Tafuta

Shirikisho la Mashirika ya Misaada Kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO kuanzia tarehe 21 hadi 24 Juni 2021: Umoja na mshikamano katika huduma. Shirikisho la Mashirika ya Misaada Kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO kuanzia tarehe 21 hadi 24 Juni 2021: Umoja na mshikamano katika huduma. 

Mkutano wa 94 wa ROACO: 21-24 Juni 2021: Mshikamano & Huduma!

ROACO, kuanzia Jumatatu tarehe 21 Juni hadi Alhamisi tarehe 24 Juni 2021 linaadhimisha Mkutano wake wa 94 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho hili. Hiki ni kipindi cha kusali na kuwaombea wafadhili wa ROACO , amani na utulivu Mashariki ya Kati. Ni muda wa kutathimini mchango wa Ijumaa kuu 2021; hali halisi katika Nchi Takatifu, Ethiopia, Siria, Armenia, Georgia na Lebanon.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO, kuanzia Jumatatu tarehe 21 Juni hadi Alhamisi tarehe 24 Juni 2021 linaadhimisha Mkutano wake wa 94 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho hili. Hiki ni kipindi cha kusali na kuwaombea wafadhili wa ROACO ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia huduma mbalimbali zinazotolewa na ROACO kwa Makanisa ya Mashariki. Ni nafasi pia kwa ajili ya kuendelea kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kuingilia kati na kuwakirimia waja wake amani, utulivu wa kisiasa, kijamii na kidini; mambo ambayo pia yamechangiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuenea kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Wajumbe wa ROACO pamoja na mambo mengine, watajadili kwa kina na mapana hali ya Nchi Takatifu, kwa kuwasikiliza viongozi wakuu wa Makanisa mjini Yerusalemu. Hii ni nafasi pia ya kujadili kuhusu Sadaka na Mchango wa Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu: "Pro Terra Sancta" kwa Mwaka 2021. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1974, Mtakatifu Paulo VI alihimiza sana umuhimu wa uwepo endelevu wa Kanisa katika Nchi Takatifu, kama amana na urithi wa imani; ushuhuda endelevu wa Jumuiya ya Wakristo unaoonesha jiografia ya ukombozi. Tangu wakati huo, Kanisa linaendelea kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoteseka kunyanyaswa na hata kuuwawa huko Mashariki ya Kati, lakini hasa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kutoka kwa Makanisa yote duniani, ni alama ya upendo na mshikamano wa Kanisa kwa watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu. Huu ni ushuhuda wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika uekumene wa damu, huduma na sala pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu katika misingi ya: haki, amani na maridhiano. Ni kwa njia ya ushuhuda wa umoja, upendo na mshikamano Kanisa linataka kuwajengea waamini na watu wote wenye mapenzi huko Mashariki ya kati Injili ya amani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi ili kuondokana na: vita, vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kiimani, dhuluma na nyanyaso kwa misingi ya kidini. Wajumbe pia watapata nafasi ya kusikiliza taarifa kutoka Ethiopia, Armenia na Georgia. Mabalozi wa Vatican kutoka Siria, Lebanon na Iraq watatoa taarifa ya hali halisi katika nchi wanamoiwakilisha Vatican. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje ya Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican atatoa hotuba elekezi.

ROACO 2021

 

21 June 2021, 15:06