Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Mei 2021 amezindua Jukwaa la Kazi la Laudato si "Laudato si Platform of Action LSAP safari shiriki itakayodumu miaka saba kuanzia sasa. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Mei 2021 amezindua Jukwaa la Kazi la Laudato si "Laudato si Platform of Action LSAP safari shiriki itakayodumu miaka saba kuanzia sasa.  

Mwaka wa Laudato si: Jukwaa la Kazi, Sera na Utekelezaji Wake!

Jukwaa la Kazi la Laudato si, linatekelezwa katika kipindi cha miaka saba. Mwaka wa kwanza ni mchakato wa ujenzi wa jumuiya, ushirikishanaji wa rasilimali na utengenezaji wa sera na mikakati ya utekelezaji kadiri ya mwono wa ekolojia fungamani, kwa kusikiliza na kujibu kilio na kujielekeza katika uchumi unaosimikwa katika ekolojia; mtindo wa maisha, elimu na tasaufi ya ekolojia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kama sehemu ya mchakato wa kufunga rasmi maadhimisho ya “Mwaka wa Laudato si”, Jumanne, tarehe 25 Mei 2021, Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kuzinduliwa kwa Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, safari shirikishi ya miaka saba, kama sehemu ya mchakato wa kujizatiti kikamilifu katika maendeleo na ekolojia fungamani. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu ametoa muhtasari wa machapisho muhimu kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Laudato si, ingawa maadhimisho haya yalikumbana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Tema mbalimbali kuhusu: Mwongozo wa Laudato si, Kipindi cha Kazi ya Uumbaji, Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education”, “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko” pamoja na maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani kwa Mwaka 2021. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anasema, kumekuwepo na upandaji mkubwa wa miti sehemu mbalimbali za dunia pamoja na uragibishaji wa utunzaji bora wa mazingira kwa njia ya mitandao ya kijamii.

Baraza linaendelea na mchakato wa kuchapisha Kitabu cha mashuhuda wa “Laudato si” utunzaji bora wa mazingira unaobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya watu, mazingira pamoja na maeneo yao ya kijamii. Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kila mtu akichangia kadiri ya nafasi na uwezo wake. Ni mwaliko wa kushirikishana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa upande wake, Padre Joshtrom Isaac Kureethadam, SDB, Mratibu wa Kitengo cha Ekolojia na Kazi ya Uumbaji, toka Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika uzinduzi wa Jukwaa la Kazi amekazia: Muda wa utekelezaji wa mkakati huu wa maendeleo na ekolojia fungamani; umuhimu wa dhana ya Sinodi katika utekelezaji wake, makundi makubwa yenye dhamana katika ekolojia fungamani na mwaliko wa kujiunga na Jukwaa hili ifikapo tarehe 4 Oktoba 2021.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kuanzisha majadiliano mapya kuhusu namna ya kuujenga mustakabali wa dunia hii, kwa kuwahusisha watu wote kwa sababu changamoto za mazingira zinawahusu na kuwaathiri watu wote. Vipaji vya kila mmoja na ushiriki wake vinahitajika kama vyombo vya Mungu kwa ajili ya kuyatunza maumbile, kila mmoja kadiri ya utamaduni, mang’amuzi, shughuli na vipaji vyake. Rej. “Laudato si”, 14. Jukwaa la Kazi la Laudato si, “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, linatekelezwa katika kipindi cha miaka saba. Mwaka wa kwanza ni mchakato wa ujenzi wa jumuiya, ushirikishanaji wa rasilimali na utengenezaji wa sera na mikakati ya utekelezaji kadiri ya mwono wa ekolojia fungamani, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kujielekeza katika uchumi unaosimikwa katika ekolojia; kwa kujikita katika mtindo wa maisha ya kawaida sanjari na kuendelea kukazia elimu na tasaufi ya ekolojia pamoja na ushirikishwaji wa jumuiya! Mwaka wa Saba, utatumika kumsifu na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Kazi ya Uumbaji.

Utekelezaji wa sera na mikakati ya Jukwaa la Kazi “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, unafanyika mintarafu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Kuna Kamati kuu ya “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, inayoratibiwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu kwa kushirikiana na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, Umoja wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa, USG na UISG, CIDSE, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kanisa Katoliki, Vyama na Mashirika ya Kitume, “Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini”, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM” pamoja na makundi mbalimbali kutoka Barani Afrika na Asia katika ujumla wake. Sekta ya familia inaongozwa na Wafokolari. Sekta ya Parokia na Majimbo na Mabaraza ya Maaskofu iko chini ya Shirika la Misaada na Maendeleo Kimataifa la Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza, CAFOD. Sekta ya shule inaongozwa na Shirika la Mtakatifu Bosco lijulikanalo kama “Don Bosco Green Alliance” pamoja na Kikundi cha Laudato si kutoka Ufilippini.

Sekta ya Shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu inaongozwa na Wayesuit na wadau wengine kutoka Vyuo vikuu. Sekta ya Hospiltali itakuwa chini ya Chama cha Afya Cha Wakatoliki nchini India, CHAI, Vyama vya Afya kutoka Marekani na viongozi wengine kutoka sekta ya afya. Sekta ya Uchumi itaratibiwa na “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko”, CIDSE, VIS, Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, USG na UISG. Huu ni mchakato unaosimikwa katika majadiliano na utekelezaji wake kama jitihada za makusudi za kuyatunza mazingira, kwa ajili ya sas ana wakati ujao. Kwa habari motomoto unaweza kuangalia kwenye anuani ifuatayo ya Mwaka wa Laudato si' (www.laudatosi.va).

Wakati huo huo, Sr. Sheila Kinsey, Katibu mtendaji wa Tume ya Haki, Amani na Mazingira, Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa, USG-UISG ameshiriki katika uzinduzi wa Jukwaa hili. Anasema, kundi hili ni sehemu ya Kamati kuu na lina kazi ya kusikiliza kwa makini, kufanya mang’amuzi na kuamua yale yanayopaswa kutendeka mintarafu karama za Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, kielelezo makini cha unabii unaowajibisha. Huu ni muda wa kuragibisha umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Watu wote wa Mungu watambue kwamba, wao ni vyombo vya Mungu kwa ajili ya kuyatakatifuza maumbile, kila mmoja kadiri ya utamaduni, mang’amuzi, shughuli na vipaji vyake.

Carolina Bianchi ni mhamasishaji wa Wanaharakati wa Mazingira Wakatoliki Duniani, “Global Catholic Climate Movement”, walioshiriki kikamilifu katika kuandaa Jukwaa la Kazi “Laudato si Plaform of Action, LSAP”. Anasema, Jukwaa hili ni muhimu sana katika kuelimisha mwingiliano kati ya binadamu na mazingira yanayopaswa kuheshimiwa, kutunzwa na kuendelezwa, ili kukuza haki ya mazingira. Kwa hakika, Kanisa linaendelea kujipambanua kuwa ni mtetezi wa mazingira nyumba ya wote!

Jukwaa la Laudato si
25 May 2021, 14:42