Tafuta

ROACO imefungua rasmi mkutano wake wa 94 kwa Ibada ya Misa Takatifu ROACO imefungua rasmi mkutano wake wa 94 kwa Ibada ya Misa Takatifu 

Mkutano wa 94 wa ROACO: 21 - 24 Juni 2021: Ibada ya Misa Takatifu!

Kardinali Leonardo Sandri, Jumanne, tarehe 22 Juni 2021 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya ufunguzi rasmi wa mkutano wa ROACO kwa mwaka 2021. Katika mahubiri yake, Kardinali Sandri ametolea nia ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafadhili waliokwisha kutangulia mbele ya haki, wakiwa na tumaini la ufufuko na maisha ya uzima wa milele. Uinjilishaji wa kina!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, (R.O.A.C.O. Riunione Opere Aiuto Chiese Orientali), kuanzia Jumatatu tarehe 21 Juni hadi Alhamisi tarehe 24 Juni 2021 linaadhimisha Mkutano wake wa 94 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho hili. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ambaye pia ni Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumanne, tarehe 22 Juni 2021 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya ufunguzi rasmi wa mkutano wa ROACO kwa mwaka 2021. Katika mahubiri yake, Kardinali Sandri ametolea nia ya Misa Takatifu kwa ajili ya wafadhili waliokwisha kutangulia mbele ya haki, wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Wajumbe wamewaombea wafadhili walio hai kwa ukarimu, sadaka na majitoleo yao kwa ajili ya kugharimia miradi mbalimbali inayoendeshwa na ROACO. Amewakumbusha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko yuko pamoja nao kwa njia ya sala na baadaye wataweza kupata nafasi ya kuzungumza naye mubashara. Ametafakari kuhusu chanzo cha habari za Abramu, wito wake na safari yake kuelekea Kanaani na Misri; kinzani na migawanyiko iliyotokea katika familia ya Abramu.

Huu ni uzoefu na mang’amuzi ya maisha ya kila siku kwa wale wanaoitwa kuacha yote na kuamua kumfuasa Mwenyezi Mungu. Imani kwa Mwenyezi Mungu kamwe haiwezi kuwafanya waja wake kuachana na historia, bali wanashirikishwa katika fursa, magumu na changamoto zake. Hii ni changamoto kwa waamini kusikiliza kwa makini ahadi na maagano yao na Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Abramu ambaye Mwenyezi Mungu aliahidi kuupatia uzao wake nchi ya ahadi. ROACO inapaswa kufikiri na kutenda kwa unyenyekevu, huku ikiendelea kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu ili kutekeleza miradi mbalimbali inayobuniwa, kupangwa na kutekelezwa na ROACO. Kama wajumbe wa ROACO wanaitwa kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kila siku kama kielelezo cha huduma kwa Mungu, jirani na Makanisa ya Mashariki. ROACO ni chombo cha uinjilishaji na huduma makini kwa watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati.

Neno la Mungu ni chemchemi ya maisha. Waamini wanahimizwa kuingia kwa kupitia mlango ulio mwembamba, ili waweze kuingia katika maisha ya uzima wa milele, vinginevyo wataingia upotevuni. Neno wa Mungu amefanyika mwili na kukaa kati ya waja wake, ili aweze kuwashirikisha utajiri wake unaobubujika kutoka katika ufukara wake. Kama wafuasi wa Kristo Yesu wanaalikwa kufuata njia nyembamba. Yale wanayotaka watendewe na watu, wao pia wanapaswa kuwatendea wengine vivyo hivyo kwani hii ndiyo Torati na Manabii. ROACO inapaswa kuendelea na kubaki kuwa ni chombo cha huduma ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima Kiroho na kimwili.

Mkutano mkuu wa ROACO ni muda muafaka wa kusali na kuwaombea wafadhili ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia huduma mbalimbali zinazotolewa na ROACO kwa Makanisa ya Mashariki. Ni nafasi pia kwa ajili ya kuendelea kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kuingilia kati na kuwakirimia waja wake amani, utulivu wa kisiasa, kijamii na kidini; mambo ambayo pia yamechangiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuenea kwa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Wajumbe wa ROACO pamoja na mambo mengine, watajadili kwa kina na mapana hali ya Nchi Takatifu, kwa kuwasikiliza viongozi wakuu wa Makanisa mjini Yerusalemu. Hii ni nafasi pia ya kujadili kuhusu Sadaka na Mchango wa Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu: "Pro Terra Sancta" kwa Mwaka 2021. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1974, Mtakatifu Paulo VI alihimiza sana umuhimu wa uwepo endelevu wa Kanisa katika Nchi Takatifu, kama amana na urithi wa imani; ushuhuda endelevu wa Jumuiya ya Wakristo unaoonesha jiografia ya ukombozi. Tangu wakati huo, Kanisa linaendelea kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoteseka kunyanyaswa na hata kuuwawa huko Mashariki ya Kati, lakini hasa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kutoka kwa Makanisa yote duniani, ni alama ya upendo na mshikamano wa Kanisa kwa watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu. Huu ni ushuhuda wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika uekumene wa damu, huduma na sala pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu katika misingi ya: haki, amani na maridhiano. Ni kwa njia ya ushuhuda wa umoja, upendo na mshikamano Kanisa linataka kuwajengea waamini na watu wote wenye mapenzi huko Mashariki ya kati Injili ya amani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi ili kuondokana na: vita, vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kiimani, dhuluma na nyanyaso kwa misingi ya kidini. Wajumbe pia watapata nafasi ya kusikiliza taarifa kutoka Ethiopia, Armenia na Georgia. Mabalozi wa Vatican kutoka Siria, Lebanon na Iraq watatoa taarifa ya hali halisi katika nchi wanamoiwakilisha Vatican. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje ya Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican atatoa hotuba elekezi.

ROACO 2021

 

22 June 2021, 15:44