Tafuta

Askofu mkuu Alain Paul Charles Lebeaupin alifariki dunia tarehe 24 Juni 2021 na kuzikwa tarehe 9 Julai 2021 mjini Roma. Askofu mkuu Alain Paul Charles Lebeaupin alifariki dunia tarehe 24 Juni 2021 na kuzikwa tarehe 9 Julai 2021 mjini Roma. 

Hayati Askofu Mkuu Alain P. C. Lebeaupin: Upendo na Huduma!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 9 Julai 2021 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Askofu mkuu Alain Paul Charles Lebeaupin usingizi wa amani na maisha ya uzima wa milele miongoni mwa watakatifu huku akiwa na matumaini ya ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Ni Shuhuda wa Upendo na Huduma kwa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mama Kanisa katika busara na hekima inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu anasema, “Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa” Mt 25:13. Tarehe 24 Juni 2021 Askofu mkuu Alain Paul Charles Lebeaupin, mtaalam mshauri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican alifariki dunia ghafla akiwa chumbani mwake mjini Roma. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Ijumaa tarehe 9 Julai 2021 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Askofu mkuu Alain Paul Charles Lebeaupin usingizi wa amani na maisha ya uzima wa milele miongoni mwa watakatifu wa Mungu, huku akiwa na matumaini ya ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Kardinali Pietro Parolin, katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa kukesha na kuomba, tayari kuungana na Kristo Yesu katika Ufalme wake wa milele kama kielelezo cha utimilifu wa maisha ya mkristo yanayopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo. Hakuna mtu mwenye haki ya wokovu, lakini waamini wote wanahamasishwa na Kristo Yesu kujibidiisha katika maisha yao ya kila siku, huku wakiendelea kujiaminisha mbele ya Mungu, ili Bwana Arusi atakapokuja awakute wakiwa tayari na taa zao zikiwaka.

Daima wakumbuke kuchukua mafuta ya akiba ya upendo na huduma kwa watu wa Mungu.  Kristo Yesu anasema, “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.” Yn 15:13-15. Upendo na huduma ni ushuhuda uliojikita katika maisha ya Askofu mkuu Alain Paul Charles Lebeaupin kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa katika ujumla wake Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni alikuwa amemteua Askofu mkuu Alain Paul Charles Lebeaupin kuwa mtaalam mshauri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Alain Paul Charles Lebeaupin alizaliwa tarehe 2 Machi 1945 huko Paris, nchini Ufaransa. Baada masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 28 Juni 1975 alipewa daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo Katoliki la Nice, nchini Ufaransa.

Alianza utume wake wa Diplomasia ya Kanisa kunako mwaka 1979 na kutumwa huko New York, Marekani, Jamhuri ya Watu wa Dominikan na Msumbiji.Tarehe 7 Desemba 1998, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Ecuador na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu. Tarehe 6 Januari 1999 akawekwa wakfu kuwa Askofu mkuu. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, tarehe 14 Januari 2005 akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Kenya na Mwakilishi wa Vatican kwenye Makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi, UN-Habitat pamoja na Shirika la Mazingira Duniani (UNEP). Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, tarehe tarehe 23 Januari 2012 akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican kwenye Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU. Katika maisha na utume wake, alikuwa ni kiongozi aliyekita utume wake katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi; ili kujenga na kudumisha umoja na urafiki kati ya Mataifa, Makanisa mahalia pamoja na Vatican. Kunako mwaka 2012 alipata ajali mjini Roma, ambayo ilipelekea afya yake kuzorota sana.

Alikuwa ni mchungaji aliyebahatika kuwa na kipaji cha kusikiliza kwa makini. Askofu mkuu Alain Paul Charles Lebeaupin, alikuwa ni mtu wa haki na upendo wa dhati; akajisadaka bila ya kujibakiza katika upendo na huduma ya upendo ndani ya Kanisa. Tarehe 16 Novemba 2020 akang’atuka rasmi kutoka madarakani. Ilipogota tarehe 27 Machi 2021, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa mtaalam mshauri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Tarehe 24 Juni 2021 akafariki dunia na mazishi yake kufanyika tarehe 9 Julai 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Tanzia
10 July 2021, 15:25