Tafuta

Kardinali Peter Turkson: Haki ya chakula: Kazi, Ubunifu na Fedha iwe ni kwa ajili ya huduma bora ya chakula. Kuna hatari watu zaidi milioni 150 wakakumbwa na baa la njaa duniani. Kardinali Peter Turkson: Haki ya chakula: Kazi, Ubunifu na Fedha iwe ni kwa ajili ya huduma bora ya chakula. Kuna hatari watu zaidi milioni 150 wakakumbwa na baa la njaa duniani. 

Haki ya Chakula: Kazi, Ubunifu na Fedha Kwa Ajili ya Huduma Makini!

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna chakula cha kutosha kuzima baa la njaa duniani, lakini kutokana na uchoyo na ubinafsi matokeo yake ni ongezeko kubwa la baa la njaa duniani. Umaskini, vita, kinzani, ukosefu wa demokrasia na haki msingi za binadamu; uharibifu mkubwa wa mazingirana athari kubwa ni kati ya vyanzo vya baa la njaa na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.  

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuwalisha wenye njaa na kuwanywesha wenye kiu ni dhamana ya kimaadili kwa Kanisa la Kiulimwengu. Chakula na maji ni kati ya haki msingi za binadamu na haki nyingine zote zinapata umuhimu wake katika: Chakula na Maji. Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga moyo wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata chakula bora na maji safi na salama kwa ajili ya matumizi yao kama sehemu ya haki msingi za binadamu pasi na ubaguzi. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kama sehemu ya kumbukizi la Miaka Mitano tangu alipochapisha Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” sanjari na uzinduzi wa Jukwaa la Kazi la Laudato si: “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, anapenda kukazia matendo zaidi. Anaitaka Jumuiya ya Kimataifa: Kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha Maskini, Utunzaji bora wa mazingira na Jukwaa la kazi ili kutekeleza sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote katika kipindi cha miaka saba kuanzia sasa!

Huu ni mchakato wa wongofu wa kiekolojia, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu na Kazi ya Uumbaji, chemchemi ya faraja na matumaini dhidi ya udhalimu. Umoja wa Mataifa tarehe 26 Mei 2021 umeendesha Mkutano wa Pili wa Kimataifa kwa njia ya mitandao, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Haki ya chakula: Kazi, Ubunifu na Fedha kwa ajili ya huduma ya Chakula”. Mkutano huu umewashirikisha wadau mbalimbali katika mchakato wa kupata uhakika na usalama wa chakula duniani na hasa baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo limeacha makovu makubwa katika maisha ya watu, ili hatimaye, Jumuiya ya Kimataifa kuanza kujielekeza katika mchakato wa kuwa na uhakika wa upatikanaji na usalama wa chakula duniani!

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika hotuba yake elekezi amekazia zaidi kuhusu haki ya kupata chakula bora hasa baada ya janga la UVIKO-19 ambalo limeacha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kuna hatari kubwa kwamba, kwa siku za mbeleni, mamilioni ya watu yakatumbukizwa katika baa la njaa na umaskini. Takwimu za FAO zinaonesha kwamba, takribani watu milioni 150 wako hatarini kukumbwa na baa la njaa na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula, sehemu mbalimbali za dunia. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna chakula cha kutosha kuzima baa la njaa duniani, lakini kutokana na uchoyo, ubinafsi na utandawazi wa kutowajali wengine, matokeo yake ni ongezeko kubwa la watu wanaopekenyuliwa na baa la njaa duniani. Umaskini wa hali na kipato, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; ukosefu wa demokrasia na haki msingi za binadamu; uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote pamoja na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya vyanzo vya baa la njaa na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani.

Mambo yote haya yanaendelea kudhohofisha mfumo wa upatikanaji na usalama wa chakula. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, chakula bora ni sehemu ya haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Balaa la njaa ni kashfa kubwa inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau mbalimbali kwa kujenga uchumi fungamani na endelevu; kwa kuondokana na mifumo inayozalisha ukosefu wa haki msingi za binadamu, sanjari na kujikita katika kanuni maadili na utu wema. Jumuiya ya Kimataifa ijenge na kudumisha utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Watu washirikishwe katika mchakato huu na asiwepo hata mtu mmoja anayebaki nyuma ya mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa ijenge mazingira ya usawa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watu wawe na uhakika wa kupata chakula bora na kwa bei wanayoweza kuimudu kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao. Mambo yote haya yanafumbatwa katika msingi wa haki jamii, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na ujenzi wa uchumi unaokita malengo yake kwa mahitaji msingi ya binadamu na utu wake.

Haki ya Chakula
28 May 2021, 15:58