Tafuta

Familia ya Mungu nchini Tanzania inahamasishwa kumkumbuka na kumwombea Hayati Dr. John Pombe Magufuli, ili Mwenyezi Mungu amtakase na kumkirimia maisha na uzima wa milele! Familia ya Mungu nchini Tanzania inahamasishwa kumkumbuka na kumwombea Hayati Dr. John Pombe Magufuli, ili Mwenyezi Mungu amtakase na kumkirimia maisha na uzima wa milele! 

Safari ya Maisha ya Kiroho ya Dr. John P. Magufuli wa Tanzania

Askofu mkuu Protase Rugambwa, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Hayati Dr. John Pombe Magufuli wa Tanzania. Baada ya Ibada ya Misa, ilifuatia dua iliyoongozwa na Bwana Abdul Hamid Ahmed na mwishoni, Balozi George Kahema Madafa alitoa neno la shukrani kwa wote waliohudhuria licha ya changamoto kubwa zinazotokana na janga la Virusi vya Korona.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S – Vatican.

Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Jumamosi tarehe 20 Machi 2021, kwa kushirikiana na Ubalozi na wawakilishi wa watanzania wanaoishi nchini Italia ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Hayati Dr. John Pombe Magufuli wa Tanzania aliyefariki dunia hapo tarehe 17 Machi 2021. Baada ya Ibada ya Misa, ilifuatia dua iliyoongozwa na Bwana Abdul Hamid Ahmed na mwishoni, Balozi George Kahema Madafa alitoa neno la shukrani kwa wote waliohudhuria licha ya changamoto kubwa zinazotokana na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Taarifa kutoka katika familia ya Hayati Dr. John Pombe Magufuli, aliyekuwa Rais wa awamu ya tano nchini Tanzania aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021, akiwa anapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Emilio Mzena inasema kwamba, Dr. Magufuli alijiandaa kikamilifu kwa safari yake ya kiroho. Itakumbukwa kwamba, Emilio Mzena aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya TISS kati ya Mwaka 1961 hadi mwaka 1975. Kwa Mpako Mtakatifu wa wagonjwa na sala za makuhani, Kanisa lote huwakabidhi wagonjwa kwa Bwana aliyeteswa na kutukuzwa ili awainue na kuwaokoa. Na kwa hakika lawahimiza wajiunge kwa hiari na Mateso na Kifo cha Kristo Yesu ili kutoa mchango wao kwa manufaa ya Taifa la Mungu. Akiwa katika hatari ya kifo, Dr. John Pombe Magufuli alijiandaa kiroho kwa kupata Mpako wa wagonjwa unaowajaza waamini nguvu ya Roho Mtakatifu. Huwaondoa katika enzi ya dhambi na kuwaweka huru. Kwa wema wake usiokuwa na mipaka, Mwenyezi Mungu huwakirimia pia nafuu katika mateso yao na kuwajalia neema. Msemaji wa familia ya Dr. John Pombe Magufuli aliwaambia waombolezaji kwamba, Rais Magufuli kabla ya kifo chake alibahatika kupata huduma ya maisha ya kiroho, iliyomwongezea amani na utulivu wa ndani na hivyo kujiandaa kupokea kifo chema!

Familia ya Mungu Parokia ya Mtakatifu Petro Jimbo kuu la Dar es Salaam, ilipata nafasi ya kumwombea na kumuaga mwamini mwenzao, waliyeshirikiana katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Hapa pakawa ni mahali pa Kanisa kutoa katekesi ya maana ya kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu kadiri ya Mafundisho ya Kanisa Katoliki. Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi katika Ibada ya Misa takatifu kwenye Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam, tarehe 20 Machi 2021 aliwaalika watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Dar es Salaam, kuupokea msiba huu mzito kwa imani na matumaini kwa Kristo Yesu. Hayati Dr. John Pombe Magufuli katika uhai wake, alimwamini Mwenyezi Mungu akamfuasa, akamshuhudia kwa vitendo na kumtumikia. Roho za wenye haki ziko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Mtu mwenye haki, yuko tayari kumpatia Mungu masitahiki yake kwa: kumwamini, kumwabudu na kumtumikia kwa imani. Mtu mwenye haki anatoa stahiki kwa jirani zake kwa: kuwapenda, kuwahurumia, kuwasaidia na kushikamana nao. Katika nafsi ya mtu mwenye haki, hujitunza, hujiheshimu na kuwajibika kikamilifu.

Ni katika muktadha huu Hayati Dr. John Pombe Magufuli, mtu wa haki anastahili kukumbukwa na kuombewa, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, msamaha na mapendo, aweze kumsamehe dhambi na mapungufu yake ya kibinadamu, apende kuyaangalia majitoleo yake na hatimaye, amkirimie maisha na uzima wa milele. Dr. John Pombe Magufuli aliunganishwa na kuzamishwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Akawa ndugu yake Kristo na kufanyika kuwa Hekalu la Roho Mtakatifu. Mama Kanisa anamwombea ili Kristo Mshindi, aweze kumshirikisha katika ushindi wake, kwa kumfufua siku ya mwisho na hatimaye, kumkirimia maisha na uzima wa milele pamoja na watakatifu wake mbinguni! Mama Kanisa katika huruma na upendo wake kwa ajili ya watoto wake waliotangulia katika usingizi wa amani wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na uzima wa milele, anawashukuru, anawakumbuka na kuwaombea.

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika mahubiri yake, amegusia kuhusu mahusiano na mafungamano kati ya mwamini na Mwenyezi Mungu na kati ya mwamini na jirani zake. Kila mtu ni zawadi ya Mungu inayopaswa kupokelewa kwa moyo wa shukrani. Kuwaombea marehemu ni wajibu kwa waamini wote. Askofu mkuu ametumia fursa hii kutoa pole kwa watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Anawalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania bila kumsamahu Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu wa Vikosi vya ulinzi na usalama. Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Protase Rugambwa, amewataka waamini kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano yao na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao kwa sababu uwepo wa kila mmoja wao ni kwa kadiri ya mapenzi, huruma, uwezo na utashi wa Mwenyezi Mungu. Ni huyu Mungu mwingi wa huruma na mapendo, atakayempokea mja wake katika makao ya uzima wa milele baada ya kumaliza safari ya maisha yake hapa duniani, na “kukunja kilago” tayari kukutana na Mwenyezi Mungu Hakimu mwenye haki.

Watu wa Mungu nchini Tanzania wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Dr. John Pombe Magufuli aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Waamini wanamwombea Dr. Magufuli ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, rehema na mapendo aweze kumtakasa na kumsamehe dhambi zake, ili hatimaye, aweze kumpokea kwenye maisha ya uzima wa milele, tuzo isiyokuwa na mwisho. Hayati Dr. John Pombe Magufuli alikuwa ni sehemu ya wabatizwa na watoto wateule wa Mungu. Kumbe, kama waamini wanalo jukumu la kumkumbuka na kumwombea katika kifungo hiki cha Sakramenti ya Ubatizo. Kwa sababu katika maisha yake, alimkiri na kumshuhudia Mwenyezi Mungu kwa maneno na matendo yake adili. Kwa wema na majitoleo yake kwa familia ya Mungu nchini Tanzania anastahili tuzo la maisha ya uzima wa milele. Ikumbukwe kwamba, hii ni tuzo inayotolewa kwa watoto wapendwa wa Mungu waliojitahidi katika safari ya maisha yao hapa ulimwenguni kutambua na kutekeleza mapenzi ya Mungu. Kama binadamu, wanahimizwa kumkumbuka na kumwombea ili Mwenyezi Mungu apende kumsafisha na kumtakasa pale aliposhindwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake na pale aliposhindwa kutokana na udhaifu wa kibinadamu kuonesha upendo kwa jirani zake.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema waendelee kumwombea Hayati Dr. John Pombe Magufuli, ili Mwenyezi Mungu kwa huruma yake isiyokuwa na kikomo, apende kumsafisha, kumtakasa na kumsamehe dhambi zake, ili hatimaye, aweze kumpokea kwenye Ufalme wake wa milele, akiwa safi na “mweupe pe kama tui la nazi”. Askofu mkuu Protase Rugambwa anakaza kusema, watanzania wanapoendelea kutafakuri mema na mazuri aliyotenda Hayati Dr. John Pombe Magufuli, kiasi cha kukirimiwa wingi wa neema na baraka, iwe ni fursa pia ya kuchunguza dhamiri, kila mtu kadiri ya nafasi yake. Lengo ni kujiandaa kwa ajili ya kifo chema. Huu ni muda wa kumuezi Dr. Magufuli si kwa maneno matupu! Bali kuendeleza kwa ari na moyo mkuu yale yote mema na mazuri aliyotenda Dr. Magufuli kama Rais wa awamu ya tano, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi: kiroho na kimwili. Hii ni fursa makini ya kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wote watakaoteuliwa kumsaidia kuwaongoza watanzania wanapoanza kuandika ukurasa mpya wa historia ya Tanzania. Wananchi wanahimizwa kutoa ushirikiano wa dhati kwa Rais na viongozi wenzake ili kuliendeleza Taifa la Tanzania liweze kudumu katika amani, kwa kukuza na kudumisha misingi ya haki, ustawi na maendeleo ya watanzania: kiroho na kimwili, ili Tanzania iweze kuwa ni nchi ya furaha, amani na mwanga wa matumaini kwa watu wote. Kila mtu ajitahidi kutenda mema yanayompendeza Mungu na jirani!

Hayati Dr. John Pombe Magufuli alikwisha waonya watanzania kamwe wasibaguane kutokana na makabila yao, itikadi zao za kisiasa wala imani zao. Wote wajisikie kuwa ni watanzania na kwamba, tofauti zao msingi ni utajiri na amana ya watanzania wote. Ndiyo maana Dr. Magufuli hakusita kuchangisha fedha kutoka kwa waamini wa dini mbalimbali ili kuboresha nyumba za Ibada hasa kuzunguka Ikulu ya Chamwino. Ni kiongozi aliyeamini kuhusu majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafungamano ya watanzania wote. Ni katika muktadha huu, Bwana Abdul Hamid Ahmed, mtanzania, mwamini wa dini ya Kiislam katika dua yake, amemwomba Mwenyezi Mungu amweke mahali stahiki Dr. Magufuli kutokana na mema yote aliyotenda hapa duniani. Pale alipoteleza kama binadamu, apate msamaha.

Wakati huo huo, Jumuiya za Watawa wanaoishi na kufanya utume wao nchini Tanzania hivi karibuni wameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, wakimkumbuka na kumwombea Hayati Dr. John Pombe Magufuli pamoja na kumtakia heri na baraka Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi mkuu wa Vikosi vya ulinzi na usalama. Watawa wamemwomba Mwenyezi Mungu awafriji na kuwadumisha watanzania katika: imani, amani, upendo, mshikamano ari na moyo wa uzalendo. Masista Wakarmeli Wamisionari wa Theresia wa Mtoto Yesu wanaendelea na sala maalum kwa ajili ya kuiombea nchi ya Tanzania. Katika salam zake za rambirambi Sr. Donatella Capello amewasihi watanzania kuendelea kushikamana kwa dhati pamoja na kuendelea kujifunza mpango wa Mungu katika maisha yao kama Taifa!

Ubalozi wa Tanzania
22 March 2021, 16:17