Tafuta

Vatican News
2021.04.20 Mkuno kwa njia ya Mtanadao kuhusu bioanuwai ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la maendeleo Fungamani ya binadamu 2021.04.20 Mkuno kwa njia ya Mtanadao kuhusu bioanuwai ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la maendeleo Fungamani ya binadamu  

Kard.Turkson:Bioanuwai ni zawadi kutoka kwa Mungu inapaswa kulindwa

Mkutano kuhusu Laudato sì kwa njia ya mtandao umefanyika tarehe 20 Aprili mchana,ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la Maendelo Fungamani ya Binadamu na Tume ya Vatican Covid-19. Wakati wa mkutano huo wamesema kuwa mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko ni muhimu ili kuunda upya mifumo ya ekolojia yenye afya na kulinda bioanuwai.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Kwa mtazamo wa Mkutano ujao kuhusu bioanuwai utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu nchini China na kuelekeza katika mafundisho ya Waraka juu ya utunzaji wa nyumba yetu ya pamoja wa Laudato si', umefanyika tarehe 20 Aprili 2021, mchana  kwa njia ya mtandao. Tukio hilo limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya binadamu na Tume ya Vatican ya  COVID-19, pamoja na kikundi cha Nguvu kazi ya Ekolojia. Waliotoa mada katika mkutano huo ni Kardinali Peter K. A. Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha maendeleo Fungamani ya Binadamu, na  Dk. Jane Goodall , DBE, Mwanzilishi Taasisi ya Jane Goodall na Mjumbe wa Amani wa Umoja wa Mataifa.

Kardinali Turkson katika tafakari ya mkutano huo amekumbusha  hali ya sasa iliyotikiswa na shida, sio tu huduma ya kiaafya, lakini  akasisitiza kuwa janga hilo limeangusha uchumi wa ulimwengu na kuzidisha pengo kati ya matajiri na maskini. Kwa maana hiyo ni muhimu kurekebisha mifano ya maendeleo  ili kuweka maskini kuwa kitovu cha hali halisi ya kutafuta suluhisho la dhati. Vile vile akikumbusha uwiano uliopo amesema janga hili linatuonya kwamba wakati mazingira yanaharibiwa, binadamu pia ni mgonjwa. Kuna uhusiano wa karibu kati ya afya asilia na afya ya ubinadamu. Afya ya ubinadamu, inategemea hali ya asili ya maumbile. Ikiwa maumbile asilia ni mabovu kutokana na uchafuzi wa mazingira au uharibifu uliofanywa na mwanadamu,  vile vile ubinadamu pia unateseka!

Bioanuwai ni kazi ya uumbaji wa Mungu. Katika Biblia inatambuliwa kama sehemu ya utukufu wa Bwana.  Katika Mafundisho jamii ya Kanisa pia inatambuliwa kama kazi endelevu ya uumbaji wa Mungu, na kama zawadi takatifu kutoka kwa mwenyezi Mungu. Kila kiumbe ana thamani ya ndani na tunu msingi. Kila kiumbe, Kardinali Turkson amesisitiza, ni dhihirisho la utukufu wa Mungu. Lakini leo hii  tunashuhudia uharibifu mkubwa wa zawadi za uumbaji. Kila mwaka, tunashuhudia kutoweka kwa maelfu ya spishi na mimea.

Kardinali Turkson pia amejikita kwenye suala la deni ambalo linaendelea kuongezeka. Hilo ndilo ameliita deni ya kiekolojia, kwa sababu gharama ya uharibifu unaosababishwa na unyonyaji wa kibinadamu wa asili, ni kubwa zaidi kuliko faida za kiuchumi zinazotokana nayo. Kwa maana hiyo kardinali akauliza swali:  Je! Tunawezaje, kulipa deni letu ya kiekolojia? Kwa kukabiliwa na swali kama hili muhimu, ni kwamba ubinadamu hauwezi kubaki bila kujali: Ni wajibu wetu kulinda viumbe hai Duniani, Kardinali Turkson amesisitiza.

Kulinda bioanuwai awali ya yote ni juu ya kazi ya kibinadamu. Sisi sote tumeitwa, kuwa na uongofu wa kiekolojia. Hii inahitaji mabadiliko ya mawazo na mtazamo: lazima mtu apite kutoka katika hamu ya kudhibiti na kutawala hadi kufikia kukutana na kazi ya uumbaji, kwa kukaribisha zawadi zake zote. Lazima tupite kutoka katika  mtazamo wa uwindaji hadi kufikia mtazamo wa kutafakari na wa upendo, amesisitiza kwa nguvu  Kardinali Turkson.

Watu asilia ni wasimamzi msingi wa viumbe hai. Kwa maana hiyo lazima tuwaheshimu na kuwalinda watu hawa na mitindo yao ya maisha ikiwa tunataka kuulinda ulimwengu. Kama Familia ya kibinadamu, Kardinali Turkson amebaini, wanaweza kujifunza mengi juu ya utunzaji wa bioanuwai kwa kuzingatia jinsi ndugu zetu wa asilia, wanaona ulimwengu na kuishi katika uhusiano na uumbaji.

Haiwezi mtu hasisikilize kilio cha dunia! Lazima tuchukue hatua kwa pamoja, ili kusiwe na upotezaji wa bioanuwai na kwamba mifumo ya mazingira iliyoharibika irejeshwe. Kwa kuhimimisha: “Tumeitwa kukumbatia mtazamo muhimu wa ekolojia katika  uchumi na sera zilizorekebishwa ili kuheshimu hadhi ya mwanadamu na uadilifu wa kazi ya  uumbaji”amehitimisha  Kardinali Turkson.

21 April 2021, 16:13