Tafuta

Ujumbe kutoka Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini kwa ajili ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan sanjari na maadhimisho ya Siku kuu ya ‘ID Al-FITR 1442 H. / 2021 A.D Ujumbe kutoka Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini kwa ajili ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan sanjari na maadhimisho ya Siku kuu ya ‘ID Al-FITR 1442 H. / 2021 A.D 

Ujumbe wa Ramadhan na Sikukuu ya ‘ID Al-FITR 1442H./2021 A.D

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limewatumia waamini wa dini ya Kiislam, ujumbe kwa ajili ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na maadhimisho ya Siku kuu ya ‘ID Al-FITR 1442 H. / 2021 A.D. Ujumbe huu unanogeshwa na kauli mbiu “Wakristo na Waislam: Mashuhuda wa matumaini. katika janga la UVIKO-19 watu wanahitaji zaidi fadhila ya matumaini katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Ramadhani inatokana na neno la Kiarabu “ان‎, Ramida au ar-ramad” likimaanisha, ukavu. Ramadhani ni kati ya miezi muhimu sana katika dini ya Kiislamu. Ramadhani ni mwezi mtukufu kwa Waislamu kwa sababu ni katika mwezi huu Mungu (Allah) alimpatia Mtume Muhammad (Salah Allah alaghi wa salaam) sura ya kwanza ya Kuruani Tukufu kunako mwaka 610. Sura hiyo al fatihah yaani ufunguzi, inasomwa yote katika kila sala kwa mwislamu. Hivyo ni maarufu kama Mama wa Kitabu au Mama wa Kuruani (Umm al Kitabu au Umm al Kuruani). Hii ni Sura inayomwalika Muislamu kutambua ukuu wa Mwenyezi Mungu, muweza wa yote; kuomba ulinzi na huruma yake ya daima na kuendelea kumsifu bila kikomo. Ramadhani ni mwezi wa tisa katika Kalenda ya Dini ya Kiislamu, ambapo Waislamu wanaalikwa kufunga, kuacha anasa na kusali zaidi ili, kuwa karibu na Mwenyezi Mungu (Allah). Japo Waislamu wanasali kila siku tena mara tano inaaminika sala katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani inabeba uzito zaidi, kwa kuwa ni katika mwezi huu mtukufu, Mtume Muhammad alikutana na Allah. Ramadhani inaanza rasmi baada ya kiongozi wa dini kutangaza kuona mwezi mpya.

Hiki ni kipindi kwa Waislamu cha kusoma Kuruani, kutafakari na kukua katika maisha ya kiroho yaani kupata thawabu mbele za Mwenyezi. Sala ya usiku katika kipindi hiki kadiri ya ahadi ya Mwenyezi Mungu anayeisali kwa imani na kuomba rehema, dhambi zake za nyuma zote zitafutwa. Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kipindi cha kujenga umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu kwa njia ya mfungo, sala na sadaka inayonafsishwa katika matendo ya huruma. Ni muda unaowawezesha waamini kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao, wanaoishi na kufanya nao kazi. Hii ni fursa ya kuendeleza mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu hasa katika mapambano dhidi ya changamoto za kila siku. Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limewatumia waamini wa dini ya Kiislam, ujumbe kwa ajili ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan sanjari na maadhimisho ya Siku kuu ya ‘ID Al-FITR 1442 H. / 2021 A.D. Ujumbe huu unanogeshwa na kauli mbiu “Wakristo na Waislam: Mashuhuda wa matumaini. Katika kipindi hiki cha janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; watu wengi wameteseka, wakaingiwa na simanzi na hata kukata tamaa ya maisha. Lakini kumekuwepo na mwamko mkubwa zaidi wa mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Kimekuwa ni kipindi ambacho waamini wengi wametarajia kuona na kuonja uwepo wa Mungu kati pamoja nao, hasa wakati wa mahangaiko na mapambano yao dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Wengi wamekimbilia huruma, msamaha, huku wakijiaminisha katika uweza wa Mungu katika mahitaji yao ya kiroho na kimwili. Lakini, kwa wakati huu, watu wanahitaji kuwa na matumaini zaidi. Matumaini ni fadhila ya Kimungu inayomwezesha mwamini kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na maisha ya uzima wa milele. Fadhila ya matumaini inavuvia matendo ya watu, huyatakasa, huwakinga watu na ubinafsi na kuwaongoza watu kwenye furaha inayobubujika kutoka katika upendo wa Mungu kwa waja wake, hata kama mwanadamu atashindwa kufahamu kwa undani zaidi upendo huu wa Mungu. Fadhila ya matumaini inamwezesha mwamini kuona matatizo na changamoto za maisha zina maana, malengo na mafundisho katika maisha yake.

Katika hali ya kukata na kujikatia tamaa, msaada na matumaini yanaweza kuletwa na wale ambao hawakuwatarajia hata kidogo. Kumbe, udugu wa kibinadamu ni chemchemi ya matumaini kwa watu wanaokumbana na shida pamoja na changamoto za maisha. Huu ni ushuhuda wa mshikamano unaotolewa na waamini, kwani udugu wa kibinadamu ni jimbo la kiulimwengu, linalowaunganisha watu wakati wa shida na mahangaiko ya maisha. Udugu wa kibinadamu unavuka mipaka ya: kikabila, kidini, kijamii na kiuchumi. Ni katika hali na mazingira kama haya, waamini wanaweza kumuiga Mwenyezi Mungu, kwa kupendana wao kwa wao sanjari na kutunza mazingira nyumba ya wote. Zote hizi kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko ni alama za matumaini. Fadhila ya matumaini inayo pia maadui wake ambao kimsingi ni: ukosefu wa imani kwa upendo na tunza ya Mwenyezi Mungu; hali ya kutowaamini wengine, kukata na kujikatia tamaa, mambo ya kufikirika, majumuisho ya wote kutokana na mang’amuzi na uzoefu hasi wa maisha. Mawazo na maelekeo mabaya hayana budi kurekebishwa ili kuimarisha matumaini kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kuwaamini jirani.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unakazia sana umuhimu wa kupyaisha matumaini ambayo kimsingi yanapata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Hali hii haijalishi mazingira na historia ya mtu. Uchungu na fadhaa ya mwanadamu na hasa wale wanaoteseka ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya watu wote wa Mungu. Fadhila ya matumaini inawasukuma waamini kujizatiti katika ukweli, wema, uzuri, haki na upendo na hivyo kuwasaidia watu wa Mungu kuwa na mawazo mapana zaidi yanayosaidia maisha kuwa bora zaidi. Kumbe, huu ni wakati wa kujikita zaidi katika mchakato wa kuimarisha fadhila ya matumaini. Wakristo na Waislam wanaitwa na kuhamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini katika maisha ya sasa na yale yajayo. Waamini wanapaswa kuendelea kuwa, wajenzi na wapyaishaji wa fadhila ya matumaini miongoni mwa watu wanaoteseka na wale waliokata tamaa kabisa. Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linawatakia waamini wa dini ya Kiislam, mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan sanjari na maadhimisho ya Siku kuu ya ‘ID Al-FITR 1442 H. / 2021 A.D. Hiki kiwe ni kipindi cha amani, ili kuvuna matunda ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Ujumbe wa Ramadhan
17 April 2021, 16:17