Tafuta

Mama Evaline Malisa Ntenga: Wanawake Ndani ya Kanisa: Changamoto ya Sinodi. Mama Evaline Malisa Ntenga: Wanawake Ndani ya Kanisa: Changamoto ya Sinodi. 

Evaline Ntenga: Wanawake Ndani ya Kanisa: Changamoto ya Sinodi!

“Wanawake Ndani ya Kanisa: Changamoto ya Sinodi” ni mada ambayo imejadiliwa na Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC kama sehemu ya maandalizi ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa WAWATA, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anadadavua changamoto za wanawake ndani ya Kanisa.

Mama Evaline Malisa Ntenga, WAWATA, Dar es Salaam, Tanzania.

Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ni wazo lililotolewa kwa mara ya kwanza na Mtakatifu Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kuanza kumwilisha dhana hii katika maisha ya Makanisa mahalia; Mabaraza ya Maaskofu; Mashirikisho ya Kanda hadi kufikia Kanisa la Kiulimwengu. Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema, Sinodi ni chombo cha kimisionari na uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa wengine.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia watu wote wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ndicho kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya maisha yao. Anahimiza umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa ili kujichotea nguvu, neema na baraka na hatimaye kujisadaka bila ya kujibakiza katika maisha na utume wa Kanisa. Katika ulimwengu mamboleo, kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji! Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa.

Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inazingatia mambo yafuatayo: Ufahamu wa kina wa Neno la Mungu, Mafundisho Jamii ya Kanisa, Katekisimu ya Kanisa Katoliki; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; pamoja na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Sinodi ya XVI ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2021-2023 itanogeshwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume”. Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC “Wanawake Ndani ya Kanisa: Changamoto ya Sinodi” ni mada ambayo imejadiliwa na Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC kama sehemu ya maandalizi ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Bi Maria Lia Zervino amezungumzia kuhusu umuhimu wa Kanisa kutambua mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa, ili kushirikisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ni sehemu ya mbinu mkakati wa maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Mbegu hii ya dhana ya Sinodi inapaswa kupandikizwa, ili hatimaye, iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Wakati huo huo, Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA katika mahojiano maalum na Radio Vatican anazungumzia kuhusu “Wanawake Ndani ya Kanisa: Changamoto ya Sinodi”. Ninaposikia Habari za Kanisa la Kisinodi napenda kurejea nukuu kutoka Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican zinazotuelezea kwamba kupitia ubatizo washiriki wote wa Kanisa wanapata karama na kipawa cha Roho Mtakatifu na kwamba jamii nzima ya Kikristo inakamilika wakati waamini wake wanapogundua umuhimu wa kutafakari na kujadili kwa sauti moja juu ya masuala yahusuyo maadili na imani. Nafasi ya kila mmoja wetu katika kulijenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, kuanzia kwa Baba Mtakatifu kwenda chini inawezekana tu pale tunapokubali na tunapotambua kuwa Kanisa linaishi.  Na hivyo kila siku kama Kanisa tunahitaji kujifunza kutoka kwa wengine ikiwa ni pamoja na wanawake, vijana na Watoto (ama kwa namna nyingine makleri wana ya kujifunza kutoka kwa walei na walei wajifunze kutika kwa makleri).

Kanisa hili haliwezi kuwa Kanisa linaloishi ikiwa halitatambua nafasi ya mwanamke katika ujenzi wa Kanisa. Kanisa likubali pia kuwa uhitaji wa mwanamke kushirikishwa haumaanishi kupewa mamlaka ya kubeza hiarakia wala kutaka demokrasia kama ilivyo katika ulingo wa siasa bali kuhakikisha kuwa mwanamke huyu anatumia mapaji na karama alizojaliwa na Mungu katika kumtangaza na kumshuhudia Kristo mfufuka. Ukisoma Injili ya Luka Sura ya 8:1-3 utaona Habari za wanawake walioponywa wakati Yesu anapita katika vijiji na miji akihubiri, tunaambiwa akina mama hawa baada ya kupona Maria (aitwaye Magdalene), Yoana mke wa Kuza, mfanyakazi mkuu wa Herode; Susana na wengine kadhaa walimtumikia Yesu kwa mali zao. Kuna changamoto ya ushiriki wa wanawake ama kushirikishwa katika maamuzi kwenye Mabaraza ya Waamini Walei kwa sababu ya namna mifumo ilivyowekwa kutokuwa rafiki kutokana na ukweli kuwa mwanamke huyu anategemewa kuwa mama, kuwa mke, kuwa mlezi, kuwa mtafuta mkate na kadha wa kadha na wakati anahangaika na haya maamuzi yalishafanywa aidha kwa sababu ya muda ama hakukuwa na namna bora ya kushirikishwa. Jambo hili linapaswa kutazamwa kwa mtazamo wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa kanisa ili kuhakikisha kwamba maamuzi yanayofikiwa pia yanamwezesha huyu mwanamke kuendelea kuwajibika huku akishiriki ujenzi wa Kanisa hili linaloishi bila kulega katika makuzi na malezi ya familia na Kanisa katika ujumla wake!

Kanisa liweke sera na mikakati ya makusudi ya kuwasikiliza: wanawake, vijana, watoto na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.  Na hiyo ndio namna pekee ya kuishi na kumwilisha Maandiko Matakatifu ambayo yanatuelekeza kuwa katika sura ya Kimungu, kwani sote tuna nafasi sawa katika kushiriki ujenzi wa Fumbo la mwili wa Kristo yaani Kanisa katika: nyanja za imani, yaani maisha ya kiroho, uchumi na kijamii kwa ujumla. Baba Mtakatifu ameanza kuwashirikisha wanawake katika Nyanja mbalimbali za uongozi katika Kanisa la Kiulimwengu. Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwaka 2020 Baba Mtakatifu Francisko alimteua Bi Maria Lia Zervino ambae ni Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC kuwa mshauri kwa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Tunategemea kuona haya yakifanyika katika ngazi zote za Kanisa hadi kwenye jumuiya ndogondogo za Kikristo huku Kanisa likiwajengea wanawake mazingira rafiki ili kuleta ile sura ya upendo, na moyo wa huruma katika maisha na utendaji wa Kanisa katika kuihudumia jamii na kuyatakatifuza malimwengu.

Wakati huo huo, Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, linayo ndoto ya kutaka kuona kwamba: Wanawake wanateuliwa pia katika Mahakama zinazohusiana na masuala ya ndoa na talaka. Wanawake wanataka kushirikishwa katika malezi na makuzi ya majandokasisi; wawe ni walezi watakaowaongoza pia waseminari katika safari ya maisha yao ya kiroho! Wanawake waendelee kushirikishwa katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Wafundwe vyema, ili waweze pia kujipambanua katika kusimamia haki msingi za binadamu! Hapa ni wanawake wote, yaani watawa na waamini walei. Ushiriki wa wanawake katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, uangaliwe upya, ili kuleta uwiano mzuri zaidi utakaosaidia kupokea maoni ya wanawake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo katika ujumla wake. Ni wakati muafaka wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa!

Wanawake na Sinodi
19 June 2021, 16:36