Tafuta

Vatican News
Dr. Josè Gregorio Hernàndez kutangazwa mwenyeheri tarehe 30 Aprili 2021 huko Venezuela. Chombo cha huduma, haki, amani na upatanisho nchini Venezuela kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Dr. Josè Gregorio Hernàndez kutangazwa mwenyeheri tarehe 30 Aprili 2021 huko Venezuela. Chombo cha huduma, haki, amani na upatanisho nchini Venezuela kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.  (AFP or licensors)

Dr. Josè Gregorio Hernàndez: Chombo: Huduma, Haki na Amani

Ibada ya Misa Takatifu kwa niaba ya Papa Francisko inaongozwa na Askofu mkuu Aldo Giordano, Balozi wa Vatican nchini Venezuela. Hapo awali, Ibada hii ilitarajiwa kuongozwa na Kardinali Pietro Parolin, lakini kutokana na maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 hataweza kuhudhuria kama ilivyo hata kwa Kardinali Marcello Semeralo. UVIKO-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Mtumishi wa Mungu Dr. José Gregorio Hernández anatarajiwa kutangazwa Ijumaa, tarehe 30 Aprili 2021 kuwa Mwenyeher. Ibada ya Misa Takatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko inaongozwa na Askofu mkuu Aldo Giordano, Balozi wa Vatican nchini Venezuela. Hapo awali, Ibada hii ilitarajiwa kuongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican lakini kutokana na maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 hataweza kuhudhuria Ibada hii.  Kardinali Marcello Semeralo, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu alitarajiwa pia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, lakini hata yeye hataweza kuhudhuria. Kardinali Parolin amewahakikishia watu wa Mungu nchini Venezuela kwamba, yuko pamoja nao kiroho, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha tukio hili adhimu katika maisha na utume wa Kanisa nchini Venezuela. Iwe ni fursa ya kupyaisha na kuimarisha imani, matumaini na mapendo miongoni mwa watu wa Mungu nchini Venezuela. Wajizatiti kikamilifu kuiga karama na fadhila za Dr. José Gregorio Hernández katika maisha, wito na utume wake kama mwamini mlei. Wote kwa pamoja wasimame kidete kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zinazoibuka kwa wakati huu, kwa kukazia misingi ya haki, amani, umoja wa kitaifa na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Sala, Tafakari ya kina ya Neno la Mungu, Ushiriki mkamilifu wa maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na Amri za Mungu, vilikuwa ni chemchemi ya utakatifu wa maisha, kielelezo makini cha Msamaria mwema, anayejisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwamba, Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández atakuwa anaadhimishwa na kukumbukwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Oktoba. Hii ni tarehe ambayo imezoeleka kwa watu wa Mungu nchini Venezuela. Baba Mtakatifu ameonesha furaha yake kwa Mama Kanisa kutambua na kuthamini mchango na ushuhuda uliotolewa na Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández katika maisha na utume wake, kiasi cha kupendwa na watu wa Mungu nchini Venezuela. Huyu alikuwa ni mwanasayansi mahiri, aliyebobea katika taaluma yake, kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, lakini zaidi kwa “maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández alisoma, akafaulu masomo yake na kutunukiwa vyeti mbalimbali vya masomo. Hapa ni mahali ambapo alifanyia kazi za tafiti mbalimbali na matokeo yake ni uvumbuzi wa dawa mbalimbali zinazotumiwa na watu wa Mungu nchini Venezuela.

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela kwamba, tukio hili la neema ni ufufuko na upyaisho wa matumaini kwa watu wa Mungu nchini Venezuela. Kardinali Baltazar Porras, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mérida na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Caracas anasema, maadhimisho haya yamekuja kwa wakati muafaka, walimwengu wanapoendelea kushuhudia maafa makubwa yanayotokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Janga hili limeonesha udhaifu wa binadamu na umuhimu wa kushikamana kwa pamoja katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Maadhimisho haya ni fursa ya kumkimbilia Mwenyeheri Dr. José Gregorio Hernández, kwa sala na maombi, ili aweze kuwafariji ndugu zake katika kipindi hiki cha mahangaiko makubwa. Mwenyeheri huyu ni kiungo muhimu sana kwa watu wa Mungu nchini Venezuela. Huu ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu nchini Venezuela kushikamana na kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Utakatifu wa maisha yake, ni tunu ambayo imewavuta watu wengi nchini Venezuela, hususan huduma ya tiba kwa maskini. Ni rejea kwa ajili ya Venezuela kuanza mchakato wa ujenzi wa haki, amani na umoja wa Kitaifa, baada ya kutikiswa sana katika miaka ya hivi karibuni, changamoto na mwaliko wa toba na wongofu wa ndani kwa watu wote wa Mungu nchini Venezuela. Mchakato wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Dr. José Gregorio Hernández kuwa Mwenyeheri uliridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Juni 2020. Mchakato huu umedumu takribani miaka 70 tangu Askofu Lucas Guillermo Castillo alipotia nia hii kunako mwaka 1949. Tarehe 16 Januari 1986, Mtakatifu Yohane Paulo II akaridhia aitwe Mtumishi wa Mungu. Hapo tarehe 30 Aprili 2021 anatangazwa kuwa ni Mwenyeheri na baadaye Mwenyezi Mungu akipenda, Kanisa hatimaye, litamtangaza kuwa Mtakatifu.

Mwenyeheri Venezuela

 

 

29 April 2021, 15:47