Tafuta

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu limeandaa Kongamano la Kimataifa kwa Ajili ya Wakleri kuanzia tarehe 17 hadi 19 Aprili 2022 Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu limeandaa Kongamano la Kimataifa kwa Ajili ya Wakleri kuanzia tarehe 17 hadi 19 Aprili 2022 

Kongamano la Kimataifa Kwa Ajili ya Wakleri 17-19 Aprili 2022!

Kongamano linatarajiwa kuadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 17 hadi 19 Aprili 2022 na litanaogeshwa na kauli mbiu “Njia ya Sinodi Ni Njia Inayotegemewa na Mungu kutoka kwa Kanisa la Millenia ya Tatu”. Baba Mtakatifu Francisko tangu mwaka 2015 ameendelea kuwahimiza watu wa Mungu kuanza mchakato wa utekelezaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Sinodi ni chombo cha kimisionari na ni sehemu muhimu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea kwa pamoja katika: Sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, mintarafu majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine, na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa wengine. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inazingatia mambo yafuatayo: Ufahamu wa kina wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia watu wote wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” unaokazia ukuhani wa waamini wote. Papa anawahimiza waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa sanjari na kukuza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Anawataka waamini wawe na ari na mwamko wa kimisionari kama chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kielelezo makini cha imani tendaji! Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa.

Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu, akiwa ameandamana na Professa Michelina Tenace pamoja na Padre Vincent Siret, Gambera wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Kifaransa, Roma, Jumatatu tarehe 12 Aprili 2021 wamezungumza na jopo la waandishi wa habari mjini Vatican kuhusu Kongamano la Kimataifa kwa Ajili ya Wakleri. Kongamano linatarajiwa kuadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 17 hadi 19 Aprili 2022 na litanaogeshwa na kauli mbiu “Njia ya Sinodi Ni Njia Inayotegemewa na Mungu kutoka kwa Kanisa la Millenia ya Tatu”. Baba Mtakatifu Francisko tangu mwaka 2015 ameendelea kuwahimiza watu wa Mungu kuanza mchakato wa utekelezaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo ni kuwashirikisha waamini wote katika utume wa Kanisa na utangazaji wa Habari Njema sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kadiri ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Walengwa wakuu wa Kongamano hili ni Maaskofu pamoja na wadau wote wanaopenda kujihusisha na masuala ya kitaalimungu, huku wakisukumwa na upendo kwa ajili ya utume wa Kanisa. Changamoto hii inatekelezwa kwa namna ya pekee kabisa kwa njia ya sala, toba na wongofu wa ndani, kwa ajili ya huduma ya Kanisa kwa watu wote wanaoteseka: kiroho na kimwili. Kardinali Marc Ouellet anasema, huu ni Ukuhani wa Upendo unaotekelezwa na waamini wote kadiri ya wito na majukumu yao ndani ya Kanisa, huku wakikamilishana. Huu ni umoja wa Wakleri, watawa na waamini walei, wenye mapaji na karama mbalimbali za Roho Mtakatifu, wanazoshirikishana na kukamilishana, ili kujenga umoja wa Kanisa la Kristo Yesu na hatimaye, kuwafikia watu wote wa Mungu. Taalimungu pamoja na tafiti makini ni kwa ajili ya Kanisa zima.

Hata hivyo, Kongamano hili la Kitaalimungu haliwezi kujimwambafai kwamba, litakuwa ni jukwaa linalotoa majibu ya matatizo na changamoto za kimisionari ndani ya Kanisa. Lakini litasaidia sana kuimarisha msingi wa utume wa Kanisa. Mama Kanisa anashiriki Ukuhani wa Kristo unaodumishwa na Ukuhani wa Daraja Takatifu na Ukuhani wa waamini walei unaohitaji mapyaisho katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji mintarafu majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni pamoja na ushiriki wa vyama vya Kitume. Dhamana na wajibu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa ni dhana inayopaswa kupewa msukumo wa pekee. Kuna uhaba mkubwa wa Miito sehemu mbalimbali za dunia kutokana na changamoto za wakimbizi na wahamiaji, mambo yanayohitaji wongofu wa kimisionari kwa watoto wote wa Kanisa. Kardinali Marc Ouellet anasema huu ni mchakato unaotafuta wongofu wa kisinodi, ili Kanisa liweze kuwa na mwono mpya katika masuala ya kitaalimungu; kwa kuzingatia mambo msingi, kwa kuthamini wito wa kila mwamini kila mmoja kadiri ya dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa, ili hatimaye, kujenga uelewa wa taalimungu inayosimikwa katika umoja, kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Wongofu wa kimisionari na utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, ni ndoto kubwa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Utafiti huu ni muhimu sana si tu kwa Maaskofu bali kwa watu wote wa Mungu wanaojihusisha na malezi katika ngazi mbalimbali. Maadhimisho ya Kongamano la Kimataifa kwa Ajili ya Wakleri, bado yamesimikwa katika shaka kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Dhana ya Sinodi na Daraja Takatifu ni kati ya tema ambazo zimejadiliwa sana katika Sinodi ya Familia, Vijana pamoja na Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia Oktoba, 2019. Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayotarajiwa kuadhimishwa Mwezi Oktoba 2022 itaongozwa na kauli mbiu “Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, ushiriki na utume” Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika ushuhuda wa maisha na utume wa Kanisa. Kardinali Marc Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu anawaalika watu wote wa Mungu kusali kwa ajili ya kufanikisha kongamano hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu mahalia waangalie changamoto za miito katika Majimbo yao, huku wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake.

Kwa upande wake, Professa Michelina Tenace, Jaalimu wa Taalimungu, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, Roma anakazia kuhusu mahusiano na mafungamano kati ya waamini waliobatizwa na kufanywa kuwa Taifa la Mungu na kushirikishwa kwa namna ya pekee katika huduma ya Kikuhani, ya Kinabii na ya Kifalme ya Kristo Yesu kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu. Utambuzi na uelewa wa Kanisa unapaswa kupyaishwa kwa kusoma alama za nyakati, ili kuendelea kuhamasisha ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha na utume wa Kanisa. Kuhani anapaswa kuyatakatifuza malimwengu kwa zawadi ya Sakramenti za Kanisa. Hili ni Kongamano litakalojadili kwa undani kuhusu Sakramenti ya Ubatizo. Waamini kwa njia ya Ubatizo wanazaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu na hivyo wanashirikishwa maisha ya Kimungu. Taalimungu ya Miito ni tema muhimu sana kwa wakati huu kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu na ujenzi wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili.

Ni wakati muafaka wa kushuhudia utambulisho makini wa Mapadre wa Kanisa kwa njia ya huduma inayosimikwa katika utakatifu wa maisha. Useja na usafi kamili ni mada tete sana katika ulimwengu mamboleo. Kumbe, hapa kuna haja ya Kanisa kujikita katika malezi awali na endelevu kuhusu miito na ushuhuda wa kinabii unaofumbatwa katika uhuru wa watumishi wa Mungu. Taalimungu ya Sakramenti za Kanisa na Liturujia ni mambo muhimu ya kupewa Kipaumbele cha pekee katika malezi ili kuweza kupata “Taalimungu ya Kipadre” ambayo imekomaa na kushiba! Kongamano hili, itakuwa ni fursa ya kuibua changamoto za maisha, wito na utume wa Mapadre; Nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Wakati huo huo, Padre Vincent Siret, Gambera wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Kifaransa mjini Roma, amepembua kuhusu malezi na majiundo ya Majandokasisi mintarafu Fumbo la Utatu Mtakatifu linalojikita katika umoja na huduma. Ni wakati muafaka wa kutafakari taalimungu msingi katika maisha na utume wa Mapadre ndani ya Kanisa. Kongamano hili ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa na sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Taalimungu ya Maisha na Wito wa Kipadre haina budi kupyaishwa kwa kusoma alama za nyakati. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu limeunda Kituo cha Utafiti wa Kiutu na Miito, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuchangia kwa hali na mali katika kufanikisha majukumu ya Kituo hiki kwa anuani ifuatayo: www.communio-vocatio.com.

Tovuti hii ni msaada mkubwa katika kufuatilia yale yanayoendelea kujiri kabla, wakati na baada ya Maadhimisho ya Kongamano la Kimataifa kwa Ajili ya Wakleri. Kati ya mada zitakazopembuliwa ni pamoja na: Mapokeo na Mwelekeo Mpya; Fumbo la Utatu Mtakatifu, Utume wa Kanisa na Sakramenti za Kanisa. Mada nyingine ni Useja na Usafi Kamili, Karama na Tasaufi. Kila siku, itasimamiwa na kuratibiwa na Baraza la Kipapa mintarafu tema husika. Baada ya maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuwatuma washiriki wa Kongamano hili ili kwenda kushuhudia hayo waliyosikia na kuona kwa macho yao wenyewe!

Kongamano Wakleri 2022

 

12 April 2021, 15:36