Tafuta

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kuanzia tarehe 9-12 Juni 2021 linaendesha Jukwaa la Furaha ya Upendo Ndani ya Familia. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kuanzia tarehe 9-12 Juni 2021 linaendesha Jukwaa la Furaha ya Upendo Ndani ya Familia. 

Furaha ya Upendo Ndani ya Familia: Jukwaa la Utekelezaji!

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kuanzia tarehe 9 hadi 12 Juni 2021 linaendesha Jukwaa la Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, ili kutathini mahali ambapo hadi sasa Kanisa limefikia katika mchakato wa utekelezaji wa Wosia wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko takribani miaka mitano iliyopita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” yalizinduliwa hapo tarehe 19 Machi 2021 na yatahitimishwa rasmni mjini Roma wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo la maadhimisho ya ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni: kujitahidi kunafsisha furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini, tayari kujitoa na kujisadaka kuwa ni chemchemi ya furaha kwa ndugu, jamaa na jirani; zawadi kubwa kwa Mama Kanisa na jamii katika ujumla wake. Pili, hii ni fursa ya kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa familia kama Kanisa dogo la nyumbani; shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani. Tatu, waamini wanakumbushwa kwamba, Sakramenti ya Ndoa inapyaisha upendo wa kibinadamu.

Kumbe, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwa familia na vijana, kwa kukazia malezi, katekesi na majiundo awali na endelevu, kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani inayoweza kutolewa ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko! Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kuanzia Jumatano tarehe 9 Juni 2021 hadi Jumamosi tarehe 12 Juni 2021 linaendesha Jukwaa la Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, ili kutathimini mahali ambapo hadi sasa Kanisa limefikia katika mchakato wa utekelezaji wa Wosia wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko takribani miaka mitano iliyopita. Hii ni fursa ya kuangalia utekelezaji wa Wosia huu wa Kitume kwa kuzama na kuangalia maisha na malezi endelevu ya ukatekumeni katika maisha ya ndoa na familia. Ni wakati wa kusikiliza shuhuda kutoka kwa wanandoa ili kupata: uzoefu, mang’amuzi, matatizo, fursa na changamoto katika maisha ya ndoa na familia. Ni wakati wa kukazia majiundo makini na endelevu kwa wale wote ambao wamepewa dhamana na wajibu wa kuwasindikiza wanandoa katika maisha yao.

Ni wakati wa kushuhudia pia upendo unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ndoa. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, Agano la Ndoa ambalo kwa njia yake, mwanaume na mwanamke huunda kati yao jumuiya kwa maisha yote, kwa tabia yake ya asili liko kwa ajili ya manufaa yao na kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Agano hili kati ya wabatizwa, limeinuliwa na Kristo Bwana kwa hadhi ya Sakramenti. Wanandoa wanaendeleza upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ambao unapaswa kujidhihirisha kwa kuzaa na kutunza uumbaji. Na Mwenyezi Mungu akawabarikia na kuwaambia: Zaeni mkaongezeke, mkajaze nchi na kuitiisha. Rej. Mwa. 1:27; 1 Yoh.4:8, 16. Huu ni umoja usiovunjika wa maisha ya wanandoa hawa wawili kwa sababu “Hata wamekuwa si wawili tena bali mwili mmoja”. Mt. 19:4. “Aliowaunganisha Mungu mwanadamu asiwatenganishe”. Mt. 19:6. Mema na matakwa ya Mapendo ya Ndoa yanadai: Umoja na kutovunjika; Uaminifu na upendo wa kweli sanjari na uwazi kwa uzazi na malezi ya watoto kama kielele cha taji lao kwa kukumbuka kwamba, watoto ni zawadi bora ya Ndoa na wanachangia sana kwa mema ya wazazi wenyewe.

Uzazi wa mapendo ya ndoa hujieneza pia kwa matunda ya maisha adili, maisha ya kiroho na ya kimungu ambayo wazazi wanayarithisha kwa watoto wao kwa njia ya malezi na makuzi makini. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha litazungumzia pia kuhusu tasaufi ya maisha ya ndoa na familia, kwa kupata ushuhuda kutoka kwa Utume wa Familia kama sehemu ya malezi na majiundo endelevu ya maisha ya ndoa na familia. Familia ni kitovu cha uinjilishaji mpya, kumbe, wanafamilia wanapaswa kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari wakitambua kwamba, kwa njia ya Ubatizo wanashiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo Yesu katika maisha yao! Ni wakati muafaka wa kupembua kwa kina na mapana kuhusu udhaifu na mapungufu katika maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu; kuporomoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; uchoyo na ubinafsi; athari za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa, kudhohofika kwa imani na matendo ya kidini pamoja na hali ngumu ya maisha. Mwishoni, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha litawasilisha Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia”: 19 Machi 2021 hadi 26 Juni 2022.

Jukwaa la Upendo
09 June 2021, 16:28