Tafuta

Kardinali Raniero Cantalamessa: Yatakatifuzeni malimwengu kwa Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Kardinali Raniero Cantalamessa: Yatakatifuzeni malimwengu kwa Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu 

Yatakatifuzeni Malimwengu kwa Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu

Kardinali Raniero Cantalamessa asema, Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” kinapaswa kuwa ni kiini cha utamadunisho, chimbuko la upendo, mawazo, ujuzi na maarifa. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanahitaji kunogeshwa kwa Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya tunu msingi za maisha ya kiroho, yaani: imani, upendo matumaini na faraja kwa watu wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya: imani, upendo, huruma, msamaha, uvumilivu, uaminifu na unyenyekevu wa Mungu, aliyejinyenyekesha na kujifanya kuwa mdogo, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake unaoleta maisha na uzima wa milele!  Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale juu Msalabani, askari alipomchoma Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama za Sakramenti za Kanisa. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Margherita Maria Alacoque akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hiki ni kielelezo cha ndani kabisa cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha na kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika kwa mara nyingine tena Mapadre na waamini walei kujichotea utajiri wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika Waraka wa Kitume wa Papa Pio XII, “Haurietis acqua” wa Mwaka 1956 kuhusu “Moyo Mtakatifu wa Yesu kiini cha huruma ya Mungu”. Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” Jimbo kuu la Milano, kilianzishwa ili kujibu hitaji la mahali pa malezi na majiundo makini ya vijana nchini Italia.

Changamoto hii ikavaliwa njuga na Padre Agostino Gemelli na wasaidizi wake wa karibu akina Armida Barelli na Giuseppe Toniolo. Na matokeo yake katika kipindi cha uhai wake miaka 100 iliyopita, Chuo hiki kimeendelea kukua na kupanuka na hatimaye, kuwa ni jukwaa la malezi na majiundo makini ya kielimu kitaifa na kimataifa! Ni kati ya vyuo vikuu vya kikatoliki maarufu sana Barani Ulaya. Kuna wanafunzi 43, 302 wanaopata elimu bora inayokidhi viwango vya soko la ajira Barani Ulaya. Ni chuo ambacho kimewekeza sana katika tafiti makini, ili kuendelea kusoma alama za nyakati. Haya ni matokeo ya sadaka kubwa ya akili na ukarimu inayotekelezwa na wadau wa Jumuiya ya Chuo Kikuu, bila kusahau kwamba, wanafunzi wana imani na wanathamini sana mchango huu. Kumbe, kuna haja ya kukazia ari na mwamko wa kimisionari, tayari kutoka na kuanza kufanya tafiti za ukweli, ustawi na maendeleo ya wengi. Chuo Kikuu kiwe ni mfano bora wa kuigwa katika ukarimu, huduma makini kwa wanafunzi, kwa kutafuta na kuambata mafao ya wengi, sanjari na kupambana na changamoto mamboleo kuhusu: utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; mifumo mbalimbali ya ubaguzi, ukosefu wa haki, amani, maridhiano na umaskini duniani.

Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri Mkuu wa Nyumba ya Kipapa, Alhamisi tarehe 17 Juni 2021 ameadhimisha Ibada ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kama sehemu ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore”, Hospitali ya Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma. Katika mahubiri yake, Kardinali Cantalamessa amewashirikisha wanajumuiya hawa uzoefu wake kama mwanafunzi, jaalimu na mhubiri wa nyumba ya Kipapa kwa takribani miaka 41 sanjari na Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu imekuwa ni fursa ya kuwakumbuka na kuwaombea, wale wote aliokutana nao katika hija ya maisha yake kama mwanafunzi na jaalimu chuoni hapo. Kunako mwaka 1979 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa na hivyo kulazimika kuacha shughuli zote za kufundisha Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore”, na kuanza kujikita zaidi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Sasa imegota miaka 41 na katika Kipindi cha Majilio na Kwaresima, amekuwa akitoa Tafakari kwa: Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na sasa Papa Francisko. Hi huduma anayoitekeleza kwa unyenyekevu na moyo mkuu! Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake kutoka katika Maandiko Matakatifu. “Lakini walimpomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu, lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. Yn 19: 33-34.

Kristo Yesu ndiye lile Hekalu ambalo wamelivunja na sasa linabubujika Damu na Maji. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Moyo Mtakatifu wa Yesu, umekuwa ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Hii ni Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, lakini pia ni ushuhuda unaofumbata mchakato mzima wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa ufupi kabisa, Fumbo la Pasaka ni kiini cha utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, Kerygma “κήρυγμα”. Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa mkuki, umekuwa ni mwanga wa maisha ya waamini. Ni katika muktadha huu, Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” kinapaswa kuwa ni kiini cha utamadunisho, chimbuko la upendo, mawazo, ujuzi na maarifa. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanahitaji kunogeshwa kwa Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya tunu msingi za maisha ya kiroho, yaani: imani, upendo na matumaini. Huu ni mwaliko kwa waamini kuondokana na upendo bandia kama ilivyo pia katika akili bandia, kwa kujikita zaidi katika upendo kwa sababu Mungu ni upendo. Deus Caritas Est! Huu ni mwaliko wa kuingiza moyo wa upendo katika shughuli mbalimbali za tafiti, sayansi na masomo. Yote haya yawe ni kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Hata miongoni mwa wagonjwa, kuna sura na mfano wa Mungu; watu wanaopaswa kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa. Matumaini yana nguvu zaidi kuliko hata dawa anayopewa mgonjwa. Kamwe maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, yasichukue nafasi ya mwingiliano, umoja, upendo na mshikamano na wagonjwa.

Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri Mkuu wa Nyumba ya Kipapa amehitimisha mahubiri yake kwa sala ifuatayo: “Jesu mitis set humilis corde, fac cor nostrum secundum cor tuum” yaanui: “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na moyo wako.” Itakumbukwa kwamba, tarehe 13 Aprili 2021, Askofu mkuu Mario Delpin wa Jimbo kuu la Milano aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Hii ilikuwa ni sehemu ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” Jimbo kuu la Milano, kilipoanzishwa. Maadhimisho hayo yalikuwa ni fursa ya kufungua Mwaka wa Masomo 2021-2022. Rais Sergio Mattarella wa Italia aliwatumia ujumbe kwa maadhimisho haya. Wanafunzi waliohitimu masomo yao Chuo hapo walitoa shukrani za dhati kwa Chuo kuwawezesha kupata elimu, ujuzi na maarifa. Leo hii wamekuwa ni watu tofauti kabisa. Askofu mkuu Mario Delpin katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa wanafunzi kusoma kwa juhudi, bidii na maarifa. Wanafunzi wajifunze vyema ili kuelewa mambo badala ya kukariri. Waondokane na maamuzi mbele kwa kudhani kwamba, tayari wanajua ili kusoma kwa bidii na kuondokana na uvivu, tayari kushangazwa na maajabu ya Mungu.

Masomo ya Chuo Kikuu yanapania kumwandaa mwanafunzi kufahamu mema na mabaya, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa watu wa Mungu. Ni changamoto ya kujifunza kwa nadharia na vitendo. Wanafunzi wanapaswa kuzama katika undani wa masomo yao, ili kuelewa vyema zaidi, tayari kuwashirikisha wengine mang’amuzi haya. Tasaufi ya wanazuoni ni mchakato unaowahamasisha kuwa na ari na moyo wa kusonga mbele hadi kufikia lengo linalokusudiwa kwa kuonesha moyo wa shukrani, kila mtu kadiri ya historia ya maisha yake. Wanazuoni wanapaswa kuwajibika katika mchakato wa kutekeleza utume wao, ili hatimaye, siku moja waweze kuwa ni mashuhuda wa matendo makuu ya Mungu aliyowatendea katika maisha yao. Wanazuoni wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa: uaminifu na uadilifu; weledi na ubora wenye viwango, ili kupandikiza mbegu ya imani na matumaini kama kielelezo cha utakatifu wa maisha ya kila siku.

Wanafunzi wa Chuo kikuu, wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha, imani, sadaka, huruma, upendo na msamaha wa kweli, kielelezo cha upya wa maisha unaobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka. Askofu mkuu Mario Delpin wa Jimbo kuu la Milano anasema, ameamua kutoa mahubiri mintarafu mazingira waliyomo. Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” inaadhimishwa wakati ambapo dunia imepigishwa magoti kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Huu ni mwaliko wa kuadhimisha Jubilei hii katika hali ya unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani, tayari kumpokea Kristo Yesu, ili aweze kuwa ni mwandani wa maisha, huku wakiendelea kuchota amana na utajiri wa huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Moyo Mtakatifu
19 June 2021, 08:45