Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Machi 2021 amekutana na kuzungumza na Rais Marcelo Rebelo de Sousa, Rais wa Ureno. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Machi 2021 amekutana na kuzungumza na Rais Marcelo Rebelo de Sousa, Rais wa Ureno. 

Papa Francisko Akutana na Rais De Sousa wa Ureno mjini Vatican.

Hii ni mara ya pili Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuchaguliwa tena kuingoza nchi ya Ureno. Viongozi hawa wawili kimsingi, wameridhishwa na mahusiano ya kidiplomasia yaliyopo kati ya nchi mbili sanjari na mchango wa Mama Kanisa katika ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini Ureno. Vijana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 12 Machi 2021 amekutana na kuzungumza na Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno, ambaye baadaye alikutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Hii ni mara ya pili Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu baada ya kuchaguliwa tena kuingoza nchi ya Ureno. Viongozi hawa wameridhishwa na mahusiano ya kidiplomasia yaliyopo kati ya nchi mbili sanjari na mchango wa Mama Kanisa katika ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini Ureno.

Kwa namna ya pekee, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kanisa nchini Ureno limeendelea kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai, amani na utulivu miongoni mwa watu wa Mungu. Kwa sasa Ureno ndiye Rais wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, wamejielekeza zaidi katika masuala ya Kimataifa na Kikanda kwa kuonesha umuhimu wa kushirikiana na kushikamana kama sehemu ya mkakati wa kupambana na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19 Kimataifa. Wamegusia umuhimu wa kulinda na kudumisha amani duniani pamoja na masuala ya mafungamano ya Kimataifa.

Itakumbukwa kwamba, kwa mara ya kwanza Rais De Sousa alifanya ziara ya kikazi mjini Vatican tarehe 17 Machi 2016 tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Rais wa Ureno. Alioneshwa kufurahishwa na mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Ureno sanjari na mchango wa Kanisa katika, mafao, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ureno, hususan katika masuala ya kijamii, maisha, utu, heshima ya binadamu na tunu msingi za maisha ya kifamilia. Baba Mtakatifu na mgeni wake katika mazungumzo hayo, waligusia pia masuala ya kimataifa na kikanda, hususan hali tete huko Ukanda wa Bahari ya Mediterannia na hali ya Bara la Ulaya katika ujumla wake. Changamoto ya wahamiaji na wakimbizi ni kati ya mambo ya kimataifa yaliyopewa uzito wa pekee wakati wa mazungumzo hayo kutokana na hali halisi ilivyokuwa kwa wakati ule!

12 March 2021, 15:25