Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Sr. Nathalie Becquart kutoka Ufaransa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu. Mwanamke wa kwanza kuwahi kushika wadhifa huu ndani ya Kanisa Katoliki. Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Sr. Nathalie Becquart kutoka Ufaransa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu. Mwanamke wa kwanza kuwahi kushika wadhifa huu ndani ya Kanisa Katoliki. 

Sr. Nathalie Becquart: Katibu Mkuu Msaidizi Sinodi za Maaskofu

Sr. Nathalie Becquart alizaliwa kunako mwaka 1969 huko Fontainebleau, nchini Ufaransa. Kati ya Mwaka 1989 hadi 1992 alikuwa masomoni ambako alijipatia Shahada ya Uzamili katika Ujasiriamali. Mwaka 1991-1992 akajipatia stashahada ya falsafa. Mwaka 1995 akajiunga na Shirika la Tasaufi ya Kiinyasiani: “Xavière, Missionnaires du Christ Jésus”. Ni "Mwanamke wa shoka".

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Februari 2021 amemteuwa Mheshimiwa sana Sr. Nathalie Becquart, kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu.  Sr. Nathalie Becquart amewahi kuwa Mkurugenzi mtendaji wa Idara ya Uinjilishaji, Vijana na Miito, Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa. Itakumbukwa kwamba, Sr. Nathalie Becquart alizaliwa kunako mwaka 1969 huko Fontainebleau, nchini Ufaransa. Kati ya Mwaka 1989 hadi 1992 alikuwa masomoni ambako alijipatia Shahada ya Uzamili katika Ujasiriamali. Mwaka 1991-1992 akajipatia stashahada ya falsafa. Mwaka 1995 akajiunga na Shirika la Tasaufi ya Kiinyasiani: “Xavière, Missionnaires du Christ Jésus”. Kati ya mwaka 2002 hadi mwaka 2006 akajiendeleza zaidi katika masomo ya Falsafa na kujipatia Shahada ya kwanza katika Falsafa. Baada ya malezi na majiundo yake ya kitawa, katika Shirika la “Xavière”, mwezi Septemba 2005 akaweka nadhiri zake za daima. Katika maisha na utume wake kama mtawa amekuwa akijihusisha na maongozi ya maisha ya kiroho, utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya, Uinjilishaji miongoni mwa vijana.

Kati ya mwaka 2012 hadi mwaka 2018 aliteuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kuwa Katibu mtendaji wa Idara ya Uinjilishaji na Miito. Kati ya mwaka 2015 hadi mwaka 2018 aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais Huduma ya Miito, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, linayounganisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki 33 kutoka Barani Ulaya. Sr. Nathalie Becquart amekuwa ni kati ya wajumbe walioshiriki katika maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya XV ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyoadhimishwa Mwezi Oktoba, 2018 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Mwaka 2019 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni mjumbe mshauri wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Ni Mtawa aliyebahatika kuwa na karama na mapaji mbalimbali ambayo kwa sasa anaweza kuyatumia kikamilifu zaidi kwa ajili ya Sinodi za Maaskofu. Ni mtaalamu aliyebobea katika masuala ya vijana na miito, maisha ya kitawa; utume na maisha ya Kanisa; Sinodi na dhana ya Sinodi; Utamadunisho, mawasiliano, tasaufi pamoja na uratibu wa miradi mbalimbali!

Sr. Nathalie Becquart katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, kwa hakika ameshangazwa sana na uteuzi wa Baba Mtakatifu Francisko kwani hakuwahi hata siku moja, kuwaza kuhusu fursa kama hii ndani ya Kanisa. Hii ni changamoto ya kuendelea kukuza ule wito wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yake. Haya ni mang’amuzi yanayopata chimbuko lake kutoka katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa na sasa, uteuzi huu, ni fursa ya kuendeleza mapaji ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu. Uteuzi huu ni kielelezo cha zawadi ya Mungu katika maisha yake, kinachompatia fursa ya kujiunga na kikosi kazi cha Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu pamoja na Askofu mteule Luis Marín de San Martín, O.S.A. Katibu mkuu msaidizi ambaye wameteuliwa wote siku moja na Baba Mtakatifu Francisko.

Kimsingi anasema Sr. Nathalie Becquart mazingira ya Sekretarieti ya Sinodi si mapya sana kwake, kwani tayari alikuwa ni mjumbe mshauri wa Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu. Hiki ni kielelezo maalum cha imani na matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwa wanawake, ili kuwashirikisha katika mchakato mzima wa kushiriki kutoa mawazo, maamuzi na utekelezaji wake. Uteuzi huu ni kwa ajili ya huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ikumbukwe kwamba, pia kuna wanawake ambao tayari wameteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Makatibu wakuu wasaidizi kwenye Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha pamoja na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume.

Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yamedadavuliwa kwa kina na mapana katika Katiba ya Kitume ya Papa Francisko “Episcopalis Communio” yaani “Kuhusu Sinodi za Maaskofu” iliyochapishwa kunako mwezi Septemba 2018. Hiki ni chombo cha uinjilishaji kinachopania kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari dhamana na wajibu wa Kanisa. Maaskofu wanahimizwa kusikiliza na kujibu kilio cha watu wa Mungu “Sensum fidei” katika maisha na utume wa Kanisa! Sr. Nathalie Becquart anakaza kusema, kwa sasa anatakiwa kutekeleza yale ambayo yameanishwa kwenye Katiba hii ya kitume! Huu ni utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, kwani wakleri, watawa na waamini walei, katika tofauti za miito na dhamana zao, lakini, wote wanafanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Sr. Nathalie Becquart anasema, ameteuwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu ambapo Shirika lake la Shirika la Tasaufi ya Kiinyasiani: “Xavière, Missionnaires du Christ Jésus” linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, Sherehe ambazo zimezinduliwa tarehe 4 Februari 2021. Karama ya Shirika inapania kujenga madaraja yanayowakutanisha watu walioko mbali na Kanisa ili kuonja wema na uzuri wa Mama Kanisa. Ni Shirika linalojielekeza zaidi kama chombo na shuhuda wa upatanisho na umoja wa udugu wa kibinadamu. Hii ni karama ambayo Sr. Nathalie Becquart anapenda imsaidie katika kutekeleza dhamana na majukumu yake katika kunafsisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa!

Sr. Nathalie
11 February 2021, 15:01