Tafuta

Vatican News
Kardinali Pietro Parolin anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq inapania kuonesha uwepo wake wa karibu kwa Wakristo; Isaidie ujenzi wa Iraq mpya pamoja na kukuza majadiliano ya kidini na kiekumene. Kardinali Pietro Parolin anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq inapania kuonesha uwepo wake wa karibu kwa Wakristo; Isaidie ujenzi wa Iraq mpya pamoja na kukuza majadiliano ya kidini na kiekumene. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Umuhimu Wake!

Kardinali Pietro Parolin katika mahojiano maalum na Vatican News anaelezea umuhimu wa hija hii ya kitume katika maisha na utume wa Kanisa; umoja na mshikimanao wa watu wa Mungu nchini Iraq; Umuhimu wa uekumene wa damu sanjari na majadiliano ya kidini, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini na upendo wa dhati kwa watu waliokata tamaa ya maisha! Amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 8 Machi 2021 atakuwa anafanya hija ya kitume nchini Iraq. Hija inapania kuonesha uwepo wake wa karibu kwa Wakristo; kusaidia kuragibisha mchakato wa ujenzi wa Iraq mpya pamoja na kukuza majadiliano ya kidini na uelewano kati ya Waislam na Wakristo ili kujenga udugu wa kibinadamu unaojipambanua kwa kusimama kidete kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Vatican News anaelezea umuhimu wa hija hii ya kitume katika maisha na utume wa Kanisa; umoja na mshikimanao wa watu wa Mungu nchini Iraq; Umuhimu wa uekumene wa damu sanjari na majadiliano ya kidini, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa watu waliokata tamaa ya maisha!

Familia ya Mungu nchini Iraq iko tayari kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko, ili aweze kuwafariji. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni wananchi wa Iraq wameteseka kutoka na madhulumu, nyanyaso, vita na mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa Dola ya Kiislam “Islamic State, IS”. Kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha na utume wa Kanisa, Khalifa wa Mtakatifu Petro anatembelea Iraq, mahali alipozaliwa Ibrahimu, Baba wa imani. Iraq ni nchi ambayo ina Wakristo wa zamani sana, lakini hata leo hii bado makovu ya vita, dhuluma na nyanyaso yanaendelea kuonekana. Ni madonda yanayotokana na mashambulizi na vitendo vya kigaidi, umaskini pamoja na janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kumbe, kuna haja kwa watu wa Mungu nchini Iraq kushirikiana na kushikamana katika mchakato wa ujenzi wa Iraq mpya, kwa kuganga na kuponya madonda ya zamani! Hii ni hija ya kwanza kutekelezwa na Baba Mtakatifu tangu kuzuka kwa maambukizi makubwa ya Virusi vya Korona, UVIKO-19. Baba Mtakatifu anaanza hija hizi kwa kutembelea Iraq, ili kuonesha uwepo wake wa karibu, ili kusaidia mchakato wa kuragibisha ujenzi wa Iraq mpya, kwanza kwa kuganga na kuponya madonda ya zamani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Uso wa huruma na upendo wa Mungu umefunuliwa kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, amewafunulia walimwengu kwamba, wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu unafumbatwa katika: upendo, ukarimu, utu na heshima ya binadamu; utu ambao watu wote wanashirikishana licha ya tofauti zao za kikabila, lugha na tamaduni, lakini wote wanapaswa kujisikia kwamba, ni sehemu ya udugu wa binadamu! Ni kutokana na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kunako Desemba 2018 alifanya hija ya kichungaji yuko nchini Iraq kama kielelezo cha mshikamano wa umoja na udugu wa watoto wa Mungu, hasa katika eneo hili ambalo limegeuka kuwa ni uwanja wa vita. Kardinali Parolin katika mahojiano haya anaikumbuka sana ile hija, iliyomwezesha kukutana na watu wa Mungu wakati wa Sherehe ya Noeli ya Mwaka 2018. Aliwakumbusha watu wa Munngu nchini Iraq kwamba, licha ya tofauti zao msingi, lakini wote ni ndugu wamoja! Ni watoto wa Ibrahamu, Baba wa imani.

Ikumbukwe kwamba, Ibrahimu ni Baba wa Wakristo na Waislam pia! Kumbe, waamini wote hawa wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa mwanga mpya katika mchakato wa ujenzi wa Iraq mpya. Hii ni hija ya kitume ya siku nne zenye uzito wa pekee sana. Baba Mtakatifu atakutana na watu wa Mungu nchini Iraq, atatembelea maeneo ya dhuluma na nyanyaso za kidini, atashiriki katika majadiliano ya kidini, ili kuwahamasisha waamini wa dini mbalimbali nchini Iraq, kushikamana katika ujenzi wa nchi yao. Ni wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini na ujasiri, ili kujenga Iraq mpya! Hii ni fursa ya kukutana na kuzungumza mubashara na Ayatollah Ali Sistani ambaye ni kiongozi mkuu wa kiroho na kisiasa nchini Iraq anayekazia sana maridhiano, amani na utulivu. Wachunguzi wa mambo wanasema, ni fursa ya kumwilisha kwa vitendo Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii”.

Malengo ya Waraka wa Kitume, "Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, anasema Baba Mtakatifu Francisko, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq inapania kupandikiza mbegu ya Injili ya matumaini. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya Wakristo milioni moja wamekimbia nchini Iraq ili kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi ughaibuni. Baba Mtakatifu anataka kuwatia shime Wakristo nchini Iraq kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo katika uhalisia wa maisha yao. Watambue kwamba, huu ni wito wao mahususi huko Mashariki ya Kati. Huu ni mwaliko wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Matumaini pamoja na kubaki katika nchi yao wenyewe, ili kuendelea kuwa mashuhuda wa Ukristo huko Mashariki ya Kati.

Kwa upande wa Serikali ya Iraq, inaona kwamba, hii ni Hija inayotangaza na kushuhudia Injili ya amani, maridhiano na utulivu baada ya miaka mingi ya vita, kinzani na vurugu mbalimbali. Hii ni changamoto kubwa kwa watu wote wa Mungu nchini Iraq kujenga, kuimarisha na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujinyenyekesha mbele ya Mungu na kuzama zaidi katika toba, wongofu wa ndani, msamaha na upatanisho wa kweli. Ni changamoto ya kufyekelea mbali ubaguzi, rushwa na ufisadi wa mali ya umma; ukosefu wa haki na usawa; ili kukazia utawala wa sheria, haki na wajibu kwa raia wote, ili kwa njia ya umoja wa kitaifa, watu wote waweze kushiriki katika ujenzi wa nchi yao. Huu ndio msingi wa ujenzi bora wa Iraq mpya! Ni sala na matumaini ya Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwamba, hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq itasaidia kupyaisha maisha ya kiroho na kimwili miongoni mwa watu wa Mungu nchini Iraq. Matunda ya hija hii ya kitume, yasambae na kuenea Ukanda wa Mashariki ya Kati, kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama unavyonogeshwa na kauli mbiu ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq. “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8.

Kardinali Parolin Iraq

 

02 March 2021, 15:18