Tafuta

Vatican News
Caritas Internationalis linasema, kuna watu milioni 270 wanakabiliwa na baa la njaa sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe, msaada wa dharura unahitajika ili kuokoa maisha ya watu hawa. Caritas Internationalis linasema, kuna watu milioni 270 wanakabiliwa na baa la njaa sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe, msaada wa dharura unahitajika ili kuokoa maisha ya watu hawa.  (AFP or licensors)

Caritas Internationalis: Watu Millioni 270 Wanakabiliwa na Njaa

Barua ya wazi kwa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa na wakuu wa nchi kuhusu hatari ya watu milioni 270 wanaotishiwa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, kuna haja ya kuchukua hatua za dharura, ili kuokoa maisha ya watu ambao kwa sasa wako hatarini. Kuna watu wanaopoteza maisha yao kwa sababu ya baa la njaa na vita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kwa kushirikiana na Mashirika ya Kiraia yameandika barua ya wazi kwa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa na wakuu wa nchi kuhusu hatari ya watu milioni 270 wanaotishiwa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, kuna haja ya kuchukua hatua za dharura, ili kuokoa maisha ya watu ambao kwa sasa wako hatarini. Kuna watu wanaopoteza maisha yao kwa sababu ya baa la njaa huko Yemen, Afghanistan, Ethiopia, Sudan ya Kusini, Burkina Faso, DRC, Venezuela, Honduras, Nigeria, Haiti, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe na Sudan Kongwe. Watu hawa wanateseka kwa baa la njaa na magonjwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, vita, kinzani na mipasuko ya kisiasa, kidini na kijamii. Ni watu wanaokumbana na mifumo mbalimbali ya ubaguzi, kiasi cha kukosekana usawa kwa watu wote.

Umaskini wa hali na kipato, ukosefu wa fursa za ajira pamoja na athari kubwa ambazo zimesababishwa na janga la Virusi vya Ugonjwa wa Korona, UVIKO-19. Lakini wanawake, wazee na watoto ndio waathirika wakubwa zaidi. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la mahitaji ya msaada wa kibinadamu, lakini hitaji hili kubwa linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujipanga vizuri zaidi ili kuokoa maisha ya watu milioni 270 wanaokabiliwa na hatari ya kufa kwa baa la njaa. Huu ni wakati wa kuitikia wito huu kwa vitendo na hivyo kuchangia kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 5.5, ili kusaidia watu zaidi ya milioni 34 ili waweze kujikwamua kutoka katika baa la njaa linalosigina utu, heshima na haki zao msingi. Msaada huu utawawezesha kujiandaa kwa siku za usoni ili kuweza kujizatiti zaidi katika mchakato wa uhakika na usalama wa chakula.

Nchi zote zinapaswa kuchangia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa pia kuhakikisha kwamba, vita, mipasuko na migogoro ya kijamii inasitishwa mara moja ili kutoa nafasi kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwahudumia watu wanaokabiliwa na baa la njaa na utapia mlo wa kutisha kwa sasa. Misaada ya kiutu, lazima iwafikie waathirika wote pasi na vizuizi. Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kwa kushirikiana na Mashirika ya Kiraia yanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza kwa wingi katika mpango mkakati wa mapambano dhidi ya umaskini, njaa na magonjwa. Jumuiya ya Kimataifa iendelee kujielekeza zaidi katika utekelezaji wa sera na mikakati ili kudhibiti athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuwatumbukiza mamilioni ya watu katika umaskini, ujinga na magonjwa. Umoja na mshikamano wa kidugu dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni muhimu sana, ili kuepuka makundi makubwa ya watu kuzikimbia nchi zao kwa kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Jambo la msingi ni kupambana kikamilifu na baa la njaa na umaskini kwa sasa na kwa siku za usoni!

Baa la Njaa Duniani
28 April 2021, 15:51