Tafuta

Tafakari Kipindi cha Kwaresima: Kardinali Raniero Cantalamessa: Kristo Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli, chemchemi ya utakatifu wa maisha na mfano bora wa kuigwa. Tafakari Kipindi cha Kwaresima: Kardinali Raniero Cantalamessa: Kristo Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli, chemchemi ya utakatifu wa maisha na mfano bora wa kuigwa. 

Tafakari Kipindi cha Kwaresima: Yesu Ni Mungu Kweli na Mtu Kweli

Yesu ni mwanadamu aliyekamilika, katika hija ya maisha na utume wake hapa duniani, akajitahidi kumwilisha utakatifu wake hatua kwa hatua katika unyenyekevu. Utakatifu wa Kristo Yesu, ni chemchemi ya utakatifu. Kama walivyosema wakati fulani "Mungu amekufa" hata Leo hii kuna watu wanaofikiri na kutenda kana kwamba “Etsi Christus non daretus” yaani “Kristo Yesu amekufa”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Kipindi cha Kwaresima, kila Ijumaa, kunakuwepo na Tafakari za Kipindi cha Kwaresima. Kauli mbiu inayonogesha tafakari za Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2021 zinazotolewa kwa Baba Mtakatifu Francisko, Makardinali, Maaskofu, wasaidizi wake wa karibu, yaani “Curia Roma” pamoja na wafanyakazi wa Jimbo kuu la Roma ni “Akawaambia, “Nanyi mwaninena kuwa mimi kuwa ni nani? Tafakari hizi zitatolewa na Kardinali Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa. Tafakari ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima ilinogeshwa na kauli mbiu Yesu alianza kuhubiri Galilaya “akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.”  Kardinali Cantalamessa alisema kutubu ni kuamini, kwa kujinyenyekesha kama mtoto mdogo, kwa kuwa na msimamo thabiti katika maisha. Kardinali Raniero Cantalamessa katika Tafakari yake ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima, Ijumaa tarehe 5 Machi 2021 amejikita kufafanua Ubinadamu wa Kristo Yesu aliyekuwa “Mungu kweli na mtu kweli”. Kristo Yesu ni mwanadamu aliyekamilika, katika hija ya maisha na utume wake hapa duniani, akajitahidi kumwilisha utakatifu wake hatua kwa hatua katika unyenyekevu.

Utakatifu wa Kristo Yesu, ni chemchemi ya utakatifu wa wafuasi wake. Katika ulimwengu mamboleo kulifikia kipindi watu wakadiriki kusema “Etsi Deus non daretur” Yaani kwa lugha nyepesi “Mungu amekufa”. Leo hii kuna watu wanaofikiri na kutenda kana kwamba “Etsi Christus non daretus” yaani “Kristo Yesu amekufa”. Mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee ni mwingiliano kati ya wale wanaoamini na wale wasioamini mintarafu haki za kiraia, kanuni za kimaadili na tamaduni kwa kuzingatia yale yaliyotokea baada ya kifo cha Kristo Yesu. Lakini ikumbukwe kwamba, mchango wa Kristo Yesu hauwezi kupimwa kwa majadiliano kati ya imani na falsafa, au na sayansi ili kuhakiki ukweli kuhusu uwepo wa Mungu au majadiliano ya kidini, ili kuangalia umuhimu wa dini katika maisha ya binadamu. Kristo Yesu, Kanisa la Injili yake ni mambo msingi yanayotegemeana na kukamilishana. Fumbo la maisha ya Kanisa linajikita zaidi katika: Kusikiliza mafundisho ya mitume; umoja wa Kanisa, Ekaristi Takatifu na sala. Haya ni mambo msingi yanayowaunganisha waamini na Kristo Yesu.

Mamlaka fundishi ya Kanisa “Magisterium” yanakita mizizi yake kwa Kristo Yesu kama wanavyofafanua Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Ni kwa njia ya Kristo Yesu watu wanaweza kuyafahamu mafundisho yanayotolewa na viongozi wa Kanisa. Ni Mamlaka inayojikita katika shughuli za kichungaji, kanuni maadili na utu wema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa sasa bila kusahau janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Changamoto zote hizi ziwasaidie waamini kumfahamu zaidi Kristo Yesu ili kumtangaza na kumshuhudia mbele za watu. Mtume Paulo anasema “Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo”. Flp. 1:21. “Vivere Christus est”. Kwa njia hii, waamini wanaweza kugundua nafasi na utume wa Kristo Yesu katika ulimwengu mambo leo. Mababa wa Mtaguso wa Chalcedon wa Mwaka 451 walitamka na kufundisha kwamba, Kristo Yesu ni Mungu kweli na mtu kweli, aliyezaliwa bila kuumbwa, wenye umungu mmoja sawa na Baba, katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Kristo Yesu anazo asili mbili, yaani asili ya Kimungu na Kibinadamu.

Ikumbukwe kwamba, Kanisa linaungama Mungu mmoja katika Nafsi tatu. Kila moja ya Nafsi hizo tatu ni ukweli wa uwamo na uwapo wa asili ya Kimungu. Kwa njia ya Mafundisho tanzu, Mama Kanisa anapenda kuimarisha sheria na kanuni msingi ili kuwawezesha waamini kutambua kwamba, Kristo Yesu ni Mungu kweli na mtu kweli. Kumbe, waamini wanapaswa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu mintarafu Mapokeo ya Kanisa, huku wakitumia “miwani” ya Mama Kanisa. Kristo Yesu ni mtu mkamilifu kabisa na wala hakuna mtu aliyekuwa na wasiwasi juu ya ubinadamu wake, isipokuwa, watu walipenda kujikita zaidi katika utakatifu wake kuliko ukweli wote wa maisha yake. Wakati wa Mtaguso wa Chalcedon, mambo yalikuwa shwari, lakini yalianza kubadilika kunako karne ya saba na huo ukawa ni mwanzo wa uzuo wa imani. Badala ya kuangalia Utakatifu wake, “wakaamua kupindua meza” na kuanza kuangalia ubinadamu wake.

Agano Jipya halichambui hata kidogo kuhusu ukweli wa Kristo kama binadamu, bali kama mtu mpya na Adamu wa mwisho “Eschatos” ni roho yenye kuhisha. Kristo Yesu ni chemchemi ya uzima mpya, changamoto kwa waamini kuvaa utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli. Kristo Yesu ni Mtakatifu wa Mungu. Utakatifu wa Kristo Yesu ulimwilishwa katika uhalisia wa maisha yake na muhtasari wake umefumbatwa katika Heri za Mlimani, moja ya mafundisho yake mazito! Kristo Yesu aliwataka wafuasi wake kujifunza kutoka kwake kwani Yeye ni mpole na mnyenyekvu wa moyo. Aliwataka kusamehe na kusahau kwa sababu hawajui watendalo. Utakatifu wa Kristo Yesu unajionesha katika maisha na matendo yake yote na wala hakutenda dhambi hata kidogo. Fumbo la Ufufuko wa wafu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ukweli huu.

Kardinali Raniero Cantalamessa anasema, Wakristo wanachota utakatifu wao kutoka kwa Kristo Yesu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanazungumzia wito wa watu wote kuwa watakatifu. “Wafuasi wa Kristo walioitwa na Mungu siyo kadiri ya matendo yao, bali kadiri ya azimio la neema yake na kuhesabiwa haki katika Bwana Yesu, katika Ubatizo wa imani walifanywa kweli watoto wa Mungu na washiriki wa tabia ya Mungu, na hivyo watakatifu halisi” LG. 40. Utakatifu wa Wakristo kabla ya kuwa ni dhamana, ikumbukwe kwamba, ni zawadi ya upendo inayofumbatwa katika imani. Hii ni changamoto kwa waamini kuuvua utu wao wa kale na kuanza kutembea katika mwanga mpya wa imani. Wawe ni watu wenye huruma na mapendo; watambue udhaifu na dhambi zao, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, ili aweze kuwahesabia haki.

Wakristo wanapaswa kumuiga Yesu katika maisha yao, kwa kutambua kwamba, utakatifu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe, wanapaswa kuishi kama watakatifu. “Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.” Kol. 3:12. Mtakatifu Paulo anakaza kusema, “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho. Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana.” Gal. 5:22-26. Wakristo wanahimizwa kuchota amana na utajiri wa imani na kuumwilisha katika fadhila, ili kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao kama alivyofundisha Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu na kwamba, Roho Mtakatifu yupo tayari kuwasaidia na kuwakumbusha yake waliyoyasahau!

Tafakari Kwaresima

 

05 March 2021, 17:31