Tafuta

Biashara ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu! Biashara ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu! 

Biashara Haramu ya Binadamu na Mifumo ya Utumwa Mamboleo!

Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni uhalifu mkubwa dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu; mambo ambayo wakati mwingine yanafumbiwa macho na jamii, lakini umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inatokomeza kabisa biashara ya binadamu na athari zake. Waathirika zaidi ni wakimbizi na wahamiaji duniani! Walindwe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha ni taasisi ya kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo kilichozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2014, ili kupambana na saratani hii ya kijamii, inayodhalilisha: utu na heshima ya binadamu kwa kuwatumbukiza watoto, wasichana na wanawake katika utumwa mamboleo. Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni uhalifu mkubwa dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu; mambo ambayo wakati mwingine yanafumbiwa macho na jamii, lakini umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inatokomeza kabisa biashara ya binadamu na athari zake. Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha, kinaongozwa na Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, kwa kushirikiana na wakuu wa Majeshi ya Polisi na Maaskofu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kikundi hiki kinaendelea kufanya kazi kwa pamoja, ili kung'oa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; utumwa mamboleo pamoja na kutoa huduma za kichungaji na kijamii kwa wahanga wa vitendo hivi vya kinyama dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Askofu William Kenney, CP, mwanachama wa Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha, amemwandikia waraka Bwana Priti Patel, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, kwa kuitaka Serikali ya Uingereza kuhakikisha kwamba, vyombo vya ulinzi, usalama, sheria na haki vinakuwa na nguvu ya kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watuhumiwa wote wa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, ili haki iweze kushika mkondo wake. Anasema, wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa wasipolindwa wanaweza kutumbukia kwenye mikono isiyokuwa salama na hatimaye, kuishia mikononi mwa wafanyabiashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Askofu William Kenney, CP, anasema, kuna haja kwa Uingereza kuimarisha miundombinu kwa ajili ya kuwatambua na kuwasaidia wahanga wa biashara na mifumo hii hatari kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Serikali ya Uingereza inapaswa kutambua kwamba, bado kuna utumwa mamboleo na wala makosa haya ya jinai si ya kufikirika kama wanavyodhani baadhi ya watu. Ni wakati muafaka kwa Serikali ya Uingereza kujielekeza zaidi katika kuwashughulikia kisheria wale wote wanaojihusisha na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na utumwa mamboleo, badala ya kuwakamata na kuwatia nguvuni waathirika wa biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Kwa Serikali ya Uingereza kuweka vizuizi vipya kwa watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, vinaweza kuchangia kwa watu wengi zaidi kutumbukizwa katika mikono ya wafanyabiashara ya utumwa mamboleo na mifumo yake.

Nyanyaso

 

 

28 July 2021, 15:05