Tafuta

Vatican News
Kardinali Pietro Parolin ametoa tamko kuhusu hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq: Ukaribu wa Baba Mtakatifu; Ujenzi wa Iraq mpya na Majadiliano ya Kidini katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Kardinali Pietro Parolin ametoa tamko kuhusu hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq: Ukaribu wa Baba Mtakatifu; Ujenzi wa Iraq mpya na Majadiliano ya Kidini katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Tamko la Vatican!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, hija hii ya kitume inafumbata mambo makuu matatu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Wakatoliki na Wakristo wote nchini Iraq, kuhamasisha ujenzi wa Iraq katika haki na usawa na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini ili kudumisha udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia tarehe 5 hadi 8 Machi 2021 inanogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, hija hii ya kitume inafumbata mambo makuu matatu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa Wakristo nchini Iraq, kuhamasisha ujenzi wa Iraq mpya katika haki na usawa na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini ili kudumisha udugu wa kibinadamu.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican akitoa Tamko Rasmi la Vatican kuhusu hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, anasema Baba Mtakatifu anakwenda nchini Iraq kuonesha uwepo wake wa karibu kwa Wakatoliki pamoja na Wakristo wote katika ujumla wao. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, Wakristo katika ujumla wao wamateseka sana. Wengi wao wamepoteza maisha na wengine kulazimika kuikimbia nchi yao, ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Ni katika muktadha huu, Iraq inahitaji uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili, aweze kuwatia shime katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu hata katika hali na mazingira magumu kama haya.

Pili, Hija hii ya Kitume inalenga kuragibisha mchakato wa ujenzi wa wa Iraq mpya. Baba Mtakatifu Francisko anataka kuwahamasisha watu wa Mungu nchini Iraq kusimama kidete dhidi ya rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma. Wawe tayari kupinga mifumo yote ya ubaguzi, ili kila mwananchi aweze kuwajibika barabara katika ujenzi wa nchi yake; kwa kuwa na haki na nyajibu sawa. Tatu, hija hii inapania pamoja na mambo mengine, kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, umoja, ushirikiano na maelewano ya kidugu. Baba Mtakatifu anataka kuwahamasisha Waislam na Wakristo kuimarisha udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Tamko Hija ya Papa
02 March 2021, 16:07