutoa heshima zao, kusali na kumwombea. Baadaye Mwili utapelekwa kwenye Chumba cha kuhifadhia maiti, Hospitali ya Mtakatifu Yosefu hadi Jumanne tarehe 20 Julai 2021, Siku ya Ibada rasmi ya mazishi itakayoadhimishwa kwenye uwanja wa Bunge. Hapo watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya DRC watatoa heshima zao za mwisho. Maziko yenyewe yatafanyika kwenye Kanisa kuu tarehe 21 Julai 2021 majira ya asubuhi baada ya Liturujia ya sala ya mwisho pamoja na kumpatia buriani, Hayati Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa.

Hayati Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Kinshasa nchini DRC alizaliwa tarehe 7 Oktoba 1939 huko Mongobelè. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi kutoka Chuo Kikuu cha Urbanian kilichoko mjini Roma, tarehe 21 Desemba 1963 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Ni kati ya wanafunzi mahiri wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu na Mwafrika wa kwanza kupata “Summa Cum Laude” ya Maandiko Matakatifu. Alibahatika kufundisha Maandiko Matakatifu na Taalimungu, Seminari kuu ya Mtakatifu Yohane XXIII pamoja na Kitivo cha Taalimungu, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Kinshasa, DRC. Tarehe 13 Februari 1980 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Inongo nchini DRC na kuwekwa wakfu tarehe 4 Mei 1980. Tarehe 7 Aprili 1981 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo wa kuu la Kisangani. Tarehe 1 Septemba 1988 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kisangani.

Tarehe 6 Desemba 2007, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa. Amekuwa ni mshiriki mzuri katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu: Uinjilishaji na urithishaji wa imani ya Mwaka 2012, Changamoto za kichungaji kwa familia katika muktadha wa Uinjilishaji ya mwaka 2014, Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia ya mwaka 2015. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Aprili 2013 akamteuwa kuwa ni kati ya Makardinali wake washauri katika mchakato wa kufanya mageuzi makubwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Amefariki dunia wakati Muswada wa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” ikiwa katika hatua zake za mwisho mwisho kabla ya kuzinduliwa rasmi. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 20 Novemba 2010 akamteuwa na kumsimika kuwa ni Kardinali. Mwezi Oktoba 2018 akang’atuka kutoka Baraza la Makardinali Washauri.

Tarehe 1 Novemba 2018, Baba Mtakatifu Francisko akaridhia kung’atuka kwake kutoka madarakani. Na Jumapili tarehe 11 Julai 2021 akaiga dunia, akiwa amewatumikia watu wa Mungu kama Padre kwa muda wa zaidi ya miaka 57. Kama Askofu mwenye dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu ametumikia kwa miaka 41 na kama Kardinali miaka 10. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 81. Waamini wanatakiwa kuchukua tahadhari wakati wa maombolezo na hatimaye maziko ya Kardinali Pasinya dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Kard. Pasinya
14 July 2021, 15:53