Tafuta

Maadhimisho ya Juma Kuu: Alhamisi Kuu, Karamu ya Bwana: Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na Amri ya Upendo wa udugu wa kibinadamu. Maadhimisho ya Juma Kuu: Alhamisi Kuu, Karamu ya Bwana: Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na Amri ya Upendo wa udugu wa kibinadamu. 

Juma Kuu: Alhamisi Kuu: Ekaristi, Daraja, Upendo na Usaliti!

Alhamisi kuu, Kristo Yesu aliwaachia Mitume wake sadaka ya maisha yake, yaani Mwili na Damu yake Azizi, katika Maumbo ya Mkate na Divai, kama kielelezo cha sadaka yake kuu. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake. Ni zawadi kubwa inayoweza kutolewa na Mwenyezi Mungu peke yake. Ekaristi, Daraja Takatifu na Amri ya Upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Alhamisi Kuu Jioni: “Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye aliwapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo”. Yn. 13:1. Haya ni maneno yanayofuatiwa na kitendo cha Kristo Yesu kuwatawadha wanafunzi wake miguu na kuifuta kwa kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni. Katika Karamu ya Mwisho, Kristo Yesu alijiandaa kujisadaka kwa mateso na kifo cha Msalaba. Maadhimisho ya Jioni ya Alhamisi Kuu yamesheheni matukio mazito katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni siku ambayo Kristo Yesu alianzisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni siku alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu ya Upadre na hatimaye, akawapatia Amri mpya ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa upendo wa udugu wa kibinadamu! Hayo yamesemwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali katika Ibada ya Misa Takatifu, Alhamisi kuu Jioni tarehe 1 Aprili 2021 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Huu ni upendo unaofikia kikomo chake Ijumaa kuu kwa mateso na kifo cha Msalaba unaokomboa. Hiki ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Kristo Yesu kwa binadamu.

Siku ya Alhamisi kuu, Kristo Yesu aliwaachia Mitume wake sadaka ya maisha yake, yaani Mwili na Damu yake Azizi, katika Maumbo ya Mkate na Divai, kama kielelezo cha sadaka yake kuu. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake. Ni zawadi kubwa inayoweza kutolewa na Mwenyezi Mungu peke yake. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni zawadi, amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anatembea na Kanisa lake kama mwanga angavu, nguvu thabiti na lishe bora kwa ajili ya historia ya mwanadamu na Kanisa katika ujumla wake. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba, Sadaka ya Ekaristi Takatifu ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo na utume wa Kanisa katika ujumla wake. Mbele ya Ekaristi Takatifu, mwamini anaweza kujiaminisha kwa Kristo Yesu kwa kumshirikisha yale yaliyoko kwenye sakafu ya maisha ya moyo wake, ili kupata faraja, amani na utulivu wa ndani.

Ekaristi Takatifu ni ukweli ambao waamini wanapaswa kuuamini na kuumwilisha katika uhalisia wa maisha yao. Ni upendo unao wawajibisha kupendana kwa kudumisha upendo wa udugu wa kibinadamu; kusamehe na kuwasaidia wale wote wanaohitaji msaada. Ni upendo unaowataka kuimarisha udugu wa kibinadamu, kwa kuwaambata na kuwakumbatia wote. Huu ni upendo unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na “akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi”; watu wanaoteseka: kiroho na kimwili. Huu ni upendo unaogeuka na kuwa ni mwanga angavu ili hatimaye, kutambua ufunuo wa Uso wa Kristo anayejionesha kati ya ndugu zake hasa wale waliojeruhiwa na wahitaji zaidi. Alhamisi Kuu ni siku ambayo Wakristo wa Kanisa Katoliki wanakumbuka na kuadhimisha, siku ile Kristo Yesu alipoanzisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na kuwaamuru waadhimishe kwa ajili ya ukumbusho wake. Baada ya mateso, kifo na ufufuko wake, akawavuvia na kuwaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” Yn. 20:23. Ni katika muktadha huu, Kristo Yesu aliwaachia Mitume wake mamlaka ya Kikuhani ili kuendeleza maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho zinazolipyaisha Kanisa na kwa wanadamu ikawa ni zawadi kubwa isiyokuwa na kifani.

Kardinali Giovanni Battista Re, anasema, ni Mapokeo ya Mama Kanisa kwamba, katika maadhimisho ya Alhamisi kuu jioni, “Coena Domini” waamini wapate muda mrefu zaidi wa kuabudu Ekaristi Takatifu, huku ikinogeshwa kwa sala na tafakari za kina. Lakini kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, utaratibu huu kwa sasa umesitishwa kwa muda, kama ilivyokuwa hata kwa Mwaka 2020. Lakini, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaporejea majumbani mwao, waendeleze huo moyo wa sala na tafakari kwa kumshukuru Kristo Yesu aliyekubali kubaki daima kama mwandani wa safari ya maisha ya kiroho katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, katika maumbo ya Mkate na Divai. Hii ni chemchemi ya matumaini na nguvu katika mapambano dhidi janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, linaloendelea kusababisha maafa makubwa sehemu mbalimbali za dunia. Watu wamejifunza jinsi ambavyo janga la UVIKO-19 lilivyoipigisha dunia magoti.

Katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, watu wa Mungu wanapaswa kujizatiti kisayansi kwa kufuata ushauri wa wataalam wa afya pamoja na kutekeleza itifaki dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ili mafanikio yaliyokwisha kupatikana yaweze kuendelezwa zaidi badala ya kutumbukia tena kwenye taharuki na hofu ya maambukizi mapya ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kimsingi vita dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni tete sana. Kumbe, silaha za kisayansi, maisha ya kiroho, kijamii na kiuchumi hazina budi kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Hili ni janga ambalo limeleta madhara makubwa katika maisha ya watu kwa kusababisha vifo na ukosefu wa ajira. Limekuwa ni chanzo kikuu cha kuchechemea kwa uchumi kitaifa na kimataifa. Sekta ya elimu katika ngazi mbalimbali imeathirika sana pamoja na kuvuruga mahusiano na mafungamano ya kijamii. Kama Kristo Yesu alivyowafundisha Mitume wake, kwa sasa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanahimizwa kumwendea Mungu kwa sala, toba na kufunga ili kuomba huruma yake isiyokuwa na kifani kwa wakati huu wa janga la UVIKO-19.

Alhamisi kuu wakati wa Karamu ya Mwisho, “Coena Domini”, Kristo Yesu alionesha upendo na urafiki wake wa ajabu kwa wafuasi wake! Lakini kwa bahati mbaya, ni katika siku hii ya Alhamisi kuu, Kristo Yesu aliposalitiwa kwa busu la Yuda Iskariote, kiasi cha kuchafua ule upendo wa Yesu aliokuwa amewapenda watu wake upeo. Hiki ni kielelezo cha udhaifu na mapungufu ya kibinadamu. Alhamisi kuu, iwe ni fursa kwa waamini kuchunguza dhamiri zao na kuangalia undani wa maisha yao na hasa zaidi, dhambi zao, tayari kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha yanayosimikwa katika msamaha wa dhambi. Kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwenyezi Mungu amekuwa karibu zaidi na waja wake. Kumbe, hakuna sababu ya kujisikia wapweke au watu waliotelekezwa. Kwa sababu Mwenyezi Mungu amekuwa daima wa kwanza kuwatafuta waja wake, kuwapenda na kuwataka watubu na kumwongokea, ili kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, waweze tena kupata msamaha na maondoleo ya dhambi. Huu ni upyaisho wa maisha ya kiroho, kwa kuwa na moyo ulio wazi kwa Mwenyezi Mungu na jirani!

Coena Domini
01 April 2021, 18:17