Tafuta

Rais Barham Ahmed Salih Qassim wa Iraq katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko amempongeza kwa jitihada zake katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene. Rais Barham Ahmed Salih Qassim wa Iraq katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko amempongeza kwa jitihada zake katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Iraq: Hotuba ya Rais wa Iraq

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq imekuwa na mwelekeo wa kihistoria, kidini na kiutu, lakini zaidi ni ushuhuda unaoonesha na kudhihirisha mahangaiko ya Papa kwa watu wa Mungu nchini Iraq. Ni watu ambao wamekumbana na majanga kutokana na sababu mbalimbali, lakini wako tayari kulinda na kutetea amana na utajiri wa imani, tamaduni na mapokeo yao.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais Barham Ahmed Salih Qassim wa Iraq katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, Ijumaa tarehe 5 Machi 2021, ametumia fursa hii, kutangaza amana na utajiri wa Iraq unaobubujika kutoka katika historia ya ukombozi. Amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kujipambanua katika mchakato wa ujenzi wa amani, haki jamii pamoja na mapambano dhidi ya umaskini sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu amejielekeza zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu kwa ajili ya kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq imekuwa na mwelekeo wa kihistoria, kidini na kiutu, lakini zaidi ni ushuhuda unaoonesha na kudhihirisha mahangaiko ya Baba Mtakatifu kwa watu wa Mungu nchini Iraq. Ni watu ambao wamekumbana na majanga pamoja na maafa kutokana na sababu mbalimbali, lakini wako tayari kulinda na kutetea amana na utajiri wa imani, tamaduni na mapokeo yao.

Kwa sasa wanataka kujitahidi kuanza mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu kwa kujikita katika: upendo na udugu wa kibinadamu. Tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni ni amana na urithi mkubwa wanaopaswa kuachiwa vijana wa kizazi kipya. Vita, mashambulizi na vitendo vya kigaidi ni mambo ambayo yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao sanjari na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Katika nyanyaso na mateso makubwa, wakristo nchini Iraq wameathirika zaidi. Huu ni wakati wa kukuza na kudumisha amani, usalama, uhuru na utawala wa sheria. Ni muda muafaka wa kuganga na kuponya majeraha ya vita, dhuluma na mashambulizi ya kigaidi, kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na ujenzi wa uchumi shirikishi pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wakristo wanayo haki ya kuendelea kuishi huko Mashariki ya Kati.

Huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum ni changamoto kubwa kwa Serikali ya Iraq. Janga la Virusi vya Korona, UVIKO-19, linaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kumbe, kuna haja ya kuunganisha nguvu kwa ajili ya kulinda na kudumisha huduma bora zaidi kwa ajili ya maisha ya mwanadamu. Ni wakati muafaka wa kujizatiti katika mchakato wa upendo, amani, utulivu, ukarimu, umoja na ushirikiano wa Kimataifa. Misimamo mikali ya kidini pamoja na vitendo vya kigaidi ni mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni matumaini ya Rais Barham Ahmed Salih Qassim wa Iraq kwamba, Vatican na Iraq zitaendelea kushirikiana katika mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kukuza historia yao ya pamoja. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq ni sehemu ya dawa ya kuganga na kuponya madonda ya vita, chuki na uhasama kati ya watu wa familia ya Mungu nchini Iraq.

Rais wa Iraq

 

05 March 2021, 16:36