Tafuta

Vatican News
Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha "Sacro Cuore, Jimbo Kuu la Milano kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha "Sacro Cuore, Jimbo Kuu la Milano kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. 

Jubilei ya Miaka 100 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha "Sacro Cuore"

Askofu mkuu Mario Delpin wa Jimbo kuu la Milano ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” Jimbo kuu la Milano, kilipoanzishwa. Maadhimisho haya yamekuwa ni fursa ya kufungua Mwaka wa Masomo 2021-2022. Rais Sergio Mattarella wa Italia amewatumia ujumbe wa matashi mema kwa video.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” Jimbo kuu la Milano, kilianzishwa ili kujibu hitaji la mahali pa malezi na majiundo makini ya vijana nchini Italia, changamoto iliyovaliwa njuga na Padre Agostino Gemelli na wasaidizi wake wa karibu akina Armida Barelli na Giuseppe Toniolo. Na matokeo yake katika kipindi cha uhai wake, Chuo hiki kimeendelea kukua na kupanuka na hatimaye, kuwa ni jukwaa la malezi na majiundo ya kielimu kitaifa na kimataifa! Ni kati ya vyuo vikuu vya kikatoliki maarufu sana Barani Ulaya. Kuna wanafunzi 43, 302 wanaopata elimu bora inayokidhi viwango vya soko la ajira Barani Ulaya. Ni Chuo kikuu ambacho kimewekeza sana katika tafiti makini, ili kuendelea kusoma alama za nyakati. Haya ni matokeo ya sadaka kubwa ya akili na ukarimu inayotekelezwa na wadau wa Jumuiya ya Chuo kikuu, bila kusahau kwamba, wanafunzi wana imani na wanathamini sana mchango huu.

Tarehe 13 Aprili 2021, Askofu mkuu Mario Delpin wa Jimbo kuu la Milano ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” Jimbo kuu la Milano, kilipoanzishwa. Maadhimisho haya yamekuwa ni fursa ya kufungua Mwaka wa Masomo 2021-2022. Rais Sergio Mattarella wa Italia amewatumia ujumbe kwa maadhimisho haya. Wanafunzi waliohitimu masomo yao Chuo hapo wametoa shukrani za dhati kwa Chuo kuwawezesha kupata elimu, ujuzi na maarifa. Leo hii wamekuwa ni watu tofauti kabisa. Askofu mkuu Mario Delpin katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa wanafunzi kusoma kwa juhudi, bidii na maarifa. Wanafunzi wajifunze vyema ili kuelewa mambo badala ya kukariri. Waondokane na maamuzi mbele kwa kudhani kwamba, tayari wanajua ili kusoma kwa bidii na kuondokana na uvivu, tayari kushangazwa na maajabu ya Mungu.

Masomo ya Chuo Kikuu yanapania kumwandaa mwanafunzi kufahamu mema na mabaya, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa watu wa Mungu. Ni changamoto ya kujifunza kwa nadharia na vitendo. Wanafunzi wanapaswa kuzama katika undani wa masomo yao, ili kuelewa vyema zaidi, tayari kuwashirikisha wengine mang’amuzi haya. Tasaufi ya wanazuoni ni mchakato unaowahamasisha kuwa na ari na moyo wa kusonga mbele hadi kufikia lengo linalokusudiwa kwa kuonesha moyo wa shukrani, kila mtu kadiri ya historia ya maisha yake. Wanazuoni wanapaswa kuwajibika katika mchakato wa kutekeleza utume wao, ili hatimaye, siku moja waweze kuwa ni mashuhuda wa matendo makuu ya Mungu aliyowatendea katika maisha yao. Wanazuoni wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa: uaminifu na uadilifu; weledi na ubora wenye viwango, ili kupandikiza mbegu ya imani na matumaini kama kielelezo cha utakatifu wa maisha ya kila siku.

Wanafunzi wa Chuo kikuu, wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha, imani, sadaka, huruma, upendo na msamaha wa kweli, kielelezo cha upya wa maisha unaobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka. Askofu mkuu Mario Delpin wa Jimbo kuu la Milano anasema, ameamua kutoa mahubiri mintarafu mazingira waliyomo. Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” inaadhimishwa wakati ambapo dunia imepigishwa magoti kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Huu ni mwaliko wa kuadhimisha Jubilei hii katika hali ya unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani, tayari kumpokea Kristo Yesu, ili aweze kuwa ni mwandani wa maisha, huku wakiendelea kuchota amana na utajiri wa huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 28 Novemba 2019 alizindua Mwaka wa Masomo wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” sanjari na uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 kwa mwaka 2020-2021 na kukazia umuhimu wa Chuo kikuu kujikita katika diplomasia kwa ajili ya ujenzi wa amani duniani. Mama Kanisa anapenda kujielekeza zaidi katika sekta ya elimu ili kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bora, ujuzi na maarifa pamoja na kuhakikisha kwamba, Chuo Kikuu cha Kikatoliki, mara kwa mara kinapima mafanikio, matatizo na changamoto zinazojitokeza. Lengo ni kukiwezesha kuchangia katika mchakato wa maendeleo fungamani, ukuaji wa uchumi, majiundo makini pamoja na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni katika muktadha huu, Chuo Kikuu kinapaswa kujielekeza zaidi katika kutoa nadharia ambayo inamwilishwa katika vitendo. Kwa kutambua changamoto zilizoko mbele yao na hivyo kutafuta nyenzo zitakazosaidia kupambana na matatizo pamoja na changamoto hizi ili hatimaye, suluhu ya kudumu iweze kupatikana kwa njia ya masomo yanayowapatia ujuzi, weledi na maarifa yanayotokana na tafiti makini za kisayansi.

Milano

 

 

 

13 April 2021, 15:44