Tafuta

Askofu mkuu Ivan Jurkovic ameteuliwa na Papa Francisko kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Canada Askofu mkuu Ivan Jurkovic ameteuliwa na Papa Francisko kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Canada 

Askofu Mkuu Ivan Jurkovic Balozi wa Vatican Nchini Canada

Askofu mkuu Ivan Jurkovič alizaliwa tarehe 10 Juni 1952 huko Kocevje, nchini Slovenia. Akapadrishwa tarehe 29 Juni 1977. Tarehe 28 Julai 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Belarus na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu na hatimaye kuwekwa wakfu tarehe 6 Oktoba 2001 na Kardinali Angelo Sodano, wakati huo akiwa Katibu mkuu wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Ivan Jurkovič, kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Canada. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Ivan Jurkovič alikuwa ni Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss. Askofu mkuu Ivan Jurkovič amewahi pia kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Urussi na Uzbekistan. Alizaliwa tarehe 10 Juni 1952 huko Kocevje, nchini Slovenia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi akapadrishwa tarehe 29 Juni 1977. Ilipogota tarehe 28 Julai 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Belarus na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu na hatimaye kuwekwa wakfu tarehe 6 Oktoba 2001 na Kardinali Angelo Sodano, wakati huo akiwa Katibu mkuu wa Vatican. Tarehe 22 Aprili 2004 akateuliwa kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Ukraine. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 19 Februari 2011 akamteuwa kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Uzbekistan.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Februari 2016 akamteuwa kuwa Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, nchini Uswiss. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Ivan Jurkovič, alikuwa mstari wa mbele katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene uliohitimishwa mjini Havana, Cuba kwa Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na Patriaki Cyril wa Moscow na Urussi nzima, viongozi wa Makanisa walioandika ukurasa wa historia mpya ya majadiliano ya kiekumene. Askofu mkuu Ivan Jurkovič, anasema, mkutano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Cyril wa Moscow na Urussi nzima ni tukio ambalo lilivuta hisia kubwa si tu kwa Wakristo wa Makanisa haya mawili, bali kama chachu na changamoto ya viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa kujenga utamaduni wa kukutana na kuzungumza uso kwa uso ili kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika maisha ya watu badala ya kuendelea kujenga kuta zinazowatenganisha watu!

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walianzisha mchakato wa majadiliano ya kiekumene na Mtakatifu Paulo VI akakutana na kuzungumza na Patriaki Athenagora, picha ambayo ilijirudia tena huko Havana, Cuba, kwa Baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na Patriaki Cyril wa Moscow na Urussi nzima. Hiki ni kielelezo cha ukomavu na ujasiri wa kiimani; tukio ambalo limekuwa ni faraja kubwa kwa Wakristo na wapenda amani sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni alama ya matumaini mapya katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kwa Makanisa kutembea na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Tamko la kichungaji ni dira na mwelekeo wa mchakato wa majadiliano ya Uekumene wa huduma kati ya Makanisa haya mawili!

Balozi Canada

 

 

05 June 2021, 15:16