Tafuta

Vatican News
Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mei Mosi, 2021 ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Mafrateri 24 kutoka katika nchi 13. Kutoka Tanzania kuna ShemasiAchiles Charukula na Edwin Jerome Lyanga Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mei Mosi, 2021 ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Mafrateri 24 kutoka katika nchi 13. Kutoka Tanzania kuna ShemasiAchiles Charukula na Edwin Jerome Lyanga  (Vatican Media)

Kardinali Tagle Atoa Ushemasi Kwa Mafrateri 24 Urbaniana Roma!

Mashemasi wamewekewa mikono kwa ajili ya huduma ya utumishi kwa taifa la Mungu wakiwa na ushirika na Askofu na umoja wa Mapadre wake, katika huduma “Diaconia” ya Liturujia, ya Neno na ya Upendo. Mashemasi waliowekwa kwa ajili ya huduma ya matendo ya huruma wawe na huruma na bidii, wakienenda katika ukweli wa Bwana, aliyejifanya Mtumishi wa wote. Mashemasi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 58 ya Kuombea Miito Ulimwenguni, iliyoadhimishwa Jumapili, tarehe 25 Aprili 2021, ulinogeshwa na kauli mbiu “Mtakatifu Yosefu Ndoto ya Wito”. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amekazia umuhimu wa: Ndoto, huduma na uaminifu; mambo msingi katika kukuza na kudumisha miito mbalimbali ndani ya Kanisa. Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Miito Ulimwenguni yamekwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu uliozinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2020 na yanatarajiwa kufungwa kwa kudema hapo tarehe 8 Desemba 2021. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Mei Mosi, 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi 24 ambao sasa wamewekwa wakfu kuwa: Mitume, Mashuhuda na Wamisionari katika Daraja ya Ushemasi. Mashemasi wapya wanatoka katika nchi 13 kielelezo cha ukatoliki na utume wa Kanisa.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Mashemasi wamewekewa mikono kwa ajili ya huduma ya utumishi kwa taifa la Mungu wakiwa na ushirika na Askofu na umoja wa Mapadre wake, katika huduma “Diaconia” ya Liturujia, ya Neno na ya Upendo. Mashemasi waliowekwa kwa ajili ya huduma ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, wawe na huruma na bidii, wakienenda katika ukweli wa Bwana, aliyejifanya Mtumishi wa wote. Huu ni mwaliko kwa Mashemasi kuungana na kushikamana zaidi na Kristo Yesu aliye njia, ukweli na uzima, kwa kuzama zaidi katika unyenyekevu, kielelezo cha Kristo Yesu aliyekuja kuhudumu na wala si kuhudumiwa! Wakumbuke kwamba, Kristo Yesu ni Mzabibu wa kweli na wao kama Mashemasi ni matawi, bila Yesu hawawezi kufua dafu hata kidogo na kwamba, hii ni neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao na wala si jeuri yao binafsi. Mashemasi watambue kwamba, wamepewa Roho Mtakatifu anayeishi na kutenda kazi ndani mwao, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na utume wao kwa Mama Kanisa. Vinginevyo, maisha yatakuwa machungu, imani itafifia, upendo utaingia mchanga na huduma itakuwa dhaifu kama “Kimbunga cha Jobo” Pwani ya Afrika Mashariki.

Matunda ya Roho yanayokusudiwa kutokana na umoja na mafungamano na Kristo Yesu yanabainishwa na Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Wagalatia 5: 22-23 anapowaalika Wakristo kuenenda kwa Roho, kwani hawatazitimiza kamwe tamaa za mwili, kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho na Roho hushindana na mwili! Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo yote haya hakuna Sheria! Roho Mtakatifu anawasaidia waamini kuwashirikisha wengine Kristo Yesu kama zawadi kubwa kutoka kwa Baba wa milele, tayari kujisadaka kama mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma na upendo. Ulimwengu unachechemea kutokana na “Wachungaji na wahudumu feki”, wanaozalisha “matunda pori” ambayo ni: kiburi, uchoyo na ubinafsi, kijicho na husuda; chuki na hasira; mipasuko na kinzani na hatima ya yote haya ni vita. Mashemasi wapya wanahimizwa kuwa ni mashuhuda wa ukuu wa Kristo Yesu katika huduma inayosimikwa kwenye unyenyekevu, ushuhuda na kwamba, wanaishi na Kristo Yesu!

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle anasema, tunda jingine la kuishi kwa kuungana na kushikamana na Kristo Yesu katika maisha na utume ni ushirikiano katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda. Mtume Barnaba na Mtakatifu Paulo ni mfano bora wa kuigwa kwa kukubali na kupokeana jinsi walivyo na hivyo wakawa ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji. Lakini katika hija ya maisha, bado kusigana kutaendelea kuwepo kama hata ilivyotokea kwa Mtume Barnaba na Mtakatifu Paulo, mwishoni, kila mtu akashika hamsini zake. Lakini waliendelea kuwa wameungana na kushikamana katika Jina la Kristo Yesu, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, na watu wengi zaidi wakapata kusikia Injili ya Kristo. Hawa ni watu waliokuwa wameungana na kufungamana katika: Imani, wakiwa ndani ya Kristo Yesu kwa ajili ya Utume wa Kanisa. Mashemasi wapya waendelee kuungana na kushikamana na Kristo Yesu Mzabibu wa kweli, hata kama matawi yatashindwa kuelewana na kushikamana.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa. Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yasaidie kunogesha Ibada kwa Mtakatifu Yosefu, Mlinzi wa Kanisa.

Mei Mosi 2021 Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kimepata jumla ya Mashemasi Wapya 29. Kati yao waliopewa Daraja Takatifu ya Ushemasi na Kardinali Luis Antonio Tagle ni Mashemasi 24. Kutoka Afrika wamo Mashemasi 11 na kati yao kutoka Afrika Mashariki wamo Mashemasi 5. Hawa ni: Shemasi Charukula Charles Achiles Narcis wa Jimbo Katoliki Kigoma, Tanzania. Shemasi Lyanga Edwin Jerome, Jimbo Katoliki la Ifakara, Tanzania. Shemasi Kayiwa Roberto Jimbo Katoliki la Kasana-Luweero, Uganda. Shemasi Keah Bawar Kharay Duop wa Jimbo Katoliki la Malakal, Sudan ya Kusini. Mwingine katika Orodha hii ni Shemasi Yai Lino Pioth Mangar, kutoka Jimbo Katoliki la Rumbek, Sudan ya Kusini.

Mashemasi Wapya

 

01 May 2021, 17:26