Tafuta

Vatican News
Monsinyo Janusz Urbanczyk amewaambia wajumbe wa OSCE kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwawezesha wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa amani na utulivu duniani. Monsinyo Janusz Urbanczyk amewaambia wajumbe wa OSCE kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwawezesha wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa amani na utulivu duniani.  (ANSA)

Vatican: Wanawake Wawezeshwe kiuchumi Kujenga Amani & Utulivu!

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanazingatia uhuru wa mtu katika mambo ya kiuchumi kuwa ni tunu msingi na haki ya mtu isiyoweza kuondolewa ambayo inapaswa kulindwa. Kila mtu anayo haki ya kushiriki katika mchakato wa maboresho ya shughuli za kiuchumi, kwa kutumia haki yake ya ubunifu. Wanawake wanapaswa kuwezeshwa kiuchumi ili kushiriki katika ujenzi wa amani. Wanawake

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Monsinyo Janusz Urbańczyk, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Shirikisho la Usalama na Ushirikiano Barani Ulaya, OSCE, hivi karibuni akichangia mada kwenye maandalizi ya Mkutano wa 29 wa OSCE kuhusu Uchumi na Jukwaa la Mazingira, amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuragibisha: usalama, utulivu na maendeleo fungamani ya binadamu, kwa kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanazingatia uhuru wa mtu katika mambo ya kiuchumi kuwa ni tunu msingi na haki ya mtu isiyoweza kuondolewa ambayo inapaswa kuenziwa na kulindwa. Kila mtu anayo haki ya kushiriki katika mchakato wa maboresho ya shughuli za kiuchumi, kwa kutumia haki yake ya ubunifu.

Ni wajibu na dhamana ya Nchi wanachama wa OSCE kuhakikisha kwamba watu wote wanashiriki kwa haki na usawa katika soko la ajira, ikiwa kama wanakidhi sifa na vigezo vinavyotakiwa bila ubaguzi. Ili kuweza kufikia lengo hili, kuna haja kwa watu kuwa na majiundo ya taaluma husika. Hatua ya pili ni kuhakikisha kwamba, watu wote wanapewa ujira sawa kwa kazi sawa bila ubaguzi, ili wote waweze kushughulikiwa katika hali ya usawa na haki. Kuhusu masuala ya kazi, familia inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwa sababu ustawi, maendeleo na uchumi wa leo na kesho wa Jumuiya ya Kimataifa unategemea kwa kiasi kikubwa familia.

Kazi na familia ni chanda na pete, zinategemeana na kukamilishana ili kulinda na kudumisha utu, heshima na maendeleo fungamani ya binadamu. Mahusiano na mafungamano haya yakiboreshwa, hapana shaka kwamba, jamii pia itaweza kuboreka zaidi. Kazi na familia ni tunu zenye kiwango cha hali ya juu, kiasi kwamba, kazi inapaswa kujielekeza zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia katika ujumla wake. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kukumbuka kwamba, kuna kazi nyingi zinazofanywa na wanawake ambapo hazilipwi ujira hata kidogo na wala hazitambuliwi katika mfumo rasmi wa uchumi, lakini ni kazi ambazo zinachangia sana katika ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia.

Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika malezi na makuzi ya watoto wao; wanaendelea kuwasaidia na kuwahudumia wazee na wagonjwa na kwa hakika, wanawake wanatoa mchango mkubwa katika ustawi wa jamii. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na mafanikio makubwa katika ujenzi wa usawa kati ya wanawake na wanaume maeneo ya kazi. Lakini bado kuna tofauti kubwa ya mishahara kati ya wanawake na wanaume kwenye kazi ile ile moja sehemu mbali mbali za dunia. Hali hii inajionesha pia hata katika masuala ya Bima na Usalama wa Kijamii. Haya ni mambo yanayopaswa kuvaliwa njuga kwa sasa na kwa siku za usoni.

Wanawake
17 February 2021, 14:44